Habari za Punde

Naibu Waziri Mhe Katambi Akabidhi Vifaa kwa Watu Wenye Ulemavu Mkoani Shinyanga.

Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Kazi, Vijana na Ajira Mhe. Patrobas Katambi akikabidhi baiskeli za magurudumu matatu kwa Makamu Mwenyekiti wa Shirikisho la Watu wenye Ulemavu Mkoa Shinyanga Bw. Mohamed Ally (aliyekaa kwenye baiskeli kushoto) na Bi. Happyness Kasembo (kulia) wakati wa hafla ya makabidhiano ya vifaa saidizi kwa watu wenye ulemavu Mkoani Shinyanga.

Na: Mwandishi Wetu – Shinyanga

Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Kazi, Vijana na Ajira Mheshimiwa Patrobas Katambi amekabidhi vifaa saidi kwa Watu wenye Ulemavu ili kuwezesha kundi hilo kushiriki katika shughuli za kiuchumi na kijamii.

Akizungumza Naibu Waziri Katambi wakati wa hafla ya kugawa vifaa saidizi kwa Watu wenye Ulemavu iliyofanyika katika Ofisi ya Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga alieleza kuwa Tanzania ni nchi yenye demokrasia imara inayojengwa kwa kufuata misingi thabiti ya kuheshimu, kutambua na kuthamini utu, usawa na haki kwa watu wote bila ubaguzi wa aina yoyote.

“Kila mtu na kila mwananchi wakiwemo Watu wenye Ulemavu wana haki sawa ya Kikatiba na Kisheria ya kushiriki kikamilifu katika mambo muhimu yanayowahusu sambamba na kupata mahitaji yao muhimu,” alisema Katambi

“Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Uongozi na usimamizi mahiri wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan imeendelea kuwajali sana wananchi na inatambua uwepo wa makundi mbalimbali katika jamii yakiwemo ya Watu wenye Ulemavu,” alieleza

Aliongeza kuwa upo umuhimu wa kutambua uwezo na mchango wa Watu wenye Ulemavu mahali popote walipo na kuweka mikakati thabiti ya kuwaendeleza na kuhakikisha ustawi wao ikiwa pamoja na kujumuishwa katika nyanja zote za kijamii, kisiasa na kiuchumi ili kuwafanya wawe na mchango zaidi katika maendeleo ya jamii zao na Taifa kwa ujumla.

“Msaada huu utawawezesha watu wenye ulemavu kushiriki katika shughuli za kiuchumi na kijamii kwani itakuwa rahisi kwao kusogea kutoka sehemu moja kwenda sehemu nyingine bila kuhitaji msaada mkubwa jambo ambalo litatoa ahueni kwa familia na wanaowategemea,” alisema

Sambamba na hayo alieleza kuwa Serikali imeandaa na kusimamia programu mbalimbali za uwezeshaji kwa watu wenye ulemavu kama vile kutenga nafasi maalum za ajira, kusisitiza uwekaji wa miundombinu rafiki katika ofisi na taasisi mbalimbali.

Aidha, Naibu Waziri Katambi alitoa shukrani kwa Kampuni ya Sigara Tanzania (TCC) na wadau wengine kwa kujitoa na kushirikiana na Serikali katika kuwahudumia Watu wenye Ulemavu.

“Nashukuru uongozi wa Kampuni ya Sigara Tanzania (TCC) kwa namna ambavyo wamekuwa wakiguswa na changamoto za watu wenye ulemavu na kuamua kutoa msaada wa baadhi ya mahitaji muhimu ikiwemo baiskeli za magurudumu matatu 10, fimbo nyeupe 60 na magongo 60,” alisema

Naye Meneja wa Kampuni ya Sigara Tanzania (TCC) Mkoa wa Shinyanga Bw. Aman Lyimo alisema kuwa wataendelea kushirikia na serikali kwa kusaidia Watu wenye Ulemavu kupitia huduma mbalimbali ambazo wanazitoa kwa jamii.

Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa Shirikisho la Watu wenye Ulemavu Mkoani Shinyanga Bw. Mohamed Ally ameishukuru Serikali kwa kuendelea kuwakumbuka na kutambua mchango wa watu wenye ulemavu kwa kuwawezesha vifaa saidizi ambavyo vitawafanya washiriki kikamilifu katika kusukuma gurudumu la maendeleo ya Taifa.

Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Kazi, Vijana na Ajira Mhe. Patrobas Katambi ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Shinyanga Mjini (kulia) akizungumza wakati wa hafla ya kukabidi vifaa saidizi kwa Watu wenye Ulemavu Mkoani Shinyanga.
Sehemu ya Washiriki wakifuatilia hotuba ya Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Kazi, Vijana na Ajira Mhe. Patrobas Katambi wakati wa hafla ya ugawaji wa vifaa saidizi kwa Watu wenye Ulemavu Mkoani Shinyanga.
Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Kazi, Vijana na Ajira Mhe. Patrobas Katambi akiwa kwenye picha ya pamoja na baadhi ya Watu wenye Ulemavu mara baada ya kukabidhi vifaa saidizi Mkoani Shinyanga.

Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Kazi, Vijana na Ajira Mhe. Patrobas Katambi akikabidhi fimbo nyeupe kwa Bw.Hassan Jumbe (asiyeoona) wakati wa hafla ya kukabidhi vifaa saidi kwa Watu wenye Ulemavu Mkoani Shinyanga.

PICHA NA OFISI YA WAZIRI MKUU

(SERA, URATIBU, BUNGE, KAZI, VIJANA, AJIRA NA WENYE ULEMAVU)

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.