Habari za Punde

Wanufaika mradi wa viungo wapatiwa mafunzo ya usindikajiWanufaika wa mradi wa VIUNGO visiwani Zanzibar wameanza kupatiwa mafunzo ya usindikaji wa mboga mboga na uongezaji wa thamani kwa bidhaa wanazozalisha,ikiwa ni awamu ya kwanza ya mafunzo hayo ya usindikaji kupitia mradi huo.

 

Utolewaji wa mafunzo hayo umekuja ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa mradi kwa lengo la kuwajengea uwezo wanufaika wa mradi kujijenga zaidi kiuchumi ikiwemo kuanzisha biashara kutokana na mazao wanayozalisha.

 

Akitoa mafunzo hayo Afisa kilimo kupitia mradi wa Viungo Salma Nassor Marshed alisema lengo la mafunzo hayo ni kuwawezesha wakulima kusindika mazao yao ili kukabiliana na uhaba wa masoko na kwamba sasa wataweza kuhifadhi mazao hayo bila kuharibika.

 

Alisema usindikaji huo pia utaongeza lishe kwa akina mama na watoto kwani wataweza kutumia mboga mboga zilizosindikwa  hata wakati wa kiangazi.

 

Sambamba na hayo alisema usindikaji huo pia utaongeza thamani ya fedha kwani mkulima ataweza hifadhi bidhaa alizosindika hata wakati wa kiangazi ambao matunda na mboga nyingi huadimika.

 

Kwa upande wake Afisa lishe kupitia mradi huo Witness William alisema mafunzo ya usindikaji wa mboga mboga  yatawafikia walengwa zaidi ya elfu tano kutoka wilaya kumi  za mradi VIUNGO Unguja na Pemba.

 

Alisema wanufaika wa mafunzo hayo watakua na jukumu la kuwafundisha wengine ili walio wengi zaidi waweze kunufaika na elimu hio kwa maslahi ya wote.

 

Akifafanua kuhusu umuhimu wa usindikaji alisema wanufaika wataweza kuimarisha afya za familia zao, sambamba na kukuza kipato chao kwa kuingiza fedha zitakazotokana na mauzo ya bidhaa zao.


Kwa upande wao baadhi ya wanaufaika wa mafunzo hayo walisema yamekuja wakati sahihi ambao wakulima wengi walikosa njia sahihi za kuhifadhi mazao yao.

 

Walisema kwa muda mrefu wamekua wakishindwa kufahamu njia bora za usindikaji wa mazao na kufanya kilimo chao kuwa cha muda maalumu na pindi wakati wa kiangazi unapofika hawakua na hata hakiba ndogo ya mboga mgoga na matunda.

 

Mradi huu wa Viungo visiwani hapa unatekelezwa na PDF kwa mashirikiano ya TAMWA-ZNZ pamoja na CFP chini ya ufadhili wa umoja wa Ulaya kwa muda wa miaka minne.

 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.