Habari za Punde

Serikali ya Awamu ya Nane Ina Dhamira ya Dhati Matumizi Endelevu ya Bahari na Rasilimali Zake Ili Kujenga Uchumi kwa Taifa.

 

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akihutubia na kulifungua Kongamani la Uchumi wa Buluu kwa Maendeleo ya Kijamii Kiuchumi na Uhifadhi Mazingira Zanzibar, lililofanyika katika ukumbi wa Hoteli ya Verde Mtoni Jijini Zanzibar, lililoandaliwa na Taasisi ya Uongozi.  

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la MapinduziDk. Hussein Ali Mwinyi amesema kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Awamu ya Nane ina dhamira ya dhati ya kupanua wigo wa matumizi endelevu ya bahari na rasilimali zake ili kujenga uchumi imara kwa Taifa.

Dk. Mwinyi ameyasema hayo leo huko katika ukumbi wa Hoteli ya Verde nje kidogo ya Jijini la Zanzibar wakati akifungua Kongamano la siku moja lililobeba  mada “Uchumiwa Buluu kwa Maendeleo ya Kijamii, Kiuchumi  na Uhifadhi wa Mazingira Zanzibar”.

Katika maelezo yake Rais Dk. Mwinyi alieleza kuwa bado kuna fursa, faida na vipaumbele vya uwekezaji zaidi chini ya Uchumi wa Buluu kama vile katika sekta za uvuvi mdogo mdogo, uvuvi wa bahari kuu, ufugaji samaki na mazao ya bahari.

Alizitajas Sekta nyengine kuwa ni ukulima wa mwani, ujenzi wa miundombinu ya kimkakati ya usafiri baharini, zikiwemo bandari, viwanda vya kusindika samaki, uchimbaji wa mafuta na gesi, pamoja na shughuli za utalii wa fukwe na michezo ya baharini.

Rais Dk. Mwinyi alisema kuwa maamuzi hayo ya uwekezaji zaidi katika uchumi wa bahari yamefanikiwa kwa kutambua uwezo na mchango wa maliasili na rasilimali za pwani na baharini zinazozunguka visiwa vidogo vidogo.

Aliongeza kuwa katika kuhamasisha matumizi endelevu ya bahari katika uzalishaji na upatikanaji wa ajira kwa Wazanzibari, Serikali imejipanga kikamilifu kuhakikisha kwamba inafanikiwa katika kutekeleza azma hiyo.

Alisema kuwa sekta ya uvuvi ni muhimu kwa maendeleo ya Zanzibar lakini hata hivyo bado haijawanufaisha Wazanzibari wengi.

Hivyo, kupitia dhana hii ya uchumi wa Buluu, Serikali inafanya jitihada za dhati za kuendeleza uvuvi wa bahari kuu na tayari mipango ya kununua vyombo vitakavyotumika kwenye aina hii ya uvuvi imekamilika.

Alisisisitiza kwamba Serikali itaendelea kutekeleza zoezi la kuwapatia wavuvi vyombo vya kisasa na mahitaji kwa ajili ya kukuza na kuimarisha masoko ya samaki yaliyopo na kujenga mapya na hili linakwenda sambamba na ujenzi wa viwanda vya kusindika samaki kwa ajili ya kuuza ndani na nje ya Zanzibar.

“Ni jambo la busara taasisi za Serikali zinazoshughulikia Uchumi wa Buluu na Uvuvi zishirikiane na taasisi binafsi katika kutekeleza mipango mikakati iliyojiwekea na ambayo tayari imeidhinishwa na Baraza la Wawakilishi”,aliongeza Dk. Mwinyi.

Rais Dk. Mwinyi alisema kuwa kwa  upande wa zao la mwani Serikali imeanza ujenzi wa kiwanda cha kusarifu mwani huko Chamanangwe Pemba, ni dhahiri kwamba kiwanda hicho kinahitaji kwa wingi malighafi ya mwani na kueleza haja ya kuongeza uzalishaji.

Aidha, Rais Dk. Mwinyi alitumia fursa hiyo kutoa wito kwa Wizara ya Utalii, taasisi za Serikali, sekta binafsi na wananchi wote kushajihisha utalii endelevu utakaomgusa kila Mzanzibari na hivyo, kuchangia juhudi za kuimarisha uchumi na kupunguza umasikini.

Akieleza kuhusu sekta ya mafuta na gesi, Rais Dk.Mwinyi alieleza kuwa Serikali inaendelea kuzikaribisha Kampuni za mafuta na gesi asilia zenye dhamira njema ya kuwekeza kwenye sekta hiyo hapa nchini.

Aidha, pamoja na taratibu za kisheria na tafiti za muda mrefu za kitaalamu, lazima kuharakishwe utekelezaji wa suala la mafuta na gesi asilia ili wananchi wafaidike na rasilimali za nchi yao.

