Habari za Punde

WAZIRI MKUU AOMBOLEZA KIFO CHA MWL. KASHASHA

Na.Irene K. Bwire

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ametuma salamu za rambirambi kwa familia na wapenzi wa soka nchini kutokana na kifo cha mchambuzi maarufu wa soka, Mwalimu Alex Kashasha (64) kilichotokea wiki iliyopita jijini Dar es Salaam.

 

Mwalimu Kashasha ambaye alifikwa na umauti wakati akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Kairuki, alikuwa mchambuzi mahiri wa mchezo wa soka kwenye televisheni ya Taifa (TBC1).

 

“Atakumbukwa kwa ustadi wake wa kuchambua mechi za soka mubashara pamoja na vipindi vya maelezo ya mechi za soka za ndani na nje ya nchi,” amesema Waziri Mkuu.

 

“Ninawaomba wanafamilia na wapenzi wa michezo tuendelee kumuombea ili apumzike kwa amani. Tutaendelea kuenzi mchango wake katika kukuza vipaji vya michezo hapa nchini.”

 

“Mwalimu Kashasha ambaye alikuwa ni kati ya walimu wazuri wa mchezo wa soka nchini, ameacha pengo kubwa kwenye tasnia ya michezo kama mwalimu na kwa watu wengi waliopita kwenye mikono yake,” amesema Waziri Mkuu.

 

Amezikwa jana kwenye makaburi ya Kinondoni, jijini Dar es Salaam.

 

IMETOLEWA NA:

OFISI YA WAZIRI MKUU,

JUMATATU, AGOSTI 23, 2021.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.