Habari za Punde

KARANI WA SENSA ATAKAYETOA SIRI KUFUNGWA MIAKA MIWILI, FAINI MIL 10

Mtakwimu Mkuu wa Serikali, Dkt. Albina Chuwa akifafanua jambo wakati wa mkutano na wadau wa Mkoa wa Dodoma wa kuhamasisha na kutoa elimu juu ya sensa ya watu na makazi.

Na Richard Mwaikenda, CCM Blog Dodoma

KARANI yeyote wa Sensa atakayetoa siri  ya mtu wakati wa Sensa ya Watu na Makazi atashitakiwa na kuhukumiwa kulipa sh. mil. 10 au kufungwa miaka miwili ama vyote kwa pamoja.

Adhabu hiyo imeelezwa na Mtakwimu Mkuu wa Serikali, Dkt. Albina Chuwa wakati wa mkutano na wadau wa Mkoa wa Dodoma wa kuhamasisha na kutoa elimu juu ya sensa ya watu na makazi.

"Uzuri sheria iko wazi kwa kosa hilo, hivyo si vizuri kwa karani wa sensa ambaye amepewa mafunzo yakiwemo ya maadili ya kutunza siri za anaowahoji halafu akafanya vinginevyo," amesema Dkt. Chuwa.

Dkt. Chuwa ameamua kujibu hivyo baada  mmoja wa wadau wa mkutano huo, Mwenyekiti wa Baraza la Wazee wa Mkoa wa Dodoma, Mchungaji Petro Mpolo kuelezea hofu waliyonayo kwa baadhi ya makarani wa sensa kutoa siri walizohojiwa jambo ambalo alidai linasababisha  wengi wao kusita kueleza ukweli.

Mkutano huo wa wadau ulioitishwa na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Sensa ya Mkoa huo, Anthony Mtaka ulihudhuriwa na Spika wa Bunge, Job Ndugai.

Wengine ni Kamishna wa Sensa, Spika mstaafu, Anne Makinda, wabunge wa mkoa huo, wakuu wa wilaya, viongozi wa dini, viongozi wa vyama vya siasa, viongozi wa mabaraza ya wazee na taasisi mbalimbali wakiwemo watu wenye ulemavu.

Sensa ya Watu na Makazi kufanyika Agosti 2022 ambapo uzinduzi utafanywa na Ris wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan Makao Makuu ya Nchi Dodoma.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.