Habari za Punde

Ufaransa na Tanzania Zatiliana Saini Mkopo wa Shs.Bil.362 Kujenga Mradi wa Umeme wa Jua Mkoani Shinyanga.

 
Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango na Mlipaji Mkuu wa Serikali, Bw. Emmanuel Tutuba na Bi. Stephanie Mouen Essombe Mkurugenzi Mkuu Shirika la Maendeleo la Ufaransa (AFD) nchini Tanzania, wakisaini  hati za  mkataba wa mkopo wa masharti nafuu wenye thamani ya Euro milioni 130, sawa na shilingi bilioni 361.71 kwa ajili mradi wa kujenga mitambo ya kuzalisha umeme wa jua. Kushoto wanaoshuhudia ni Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Maendeleo la Ufaransa (AFD) nchini Tanzania Bi. Stephanie Mouen Essombe, Wanaoshuhudia nyuma ni Bw. Joguet Vicent Mratibu wa Miradi ya Nishati wa AFD na Bi. Loveness Msechu Mwanasheria Wizara ya Fedha na Mipango, Jijini Dodoma.

Na: Josephine Majura WFM Dodoma

Serikali ya Ufaransa kupitia Shirika lake la Maendeleo la Ufaransa (AFD), imeipatia Serikali ya Tanzania mkopo wa masharti nafuu wenye thamani ya Euro milioni 130, sawa na shilingi za Tanzania bilioni 361. kwa ajili ya kugharamia mradi wa ujenzi wa mitambo ya kuzalisha umeme wa jua.

 

Mkataba wa makubaliano ya msaada huo umesainiwa Jijini Dodoma na Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Emmanuel Tutuba, kwa niaba ya Serikali ya Tanzania na Balozi wa Ufaransa nchini Tanzania Mhe. Bw. Frederic Clavier Pamoja na Mkurugenzi Mkazi wa Shitrika la Maendeleo la Ufaransa (AFD) Bi. Stepanie Mouen Essombe, kwa niaba ya Serikali ya Ufaransa.

 

Akizungumza wakati wa kusainiwa kwa Mkataba huo, Bw. Tutuba alisema kuwa mkopo huo utatumika kujenga mitambo ya kuzalisha umeme-jua kiasi cha Megawatt 50 katika Wilaya ya Kishapu, mkoani Shinyanga.

 

“Ni matumiani yangu kwamba AFD wataridhia kutupatia fedha kwa ajili ya kutekeleza awamu ya pili ya mradi huo iliyopangwa kuzalisha Megawatt nyingine 100 ili kuweza kufikia kiwango cha uzalishaji kilichokusudiwa cha Megawatt 150”, alisisitiza Bw. Tutuba.

 

Alisema kuwa Shirika la Maendeleo la Ufaransa lilitoa pia msaada wa Euro milioni 7 kwa ajili ya kufanya upembuzi yakinifu wa mradi ambao utatekelezwaji wake utaanza Mwezi Machi 2022 hadi Machi mwaka 2023.

 

Bw. Tutuba alisema kuwa faida za mradi huo utaongeza uhakika wa upatikanaji wa nishati ya umeme  na kuiwezesha TANESCO kutimiza malengo yake ya kuzalisha umeme kupitia vyanzo mbalimbali kupitia nishati jadidifu, utapunguza utegemezi wa umeme wa nguvu za maji na kuzalisha umeme wa ziada utakao tumika majira ya ukame.

 

“Sehemu ya mkopo  uliosainiwa  utatumika kufanya maboresha na kuimarisha Grid ya Taifa ili kuifanya ya kisasa ili kupunguza upotevu wa umeme” aliongeza Bw. Tutuba

 

Bw. Tutuba aliishukuru Serikali ya Ufaransa kwa kuipatia Serikali ya Tanzania mkopo huo kwani utasaidia upatikanaji wa umeme wa uhakika ambapo utachochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi katika Mkoa wa Shinyanga na maeneo mengine nchini.

 

Kwa upande wake Balozi wa Ufaransa hapa nchini, Mhe. Bw. Frederic Clavier, alisema kuwa Serikali yake itaendelea kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo ili kuhakikisha Mpango wa Taifa wa Tatu wa Maendeleo wa Miaka Mitano (2021/22 – 2025/26 unafikia malengo yake.

 

Mhe. Clavier alifafanua kuwa kukamilika kwa mradi huo kutaifanya Tanzania kushika  nafasi ya 2 kwa ukubwa Afrika Mashariki katika uzalishaji wa umeme wa nguvu ya jua na kuifanya TANESCO kuwa na umeme wa uhakika kutoka katika chanzo rafiki wa mazingira.

 

Naye Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Maendeleo la Ufaransa (AFD) Bi. Stephanie Mouen Essombe, alisema kuwa kati ya mwaka 2016 na 2020, Ufaransa imetoa zaidi ya Euro bilioni 6 kwa ajili ya Miradi ya Nishati sawa na shilingi za Tanzania trilioni 17 ambapo kati ya fedha hizo shilingi trilioni 2.8 zimetumika kwenye miradi ya umeme-jua.

 

Alisema kuwa kukamilika kwa mradi huo wa Umeme-Jua mkoani Shinyanga utaiwezesha TANESCO kuzuia zaidi ya tani 43,460 za hewa ya ukaa na kuchangia jitihada za Serikali ya Ufaransa za kuhifadhi mazingira duniani.

