Na Kassim Abdi, OMPR
Jamii Nchini imetakiwa kutoa taarifa kwa mamlaka husika kwa kuwafichua watu wanaojihusisha na vitendo haramu dhidi ya dawa za kulevya.
Makamu wa Pili wa Rais Mhe. Hemed Suleiman Abdulla alieleza hayo baada ya kutekeleza ibada ya sala ya Ijumaa alijumuika na waumini katika mskiti wa Tunduni uliopo Wilaya ya Kati Unguja.
Alisema viongozi wa Dini wana nafasi kubwa ya kukemea vitendo viovu ikiwemo kupiga vita matumizi ya dawa za kulevya jambo linalosababisha athari hasa kwa rika la vijana.
Mhe. Hemed alieleza kuwa, suala la uwingizaji, usambazaji na utumiaji wa dawa za kulevya katika jamii halikubaliki na linapaswa kupigwa vita na kila mtu bila kujali tofauti zozote zile za kisiasa, Kiimani au kimaeneo.
Akizungumzia juu ya takwimu za watu wanaotumia madawa ya kulevya Makamu wa Pili wa Rais alisema kwa sasa Zanzibar ina watu takribani Elfu Kumi (10,000) wanajihusisha na matumizi ya dawa za kulevya kitendo ambacho kinaashiria miaka kumi ijayo kila nyumba Zanzibar itakua na mtumiaji wa dawa hizo jambo ambalo halitoi picha nzuri kwa kizazi cha baadae.
Alieleza katika kudhibiti kadhia hiyo serikali ina mpango wa kubadilisha sheria haraka iwezekanavyo ili kuwabana wale wote wanaojihusisha na vitendo hivyo sambamba na kuchukuwa hatua kali zitakazotoa fundisho kwa kila mmoja anaeshiriki.
“Nawaomba waumini na wananchi wote kwa ujumla tusimame kidete kupinga madawa ya kulevya Zanzibar” Alisema Makamu wa Pili
Akigusia juu ya maradhi ya Covid -19 Mhe. Hemed alitaka jamii kuendelea kuchukua tahadhari juu ya maradhi hayo kwa kufuata miongozo na maelekezo kutoka kwa watalamu wa Afya nchini ikiwemo kuepuka mikusanyiko isiokuwa ya lazima.
Alifafanua kwamba, Jamii imeshuhudia athari zitokanazo na ugonjwa wa Corona kupitia mataifa mbali mbali duniani hivyo kuna haja ya wazanzibar kujilinda kwa nguvu zote ili kuepuka athari za ugonjwa huo.
Nae, Khatibu katika mskiti huo Sheikh Hassan Sleyum aliwakumbusha waumi kuwa kitu kimoja kwa kudumisha umoja na mshikamano miongoni mwao ili kufuata kwa vitendo mafundisho ya dini ya kislamu pamoja na kuunga mkono maelekezo yanayotolewa na viongozi wakuu wa nchi katika mustakbali wa kuwaletea maendeleo wananchi wake.
No comments:
Post a Comment