Habari za Punde

Waziri Mkuu Mhe.Kassim Majaliwa Azindua Kiwanda cha Kuchambua Pamba *Awataka wakulima waongeze mashamba kutokana na uwepo wa soko la uhakika

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Kassim Majaliwa amezindua kiwanda cha kuchambua pamba cha Kampuni ya NGS Investment Ltd na kuwataka wakulima watumie fursa ya uwepo wa kiwanda hicho kwa kuongeza mashamba kwa sababu kinawapa uhakika wa soko la zao hilo.

Pia, Waziri Mkuu amesema Serikali itaendelea kuajiri watumishi katika sekta ya kilimo na kuwasambaza kwenye maeneo mbalimbali nchini hususan ya vijijini kwa ajili ya kuwasaidia wakulima kuweza kulima mazao yao kwa kufuata mbinu bora za kilimo na kuongeza tija.

 

Waziri Mkuu amezindua kiwanda hicho leo (Alhamisi, Agosti 26, 2021) kilichopo katika kijiji cha Ifukutwa wilaya ya Tanganyika mkoani Katavi. Amesema zao la pamba ni miongoni mwa mazao ya kimkakati, hivyo Serikali itaendelea kulisimamia katika hatua zote.

 

Amesema mbali na kiwanda hicho kutoa soko la uhakika kwa wakulima wa pamba pia manufaa mengine ni kwa wananchi wanaoishi katika maeneo yanayozunguka kiwanda kupata ajira za moja kwa moja na za muda, hivyo kupunguza tatizo la ukosefu wa ajira.

 

Mheshimiwa Majaliwa amesema Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan amedhamiria kuinua uchumi wa nchi kwa kuendeleza ujenzi wa miundombinu ili itumike na wananchi kusafirisha mazao na kusambaza bidhaa mbalimbali.

 

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya NGS, Njalu Silanga amesema ujenzi wa mradi wa kiwanda hicho ulianza Januari 2020 na unatarajiwa kugharini Dola za Marekani milioni mbili sawa na shilingi bilioni 4.5.

 

Mkurugenzi huyo amesema kuwa kiwanda hicho kinauwezo wa kuchakata tani 50,000 za pamba kwa msimu mmoja ila uzalishaji wa pamba katika mkoa wa Katavi bado uko chini ikilinganishwa na uwezo wa kiwanda kutokana na upatikanaji wa pamba ghafi.

Awali, Waziri Mkuu alitembelea shamba la mikorosho la Jumanne Karegere lenye ukubwa wa ekari 40 na mikorosho 1,080 ambapo aliuagiza uongozi wa Halmashauri ya wilaya ya Tanganyika ukutane na mkulima huyo kwa ajili ya ufuatiliaji wa mara kwa mara wa zao hilo.

Waziri Mkuu alisema kwa kuwa zao la korosho ndio linaanza kulimwa katika mkoa huo ni vema wakaweka utaratibu wa kuwapeleka wakulima katika vituo vya utafiti wa kilimo kwa lengo la kuwafanya wakulima hao kulima kwa tija.

Naye, mmiliki wa shamba hilo Karegere aliishukuru Serikali kwa kuwaongezea zao lingine na yeye ni miongoni mwa wakulima walionufaika kwa kupewa miche ya mikorosho bure.

IMETOLEWA NA:

OFISI YA WAZIRI MKUU,

ALHAMISI, AGOSTI 26, 2021.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.