Waziri wa Nishati Mhe. Dkt. Medard Kalemani akiwasisitiza wananchi wa wilaya Chato kuchangamkia fursa ya ujenzi wa bomba la mafuta litakalojengwa kutoka Hoima nchini Uganda hadi Chongoleani Tanga -Tanzania wakati wa Mkutano wa wananchi na wadau kuhusu fursa za Mradi wa Ujenzi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki tarehe 10 Agosti, 2021 Mkoani Geita.
Baadhi ya washiriki wa Mkutano wa wananchi na wadau kuhusu
fursa za Mradi wa Ujenzi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki uliofanyika tarehe 10 Agosti, 2021 mkoani Geita
wakifuatilia kwa makini hotuba ya Waziri
wa Nishati Mhe. Dkt. Medard Kalemani (Hayumo pichani) wakati wa mkutano huo.
Na Dorina Makaya –
Chato, Geita.
Serikali ya Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania imetoa kiasi cha shilingi bilioni 259.96 kwa ajili ya
utekelezaji wa Mradi wa Bomba la Mafuta.
Hayo yameelezwa na
Waziri wa Nishati, Mhe. DKt. Medard Kalemani wakati akizungumza na wananchi wa
Kata ya Bukome, Kijiji cha Nyakato, Wilayani Chato Mkoani Geita tarehe 10
Agosti, 2021.
Waziri Kalemani
amewataka wananchi hao kuchangamkia fursa mbalimbali za ujenzi wa bomba la
mafuta litakalopita katika mikoa 8 ya Kagera, Geita, Shinyanga,Tabora, Singida,
Dodoma, Manyara na Tanga.
Waziri Kalemani
amezitaja fursa hizo kuwa ni pamoja na usafirishaji, ulinzi, chakula, vinywaji,
huduma ya malazi na mafuta kwa ajili ya magari na mitambo. Amezitaja fursa
nyingine kuwa ni pamoja na shajala, bidhaa za ujenzi zinazopatikana hapa
nchini, shughuli za ujenzi, huduma za mawasiliano na ukodishwaji wa mitambo ya
ujenzi.
Dkt. Kalemani
ameeleza kuwa Jumla ya shilingi bilioni 28 zinategemea kulipwa kwa wananchi
waliopitiwa na bomba la mafuta kutoka Hoima nchini Uganda hadi Chongoleani
Tanga nchini Tanzania.
Aidha, Waziri
Kalemani amesema, mradi wa ujenzi wa Mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi utaanza
kutekelezwa ifikapo Septemba 2021.
Akizungumza kwa niaba
ya Mkuu wa Mkoa wa Geita, Rosemary Senyamule, Mkuu wa Wilaya ya Chato Martha
Mkupasi amewataka wananchi kutunza miundombinu ya bomba la mafuta ambayo
itapita kwenye maeneo yao.
No comments:
Post a Comment