Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe.Othman Masoud Othman akiwa katika ziara yake Kisiwani Pemba akichuma karafuu.
Waziri wa Biashara na Viwanda na Maendeleo ya Viwanda Zanzibar Mhe.Omar Said Shaban akizungumza na wakulima wa zao la karafuu wakati wa ziara ya Makamu wa Kwanza wa Rais Mhe.Othman Masoud Othman kisiwani Pemba.
Waziri wa Kilimo Umwagiliaji Maliasili na Mifugo Mhe.Dkt. Soud Nahoda Hassan akizungumza na Wakulima wa zao la karafuu kisiwani Pemba wakati wa ziara ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Othman Masoud Othman Kisiwani Pemba.
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Othman Masoud Othman, amesema Serikali ipo katika mpango wa kuisimamia biashara ya karafuu ili kuleta tija kwa serikali na wakulima wa zao hilo.
Ameyasema hayo leo (Agost 11) wakati alipofanya ziara ya kutembelea mashamba ya mikarafuu yaliyopo Kichunjuu, Mkoa wa Kusini, pamoja na Mgogoni, Mkoa wa Kaskazini Pemba, kwa lengo la kusikiliza matatizo yanayowakabili wakulima wa zao hilo.
Mhe. Othman amesema kwa muda mrefu zao la karafuu limepoteza uhalisia wake hasa katika uzalishaji, jambo ambalo kwa kiasi limekuwa likiwarudisha nyuma wakulima hasa katika kujinyanyua kiuchumi.
"Awali Zanzibar ilikuwa ikizalisha hadi kufikia kilo elfu ishirini za karafuu lakini sasa wakulima wamekuwa wakizalisha wastani wa kilo elfu tisa tu. Mabadiliko haya yanatokana na kukosekana kwa miundombinu bora kwa wakulima na hivyo kusababisha kupungua kwa idadi ya karafuu inayofika katika soko la dunia,” alifafanua Makamu huyo wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar.
Akigusia juu ya Shirika la Biashara la Taifa la Zanzibar (ZSTC), Mhe. Othman amesema bado kumekuwa na tatizo kubwa kwa shirika hilo hasa katika utoaji wa miche ya mikarafuu, ambayo bado haimnufaishi mkulima katika kuendeleza ukulima wa zao hilo.
Hata hivyo, amewahakikishia wakulima kuwa Serikali itaendelea kuwasimamia katika kuwatatulia matatizo yanayowakabili kupitia mpango unaotaka kuwekwa, ambao utakuza zaidi biashara ya karafuu na kukuza soko lake duniani.
Kwa upande wake, Waziri wa Biashara na Maendeleo ya Viwanda, Mhe. Omar Said Shaaban, amesema katika kuhakikisha uzalishaji wa karafuu unakuwa katika ubora nchini, Wizara hiyo ina mpango wa kuandaa mkutano na wadau wa karafuu kwa lengo la kuandaa muelekeo mpya wa kisera na mageuzi katika uendelezaji wa zao hilo.
"Kutokana na mabadiliko ya soko la karafuu, serikali inaendelea kupanga bei ambazo zitakuwa ni mkombozi kwa wakulima pamoja na kuandaa mazingira rafiki kwa lengo la kukuza uzalishaji wake nchini", alifafanuwa Mhe. Omar
Naye Waziri wa Kilimo, Dk. Soud Nahoda Hassan, akizungumzia sifa ya karafuu jambo ambalo limekuwa tatizo kubwa kwa wakulima, amesema Wizara kwa kushirikiana na wakulima inaangalia namna ya kuliweka sawa jambo hilo kwa lengo la kuona tatizo hilo linaondoka na wanafaidika.
Aidha alisema Serikali ipo katika mpango wa kuwapa mashamba wakulima hao ambapo kwa sasa Wizara ya Ardhi inaendelea na zoezi la upimaji wa ardhi kwa ajili ya ugawaji huo.
Nao wakulima hao wameiomba serikali kuwatatulia matatizo wanayokabiliana nayo ikiwemo suala la bei ya karafuu, miche pamoja na uharakishaji wa malipo wakati wanapofanya mauzo yao.
*Kitengo cha Habari*
*Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar*
No comments:
Post a Comment