Habari za Punde

Asasi za Kiraia Pemba Waipongeza TAMWA -Zanzibar Kwa Juhudi Zake.


WADAU wa masuala ya usawa wa kijinsia kutoka Asasi za Kiraia Pemba wamekipongeza Chama Cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania, Zanzibar (TAMWA ZNZ) kwa juhudi zake za kupigania na kuhamasisha haki ya usawa kwa wanawake kushiriki katika nafasi za uongozi na siasa visiwani Zanzibar.

Wametoa pongezi hizo kisiwani Pemba wakati wa mkutano wa kujadili hali ya utekelezaji wa mradi wa kuwawezesha Wanawake kushiriki katika nafasi za Uongozi na Siasa (WPEL) unaotekelezwa na TAMWA ZNZ kwa kushirikiana na shirika la UN Women.

Akitoa maoni juu ya utekelezaji wa mradi huo, Dina Juma Makota kutoka jumuiya ya PEGAO, alisema kupitia mradi huo wanawake visiwani Zanzibar wamefanikiwa kujifunza na kuongezewa ujasiri wa kujitokeza kushiriki kugombania nafasi mbalimbali za uongozi katika ngazi tofauti.

“Mradi huu umefanikiwa sana  …kubadili na kuimarisha ujasiri wa wanawake kwani matokeo tumeyashudia wakati wa uchaguzi mkuu uliopita wanawake wengi walijitokeza katika vyama vyao. Na hata wale ambao hawakufanikiwa kupata nafasi hizo wamepata kujifunza na kuongeza uthubutu wa kusimama kugombania nafasi ya uongozi inapotokea wakati wowote,” alisema Dina.

Nae Ali Shapandu kutoka Wilaya Micheweni alisema uwepo wa mradi umesaidia kubadili baaadhi ya dhana potofu za wanajamii waliokuwa hawaamini katika uwezo wa wanawake katika uongozi.

Alisema, “mfano kule kwetu Micheweni kwa muda mrefu jamii ilikuwa haiamini kama mwanamke anaweza kuwa kiongozi, na ilikuwa ni vigumu sana kuona mwanamke anajitokeza kugombea, lakini mabadiliko tumeanza kuyaona tangu 2015 tulikuwa na wawakilishi wanawake, lakini zaidi tumeona kwenye uchaguzi 2020 wanawake wengi walijitokeza na hatimaye kwa mara ya kwanza mmoja akafanikiwa kushinda uwakilishi wa Jimbo la Konde ambaye yule ni matunda yenu TAMWA ZNZ.”

Amina Omar mmoja wa wadau hao akigusia kuhusu changamoto zinazowakabili wanawake katika uongozi alisema licha ya mwitikio mkubwa walioupata wanawake kutaka kushiriki katika nafasi za uongozi lakini bado uwepo wa rushwa ya pesa na ngono kwa wanawake ni kikwazo kikubwa kufikia malengo yao.

“Wanawake kikwazo kikubwa ambacho kinatukabili kwasasa ni uwepo wa rushwa. Kuna rushwa za aina mbalimba lakini hasa hii rushwa ya ngono na Pesa ni mtihani sana kwakweli kwetu na sijui tufanyeje ili tuepukane nah ii,” alisema,

Kwa upande wake, Ali Khamis Kombo alisema, “wanawake wafanyakazi wa serikali wanaojitokeza kugombea nafasi za uongozi kupitia vyama vya upinzani maranyingi baada ya uchaguzi wanapitia misukosuko kwenye ajira zao jambo ambalo linawarudisha nyuma kwa kuogopa kupoteza ajira zao,”

Mapema afisa ufuatiliaji na tathimini wa TAMWA ZNZ, Moh’d Khatib aliwataka wadau hao kuendelea na jukumu la kutoa elimu na kyhamasisha zaidi jamii ili lengo la usawa wa kijind=sia katika vyombo vya maamuzi liweze kufikiwa.

Mkutano huo wa kujadili hali ya utekelezaji wa mradi wa kuwawezesha Wanawake kushiriki katika nafasi za Uongozi na Siasa (WPEL) unaotekelezwa na TAMWA ZNZ kwa kushirikiana na shirika la UN Women uliwashirikisha wadau kutoka asasi za kiraia  kisiwani Pemba.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.