Baadhi ya Waandishi wa habari wakiskiliza Ufafanuzi uliyotolewa na Naibu Katibu Mkuu kutoka Chama cha Walimu Zanzibar (ZATU) Salim Ali Salim (hayupo pichani) juu ya tukio lilotokea katika Skuli ya Sunni Madrasa iliyopo Mkunazi Mkoa wa Mjini Magharibi hafla iliyofanyika katika Ofisini za Chama hicho Kijagwani Zanzibar.
Picha na Maryam Kidiko – Maelezo Zanzibar.
Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Mhe Simai Mohammed Said ametoa agizo la kuwasimamisha kazi Walimu wote walioshiriki kuwaadhibu watoto kinyume na kanuni elekezi hadi uchunguzi utakapo kamilika.
Mhe Simai ametoa agizo hilo kufuatia Mwalimu Suleiman Mohamed Suleiman kumuadhibu Mwanafunzi kinyume na utarabu wa adhabu kwa Mwanafunzi pamoja na kutoa taarifa katika vyombo vya habari taarifa zisizo na ukweli.
Mhe Simai ameyasema hayo wakati wa mkutano wa pamoja na watendaji wa Skuli ya Sunni Madressa na Wazazi huko Mkunazini Mjini Unguja.
Amesema kumpiga mtoto si njia sahihi ya kumfunza bali zipo njia mbadala ambazo anaweza kuelekezwa kwa mujibu wa taratibu za adhabu mbadala kwa watoto na akawa mtoto mwema.
Aidha Mhe Simai amempa agizo Mrajis wa elimu kufanya uhakiki wa leseni za Walimu wote hasa wa Skuli binafsi na kuwachukulia hatua wale wote watakaobainika kukosa sifa za ualimu.
Amesema kuna baadhi ya Walimu wanafanya kazi bila ya kuthibitishwa na kupewa leseni na hivyo kufanya kazi kinyume na maadili na taratibu za fani hiyo.
Akizungumzia suala la watoto walio na umri mdogo kuendesha vyombo vya moto hasa wanapokwenda Skuli, Mhe. Simai amewataka wakuu wa Skuli binafsi kulikemea suala hilo kwani linaleta athari kubwa hasa wanapopata ajali.
Pia Mhe Sjmai amezitaka Skuli zote za binafsi kuhakikisha wanajiunga na chama cha wamiliki wa Skuli binafsi ili kuondosha baadhi ya malalamiko yanayozikabili Skuli hizo, kupitia umoja wao.
Nae Mrajis wa Elimu Wizara ya Elimu Zanzibar bi Zuwena Mataka amesema sheria ya elimu ina miongozo na kanuni zake ambazo zinaelekeza juu ya adhabu mbadala hivyo kila mwalimu hana budi kuzifuata sheria na kanuni hizo.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa jumuiya ya Skuli binafsi bwana Feisal Mohamed Said amesema lengo la kuwekwa jumuia hiyo ni kushirikiana na kusaidiana katika mambo mbali hasa ya kitaaluma pamoja na kutatua changamoto zinazozikabili Skuli za binafsi.
No comments:
Post a Comment