Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali
Mwinyi, amesema kuwa ujenzi wa majengo mapya ya Hospitali ni lazima uendane na
uwepo wa vifaa vya kisasa.
Hayo aliyaeleza leo mara baada ya kufika na kupata maelezo ya ujenzi wa jengo jipya la wodi ya wanawake na watoto linalojengwa katika eneo la hospitali ya Chake Chake, iliyopo Mkoa wa Kusini Pemba.
Katika
maelezo yake, Rais Dk. Mwinyi alisema kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar,
itahakikisha kuwa baada ya kumalizika kwa ujenzi huo kunakuwepo vifaa vitakavyoendana
na jengo hilo jipya.
Alisema
kuwa mbali ya kujengwa jengo hilo ni vyema kukaangaliwa uwezekanao wa kujenga
majengo mengine ya ghorofa kutokana na mazingira ya eneo hilo.
Rais
Dk. Mwinyi alisema kuwa amefarajika na ujenzi wa Hospitali ya Chake Chake
unavyoendelea na kuahidi kutafuta fedha za ziada ili kuona kuwa ujenzi huo
unakamilika kwa wakati uliopangwa.
Alifahamisha
kuwepo kwa ujenzi huo pamoja na vifaa utapunguza changamoto wanazozipata
wananchi za kufanyiwa vipimo katika Hospitali hiyo na hatimae kusomwa katika
hospitali ya Mnazi Mmoja ama hospitali ya Muhimbili.
Alieleza
Serikali itaendelea kutatua changamoto zinazowakumba watendaji wa Wizara ya
Afya ikiwemo stahiki zao lakini aliwasihi kufanya kazi kwa uadilifu wakifikiria
kauli nzuri kwa wagonjwa ambayo pekee yake ni tiba.
Akitoa
maelezo ya ujenzi huo, Daktari dhamana wa Hospitali ya Chake Chake, Abrahman
Said Suleiman , alisema kuwa kumalizika kwa jengo hilo la wodi ya akinamama na
watoto kutaondoa matatizo mengi ikiwepo
ongezeko la Vitanda kutoka 63 vilivyoko sasa na kufikia vitanda 116.
Hata
hivyo, alisema kuwa Hospitali ya Chake Chake imekuwa ikipokea wagonjwa wengi
ikiwa ni ya pili ukiachia ya Mnazi mmoja kwani katika mwezi wa July 2020 hadi
June 2021 tayari wagonjwa 61,000 walishapatiwa matibabu hospitalini hapo.
Aliomba
baada ya kumalizika kwa Wodi hiyo ya akinamama na watoto wanaomba kupatiwa
vifaa mbali mbali vya matibabu ikiwemo mashine ya kutambua maradhi yasiyoambukiza
na mashine ya Xray.
Aidha,
Rais Dk. Mwinyi alipata fursa ya kusikiliza changamoto mbali mbali zilizotolewa
na wananchi waliofika katika eneo hilo la Hospitali ya Chake Chake.
Akitembelea
mradi wa maji katika kijiji cha Chanjaani Pemba, Rais Dk. Mwinyi alisema kuwa
miongoni mwa vipaumbele vya Serikali ni kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya
maji safi na salama kwa uhakika ambalo ni suala muhimu kwa wanaadamu.
Alieleza
kuwa Serikali itatafuta njia ya kuiwezesha ZAWA, kupata fedha za kusambazia
mabomba ya maji kwa haraka ili tatizo
walilonalo wananchi hao liweze kumalizika kwa haraka.
Akizungumzia
juu ya kero ya barabara, Rais Dk. Mwinyi alisema kuwa hivi sasa kuna
makubaliano na kampuni ya ujenzi wa bara bara
za kilomita 220 za Unguja na Pemba hivyo, aliwataka wananchi kuvuta
subira.
Akikagua
ujenzi wa barabara ya Kipapo – Mgelema, Rais Dk. Mwinyi alitowa ahadi kwa
wananchi kuwa Serikali itaimaliza ujenzi wa barabara hiyo kwa kiwango cha lami
bila ya kuchelewa.
Sambamba
na hayo, katika kuwaunga mkono wananchi wa kijiji cha Mgelema katika sekta ya
elimu na yeye kwa upande wake aliahidi kuchangia TZS. millioni 5 kwenye ujenzi
wa Skuli ya msingi ambayo tayari wananchi wenyewe wameonesha juhudi ya
kuchangishana elfu hamsini (50,000/=) kwa kila mtu , ili kukamilisha ujenzi
huo.
Mapema,
Rais Dk. Mwinyi alipokea taarifa ya Utekelezaji ya Mkoa wa Kusini Pemba huko
katika ukumbi wa Makonyo uliopo Wawi, Chake Chake Pemba.
No comments:
Post a Comment