Habari za Punde

*MAKINDA AVUTIWA NA MICHENJELE*

 
Na Mwandishi wetu Mihambwe


Spika Mstaafu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye pia ni Kamisaa wa Sensa Tanzania Bara Mhe. Anne Semamba Makinda  amevutiwa na hamasa waliyonayo wakazi wa kata ya Michenjele juu ya sensa ya makazi kwani hakutarajia hali hiyo.

Mhe. Makinda ameyasema hayo wakati akiwahutubia wakazi wa Kijiji cha Bandari kilichopo kata ya Michenjele ambapo amewapongeza namna walivyohamasika na wanavyoshirikiana na Viongozi wa Serikali.

"Wakati nakuja nilijua nitawakuta wakazi wa Kijiji cha Bandari pekee lakini ajabu wakazi karibu wa kata nzima mmekuja, ni ishara ya upendo, ushirikiano na mpo tayari kwa zoezi la majaribio ya sensa ya Watu na Makazi" Alisema Mhe. Makinda.

Mhe. Makinda aliwaelezea bahati ya kipekee waliyoipata wakazi wa Kijiji cha Bandari kwenye zoezi hili la majaribio ya sensa ya Watu na Makazi.

"Ni jambo la heri kwa mkoa mzima, Kijiji cha Bandari kilichopo kata ya Michenjele Tarafa ya Mihambwe zoezi la majaribio ya sensa ya Watu na Makazi yanafanyika. Lengo la sensa si kujua idadi tu bali pia kujua mahitaji ya sasa ya Wananchi, hii ni sensa ya maendeleo." Alisisitiza Mhe. Makinda.

Akizungumza kwa niaba ya Wakazi wa Tarafa ya Mihambwe, Afisa Tarafa Mihambwe Emmanuel Shilatu alimuomba Mhe. Makinda afikishe salamu za shukrani kwa Rais Samia kwa upendo wake mkubwa kwa Watanzania.

"Kwa niaba ya Wakazi wa Tarafa Ya Mihambwe tunaomba ufikishe salamu zetu za pongezi, upendo na shukrani kwa Rais Samia kwa kuonyesha uhodari, umakini, uzalendo wa kuwatumikia Watanzania wote pasipo ubaguzi. Tunamuhaidi ushirikiano wa kulijenga Taifa letu nyakati zote." Alisema Gavana Shilatu.

Zoezi la majaribio 2021  linafanyika kwenye mikoa 18 Tanzania na kimkoa zoezi linafanyika Kijiji cha Bandari kilichopo kata ya Michenjele Tarafa ya Mihambwe.

Hili ni zoezi la majaribio ya sensa ya Watu na Makazi ili kujiridhisha namna zoezi litakavyoweza kufanyika kwa ufanisi zaidi mwaka 2022 wakati zoezi lenyewe kitaifa.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.