Habari za Punde

*Elimu Zaidi Itolewe Juu ya Umuhimu wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar. - Mhe. Masoud.*

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe.Othman Masoud Othman akikabidhiwa mpango mkakati wa uanzishwaji wa miradi yenye lengo la kuunga mkono serikali ya umoja wa kitaifa katika jumuiya yao. akikabidhiwa na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wanawake wenye Ulemavu Zanzibar.Bi.Salma Haji Saadat, wakati walipofika Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais Migombani kwa mazungumzo.

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Othman Masoud Othman akizungumza a Uongozi wa Jumuiya ya Wanawake wenye Ulemavu Zanzibar (JUWAUZA) walipofika Ofisi kwake Migombani Jijini Zanzibar kwa mazungumzo.

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe.Othman Masoud Othman akiwa katika picha ya pamoja na Uongozi wa Jumuiya ya Wanawake wenye Ulemavu Zanzibar JUWAUZA, baada ya kumaliza mazungumzo yao yaliofanyika katika Ofisi ya Makamu wa Rais Migombani Jijini Zanzibar.

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Othman Masoud Othman, amesema Jumuiya na taasisi mbali mbali zilizopo nchini, zina nafasi kubwa ya kuendelea kutoa taaluma kwa jamii juu ya umuhimu wa serikali ya umoja wa kitaifa ili kujenga maslahi mapana kwa Zanzibar. 

Ameyasema hayo wakati alipokutana na Uongozi wa Jumuiya ya Wanawake wenye Ulemavu Zanzibar JUWAUZA, uliofika ofisini kwake Migombani Mjini Unguja kwalengo la  kujitambulisha pamoja na kuelezea mpango mkakati wa uanzishwaji wa miradi yenye lengo la kuunga mkono serikali ya umoja wa kitaifa katika jumuiya yao.

"Ni muhimu sana kuwaelimisha wanajamii juu ya umuhimu na faida za uwepo wa Serikali ya Umoja wa kitaifa, kwani bado jamii ya waliowengi wameshindwa kuelewa lengo na umuhimu wa kuwepo kwake" alieleza Makamu huyo wa Rais

Amesema kutolewa kwa elimu hiyo kutaendelea kukuza uhusiano mwema uliopo katika jamii pamoja na kujenga misingi imara kwa kizazi kijacho hali itakayoendelea kuifungua Zanzibar hasa katika upande wa sekta ya uwekezaji.

Akitoa tahadhari juu ya kutumika kwa vijana katika kuvunja amani Mhe. Othman alisema "Mara nyingi katika ghasia na uvunjifu wa amani kisiasa, vijana ndio wanaosukumwa na kuwekwa mstari wa mbele.Huu sio urithi mzuri tunaowaachia, tunatakiwa tuwajenge katika umoja na mshikamano,kwa mustakbali wao na taifa kwa ujumla". 

Aidha, Mhe. Othman ameipongeza Jumuiya hiyo kwa kuanzisha mradi huo ambao utatoa manufaa makubwa kwa nchi katika upande wa kukuza umoja na mshikamano kwa wananchi. 

Amewaahidi kuwa serikali itaendelea kuunga mkono mradi huo pamoja na miradi itakayoanzishwa na jumuiya nyengine ili kuleta maendeleo katika nchi. 

Hata hivyo ameuhimiza uongozi wa Jumuiya hiyo kutumia vyema fursa wanazozipata, kwa lengo la kupanua wigo katika utekelezaji wa miradi mbali mbali itakayoinyanyua jumuiya yao.

Mbali na hayo Mhe. Othman akawasisitiza juu ya haja ya kushirikiana na taasisi mbali mbali zilizopo nchini ikiwemo zinazohusika na usalama barabarani ili kuandaa mikakati itakayowasaidia kupunguza ajali za barabarani ambazo ndio chanzo kikubwa cha Walemavu nchini.

Akitoa maelezo juu ya mradi wa “SISI NI WA MOJA” ambao upo ndani ya jumuiya hiyo, Afisa ufuatiliaji tathmini na mafunzo, Ndugu Suleiman Baitani, amesema mradi huo una lengo la kutoa taaluma kwa wananchi juu ya umuhimu wa serikali ya umoja wa kitaifa pamoja na kufahamisha nafasi ya mwananchi katika serikali hio, hali itakayosaidia kujenga jamii yenye maridhiano.

Amesema mradi huo utahusisha majimbo sita, mawili kwa upande wa kisiwa Cha Pemba na Manne kwa Unguja, ikiwa ni kuunga mkono juhudi za pamoja katika Kukuza Amani iliyopo nchini.

Jumuiya ya Wanawake wenye Ulemavu ni miongoni mwa Jumuiya zisizokuwa za kiserikali iliyoanzishwa mwaka 2008 ikiwa na lengo la kutetea haki za wasichana na wanawake wenye ulemavu nchini.

*Kitengo cha Habari*
*Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar*

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.