Habari za Punde

SMZ Yaishauri Kamati ya Zanzibar International Marathon Kutanua Wigo.

 

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Othman Masoud Othman akifanyiwa usajili wa kushiriki Mbio za Zanzibar International Marathon na Mwakilishi wa Benki ya NMB Ndg. Mkubwa  Omar Mohammed, Benki ya NMB ni Mdhamini wa Zanzibar International Marathon kwa mwaka 2021, usajili huo umefanyika katika Ofisi yake Migombani Jijini Zanzibar. 

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe.Othman Masoud Othman akizungumza na Mabalozi na Kamati ya Zanzibar International Marathon walipofika Ofisini kwa mazungumzo na kumfanyia usajili wa kushiriki Mbio za Zanzibar Marathon zinazotarajiwa kufanyika 18, Julai Zanzibar. mazungumzo hayo yamefanyika Ofisini Kwake Migombani Jiji Zanzibar. 

Na.Mwandishi wa OMKR Zanzibar.
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mheshimiwa Othman Masoud Othman, ameyasema hayo leo (Julai 8) wakati akizungumza na Kamati ya Mashindano ya Mbio, Zanzibar International Marathon, waliofika ofisini kwake Migomba mjini Zanzibar kwa lengo la kujitambulisha na kueleza dhamira yao juu ya mashindano hayo.
 
Mbali na kuonesha furaha yake kwa hatua hiyo muhimu ya kusimamia mashindano hayo, Mheshmiwa Othman amewasihi  waandaaji kuiboresha na kuiendeleza zaidi ikiwemo kuibadilisha Kamati hiyo na kuwa taasisi ili kuweza kufanya mambo makubwa zaidi kwa jamii ya Zanzibar na pia kuepuka kusambaratika.
 
"Dunia hivi sasa ina ushindani mkubwa, ukiwemo wa kiuchumi. Mashindano haya ya Zanzibar International Marathon yatapelekea kulitangaza jina la Zanzibar kimataifa na kuzalisha wawekezaji na fursa nyengine zaidi za kiuchumi mbali na utalii", alisema Makamu huyo wa Kwanza wa Rais. 
 
Aidha, Mheshimiwa Othman ameeleza kwamba changamoto kubwa iliyopo katika nchi zinazoendelea ni amani na usalama, hivyo uwepo wa mashindano makubwa kama hayo kwa Zanzibar, ni kichocheo cha ujenzi wa amani katika visiwa hivi.
 
Mheshimiwa Othman amewataka waandaaji wa mashindano hayo kuwa wabunifu zaidi ili kuweza kuwasaidia vijana wenye vipaji katika kupambana na soko la ajira na kuwaepusha kujihusisha na makundi yasiyofaa yakiwemo ya kihalifu.
 
Naye Balozi wa Zanzibar International Marathon, Bwana Farouk Karim, amesema mashindano hayo yatafanyika tarehe 18 Julai na yatawakutanisha zaidi ya wananchi 3,000, wakiwemo viongozi mbalimbali wa kiserikali na taasisi binafsi na pia wafanyabiashara.
 
Kwa upande wake, mwakilishi kutoka Benki ya NMB, ambayo ni miongoni mwa wadhamini wa mashindano hayo, Ndugu Mkubwa Omar Muhamed, amesema  wameingia kuwa wadhamini ili kuungana na juhudi za serikali za kukuza uchumi pamoja na kuitangaza Zanzibar kimataifa.

Mashindano hayo yatafanyika katika mkoa wa Mjini Magharibi Unguja.

 *Kitengo cha Habari*
*Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar*


No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.