Sambamba na hayo, Rais Dk. Mwinyi alisemakuwa utekelezaji wa dhana ya Uchumi wa buluu hautawezekana buila ya kuwa na bandari za kisasa na zenye ufanisi wa hali ya juu, hivyo ndie iliyopelekea Serikali ya Awamu ya Nane kufikiria kujenga bandari kubwa katika maeneo ya Mangapwani.

“Ni matumaini yangu kwamba kukamilika kwa bandari hii ya kisasa kutakuwa ni suluhisho la kudumu la changamoto nyingi zinazojitokeza sasa katika bandari yetu ya Malindi na hivyo ajira nyingi zitapatikana na hatimae Uchumi wa nchi yetu utaimarika zaidi’,alisema Dk. Mwinyi.

Pamoja na hayo Rais Dk. Mwinyi alisema kuwa utekelezaji wa dhana ya uchumi wa Buluu lazima uende sambamba na Dira ya Zanzibar ya 2050, Mkakati wa Utekelezaji pamoja na Sera mpya ya Uchumi wa Buluu.

Hata hiyo, Rais Dk. Mwinyi alieleza matumaini yake kwa Wizara zinazohusika, sekta binafsi, washirika wa maendeleo na wananchi kwa ujumla watashirikiana vyema katika kufanikisha utekelezaji wa dhana hii kwa lengo la kukuza maendeleo ya kiuchumi na kijamii ndani ya Zanzibar.

Nae Waziri wa Uchumi wa Buluu na Uvuvi Abdulla Hussein Kombo alieleza kuwa  hivi sasa Zanzibar imekuwa katika gumzo la kitaifa,kikanda na kimataifa  kutokana na mchakato wa Uchumi wa Buluu aliouanzisha tokea wakati wa Kampeni.

Alisema kuwa kwa sasa huwezi kuuzungumza Uchumi wa Buluu hapa Tanzania na Afrika ya Mashariki na sehemu nyenginezo kwa jumla bila ya jina la Dk. Hussein Ali Mwinyi.

Kadari Singo ambaye ni Afisa wa Taasisi ya Uongozi ambayo ndiyo iliyoandaa Kongamano hilo alieleza namna Taasisi hiyo ilivyoamua kufanya Kongamano hilo hapa Zanzibar huku akitumia fursa hiyo kueleza dhima ya Kongamano hilo.

Nao Viongozi kutoka Mashirika ya Maendeleo yakiwemo UNDP, UNEP pamoja na UN WOMENwalieleza azma yao ya kuendelea kuiunga mkono Zanzibar katika kufikia ndoto yake ya kutekeleza Uchumi wa Buluu kwa manufaa ya Taifa na wananchi wake.

Akitoa mada kuu ya Uchumi wa Buluu, Profesa Joseph Semboja ambaye pia ni Mtafiti Mwandamizi kutoka taasisi ya Uongozi alieleza kuwa   ili kufikia malengo yaliyowekwa na Dira ya 2050 ni muhimu kukawa na mkakati wenye uhalisia.

Alitumia fursa hiyo kueleza maana ya uchumi shindani na ushindani na kusisitiza kwamba ushindani ni ushindani wa soko la uchumi shindani ni tija hivyo, ndio maana kuna sisitizwa kwamba uchumi wa Buluu uwe uchumi shindani.

Alisema kuwa uchumi shindani unazalisha mali zaidi, unaongeza viwango vya maisha vya Wazanzibari, unaleta faida zaidi kwa muwekezaji awe mtu binafsi au serikali, ambapo pia, inaifanya serikali ipate faida zaidi kwa uwekezaji wake, unaleta utulivu na uvumilivu wakati wa mtikisiko wa uchumi ambapo pia, unalinda uchumi wa ndani.

Sambamba na hayo, Profesa Semboja alisema kuwa iwapo Zanzibar inataka kuimarisha uchumi wake ni lazima ikaweka kipaumbele kwenye uchumi shindani, na kusema kuwa Mapinduzi ya Kiuchumi ni yale yenye tija.

Alieleza mambo mawili ya kuzingatia katika kutengeneza mikakati ya uchumi shindani ikiwa ni pamoja na kufanya tathmini ya hali halisi ya mambo yalivyo na mambo yatakayoathiri utekelezaji wa mkakati huo na sehemu ya pili kutengeneza mkakati.

Pia, alieleza umuhimu wa kuvitumia vivutio vya kitalii vilivyo hapa Zanzibar ikiwa ni njia moja wapo ya kuimarisha uchumi wa Buluu.

Viongozi mbali mbali vyama vya siasa na Serikali walihudhuria akiwemo Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar Hemed Suleiman Abdullah, Spika wa Baraza la Wawakilishi Zubeir  Ali Maulid na viongozi wengine wakiwemo Mabalozi wadogo wanaoziwakilisha nchi zao hapa Zanzibar pamoja na viongozi wa sekta binafisi na Mashirika.

Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar

Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 

 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.