Habari za Punde

Balozi wa Denmark Nchini Tanzani Bi Mette Amefurahishwa na Jitihada za Pamoja za Kupambana na Vitendo vya Udhalilishaji wa Kijinsia kwa Wanawake na Watoto Visiwani Zanzibar.

Naibu Balozi wa Denmark Nchini Tanzani Mette  Bech Pilgaard  akizungumza na baadhi ya wanamitandao ya kupinga udhalilishaji kutoka maeneo tofauti Zanzibar,mkutano huo ulifanyika Shehia ya Mwanakwerekwe mjini Unguja.
Baadhi ya wanamitandao ya kupinga udhalilishaji kutoka mkoa wa kusini na kaskazini Unguja wakifuatilia taarifa katika mkutano huo.
Meneja wa miradi TAMWA-ZNZ Ally Muhammed (kulia)akiwakaribisha maafisa ubalozi wa Denmark Nchini Tazania wakati walipofanya ziara katika shehia ya Mwanakwerekwe mjini Unguja kwa lengo la kuzungumza na wanamitandao ya kupinga udhalilishaji.
Mkurugenzi wa TAMWA-ZNZ Dkt,Mzuri Issa akiwakaribisha maafisa hao wa Ubalozi walipotembelea ofisi za Chama hicho Tunguu Wilaya ya kati Unguja.

Na Muhammed Khamis,TAMWA-ZNZ,

Naibu Balozi wa Denmark Nchini Tanzani Bi  Mette  Bech Pilgaard  ameleza kufurahishwa kwake na jitihada za  pamoja za kupambana na vitendo vya udhalilishaji wa kijinsia kwa wanawake na watoto visiwani Zanzibar zinazofanywa  na TAMWA-ZNZ kwa kushirikiana na wadau wengine mbali mbali.

Ameyasema hayo wakati alipokua akizungumza na baadhi ya wahanga wa matukio ya udhalilishaji visiwani hapa na mitandao ya kupinga udhalilishaji katika shehia ya Mwanakwerekwe mjini Unguja kufuatia ziara maalumu ya kutazama utekelezaji wa mradi huo wa miaka mitatu.


Alisema kupitia uwasilishwaji wa taarifa ambazo zimetoka kwa wazazi ambao ni waathirika wa matukio ya udhalilishaji ni dhahiri kuwa kuna kazi kubwa ambayo imefanyika kwenye jamii ikiwemo kuibadili mtazamo na hatimae kutoa mashirikiano mazuri katika ufuatiliaji wa kesi tofauti za udhalilishaji.


Alisema inapendeza na kutia moyo kuona baadhi ya watendaji wa makossa ya udhalilishaji wanaingizwa hatiani na kuhukumiwa bila shaka kuna kazi kubwa ambayo imefanywa na inapaswa kuthaminiwa na kila mmoja katika mapambano hayo.


Sambamba na hilo Naibu Balozi huyo aliwataka wanamtandao wa kupambana na udhalilishaji na wanahabari maalumu ambao wanafanya kazi ya kuripoti taarifa hizo kutokata tamaa badala yake waendelee kuwa msaada kwa wengine kwa lengo la kupata jamii bora.


Wakitoa ushuhuda baadhi ya wazee ambao ni waathirika wa matukio ya udhalilishaji mmoja miongoni mwao alisema kupitia elimu aliopatiwa na wanamtandao wa kupinga udhalilishaji ilimfanya kuwa jasiri na kutorudi nyuma.


Alisema alifuatilia kesi hio kwa ukaribu sana kupitia msaada aliopatiwa na wanamitandao hao na baadhi ya maafisa kutoka TAMWA-ZNZ ambao mara baada ya kesi yake kusikilizwa kwa muda mrefu hatimae aliemtendea kosa hilo mtoto wake alihukumiwa kwenda chuo cha mafunzo miaka 30.


Mzazi mwengine alisema kupitia mafunzo waliofanyiwa na TAMWA-ZNZ mtoto wake alijenga ujasiri mkubwa wa kutoa ushahidi Mahakamani na kilichobakia sasa kwenye kesi hio ni utolewaji wa hukumu tu na anaamini kuwa haki itatendeka.


Kwa upande wao baadhi ya waandishi wa habari walioshiriki kwenye mradi huo waisema awali walikutana na mazingira magumu ya jamii kukubali kutoa taarifa lakini kupitia elimu waliosambaza hatimae waliweza kusimama imara na kuwafichua watendaji wa kadhia hio.


Akiwasilisha ripoti ya utekelezaji wa mradi huo  Afisa ufuatiliaji na tathmini Mohamed Khatib alisema katika miaka yote mitatu ya utekelezaji wa mradi huo juhudi mbali mbali zilifanyika ikiwemo za utowaji wa elimu kwa jamii kuhusu udhalilishaji wapatao 35,700 ambapo kwa upande wa Unguja ni 19,635 na Pemba 16,065.


Akiendelea kufafanua zaidi Afisa huyo alisema katika kipindi chote cha miaka mitatu ya utekelezaji wa mradi huo kesi zipatazo 1377 ziliriripotiwa katika vituo mbali mbali vya polisi na kuzifuatilia na  idadi kubwa ya kesi hizo zilikua ni za kubaka ambazo ni 403 na kwa upande wa kesi  zilizopatiwa hukumu zilikua ni kesi 163 na kesi ambazo zipo vituo vya polisi ni 581,mahakamani  198 na kesi zilizofutwa kwa sababu mbali mbali ni 92.


Alisema kuripotiwa kwa kesi hizo katika maeneo mbali mbali ya Unguja na Pemba kunatokana na ujasiri waliojengewa wanajamii katika maeneo yao ambapo awali watu wengi walikua wakishindwa kuripoti wanapofanyiwa matendo hayo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.