Wanabodi wa Emerson Zanzibar Foundation/Wakfu wa Emerson, tumepokea kwa huzuni taarifa kwamba Mwenyeenzi Mungu amemhitaji Mzee wetu Bwana Haji Gora Haji leo Jioni. Karibuni Mzee Gora alizidiwa na kulazwa hospitali ya Bububu.
Inakisiwa marehemu alikuwa na miaka 88. Ameacha watoto, wajukuu na vitukuu. Kesho Ijumamosi, saa 7 Mchana tunamsindikiza Mzee wetu kisiwani Tumbatu, kulikozikwa kitovu chake.Twawapa mkono ukoo wa Mzee Haji Gora. Na mzee wetu azidi kumrehemu. Amin.
Niliwahi kusikia Mzee Haji Gora alipokwenda Holland kutongoa mashairi, mwandishi wa khabari akamuuliza vipi hujishajiisha na kupata raghba ya kutunga mashairi. Mzee Haji Gora akajibu ‘’..Majaaliwa ya Mwenyeenzi Mungu’’. Mwandishi wa Khabari huyo hakuelewa jibu la Mzee Gora. Akaripoti Waswahili hawana/hawaelewi ‘’inspiration’, yaani ushajiishwaji. Jibu la Mzee Haji Gora lilikuwa sahihi.
Kwani uhai wake Mungu almijaalia kipaji na kujipatia sifa nyinigi zenye herufi ya “Mim”: Mtungaji mashairi, mwandishi, mwanafalsfa n.k. ambazo ziliwavutia wengi. Mmoja wapo wa washabiki wake wakubwa alikuwa Hayati Emesrons Dewey Skeens, mwekezaji wa hoteli na mwanzilishi wa Wakfu wa Emerson Zanzibar Foundation.
Hivyo, Mwaka 2015 kulizinduliwa kijitabu cha Kiingereza chenye mashairi kumi na mbili ya Mzee Haji Gora, pamoja na tawasifu yake ndogo. Kijitabu hicho kilitayarishwa na Said el Gheithy na Bi. Judith Ridell kutangaza ushairi wa Marehemu Mzee Haji Gora kwa wageni wasiojuwa Kiswahili wanaofikia hoteli za Emerson.
Uzinduzi huo ulifanikiwa sana. Vile vile mwaka 2016, Wakfu wa Emerson Foundation ukagharimia kuhariri, kuchapicha na kusambaza maelezo aliyoyakusanya Bwana Ally Saleh na kutoa kitabu alichokiita Maisha ya Haji Gora, Msanii atayedumu milele. Kufuatana na mkataba wake na Mfuko wa Emerson Foundation Mzee Haji Gora anapata pesa zote za vitabu vikiuzwa.
Marehemu ni Mbobezi wa fani yake, mithili ya Shakespeare, yule mwanaliterati mashuhuri wa Uingereza aliyeishi Karne ya 19. Wote hawa hawakujaaliwa kwenda chuo kikuu. Lakini uandishi wa wabobezi hawa unasomeshwa vyuo kikuu.Hakika tumeondokewa. Lakini alotuachia Mzee Haji Gora ni urithi mkubwa.
Said el-Gheithy
Mwenyekiti
No comments:
Post a Comment