 

“Katika kipindi cha mwaka 2020, Ufaransa imetoa misaada na mikopo yenye thamani ya Euro milioni 330 sawa na shilingi za Tanzania bilioni 932 na kwamba kusainiwa kwa kiasi kingine cha Euro milioni 130, kutaifanya jumla ya mikopo yenye masharti nafuu inayotolewa na Ufaransa kupitia shirika lake kufikia Euro 580 sawa na sh. Tril. 1.6.

 

Alisema kuwa mwaka huu, Shirika lake linaandaa mkakati ama mpango mpya wa namna ya kushirikiana na Serikali katika kutekeleza miradi mbalimbali ya kimkakati ikiwemo hifadhi ya mazingira na kilimo endelevu kwa upande wa Tanzania Bara na Tanzania Visiwani, miradi ambayo imewasilishwa kwenye Bodi ya Wakurugenzi ya Shirika hilo.

 

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Ugavi wa Umeme (TANESCO) Mhandisi Dkt. Titto Mwinuka, kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, alisema kukamilika kwa mradi huo utachangia kufikia lengo la Taifa la upatikanaji wa umeme kufikia Megawatt 5,000 kufikia mwaka 2025.

 

Aliongeza kuwa mradi huo utasaidia kuwa na mchanganyiko wa vyanzo mbalimbali vya nishati kwa sababu lengo la Serikali ni kuwa na vyanzo vingi vya nishati ikiwemo maji, nyuklia na jua.

 

Dkt. Mwinuka aliahidi kusimamia kikamilifu mradi huo ili ikuhakikisha unakamilika kwa wakati ili kufikia lengo lililokusudiwa.

Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango na Mlipaji Mkuu wa Serikali, Mhe. Bw. Frederic Clavier, Balozi wa Ufaransa nchini Tanzania, wakisaini   mkataba wa mkopo wa masharti nafuu wenye thamani ya Euro milioni 130, sawa na Shilingi bilioni 361.71 kwa ajili ya mradi wa kujenga mitambo ya kuzalisha umeme wa jua. Wanaoshuhudia ni Bw. Joguet Vicent Mratibu wa Miradi ya Nishati wa AFD na Bi. Loveness Msechu Mwanasheria Wizara ya Fedha na Mipango, Jijini Dodoma.

Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango na Mlipaji Mkuu wa Serikali, Bw. Emmanuel Tutuba na  Balozi wa Ufaransa nchini Tanzania Mhe. Frederic Clavier, wakibadilishana hati za mkataba wa mkopo wa masharti nafuu wenye thamani ya Euro milioni 130, sawa na Shilingi bilioni 361.71 kwa ajili mradi wa kujenga mitambo ya kuzalisha umeme wa jua, katika hafla iliyofanyika Jijini Dodoma.

Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango na Mlipaji Mkuu wa Serikali, Bw. Emmanuel Tutuba na Mkurugenzi Mkuu Shirika la Maendeleo la Ufaransa (AFD) nchini Tanzania Bi. Stephanie Mouen Essombe, wakibadilishana hati za mkataba wa mkopo wa masharti nafuu wenye thamani ya Euro milioni 130, sawa na Shilingi bilioni 361.71 kwa ajili mradi wa kujenga mitambo ya kuzalisha umeme wa jua, katika hafla iliyofanyika Jijini Dodoma.

Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango na Mlipaji Mkuu wa Serikali, Bw. Emmanuel Tutuba na Bi. Stephanie Mouen Essombe Mkurugenzi Mkuu Shirika la Maendeleo la Ufaransa (AFD) nchini Tanzaniawakionesha hati za mkataba wa mkopo wa masharti nafuu wenye thamani ya Euro milioni 130, sawa na Shilingi bilioni 361.71 baada ya kusainiwa, kwa ajili ya mradi wa kujenga mitambo ya kuzalisha umeme wa juakatika hafla iliyofanyika Jijini Dodoma.

Baadhi ya Wataalam kutoka Shirika la Ugavi wa Umeme nchini (TANESCO) pamoja na baadhi ya maafisa wa Wizara ya Fedha na  MIpango, wakiwa katika tukio la kusainiwa kwa Mkataba wa mkopo nafuu wa zaidi ya shilingi bilioni 361.7 kwa ajili ya mradi wa kujenga mitambo ya kuzalisha umeme wa juaMegawati 150 wilayani Kishapu mkoani Shinyanga, kati ya Tanzania na Ufaransa kupitia Shirika lake la Maendeleo la AFD, Jijini Dodoma.

Kamishna wa Idara ya Fedha za Nje Wizara ya Fedha na Mipango Bi. Sauda Msemo na Kamisha Msaidizi wa Idara hiyo Bw. Melkizedeck Mbise, wakifuatilia kwa makini tukio la kusainiwa kwa Mkataba wa mkopo wenye masharti nafuu wenye thamani ya sh. bilioni 361.71 uliotolewa na Ufaransa kwa ajili ya mradi wa umeme-jua utakaotekelezwa wilayani Kishapu mkoani Shinyanga, tukio hilo limefanyika Jijini Dodoma.

(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Wizara ya Fedha na Mipango – Dodoma)


No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.