Habari za Punde

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk.Hussein Ali Mwinyi Ameongoza Maziko ya Jaji wa Mahkama Kuu Zanzibar.

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekitib wa Baraza la Mapinduzi Alhja Dk.Hussein Ali Mwinyi akiweka mchanga katika kaburi la Marehemu Jaji ya Mahkama Kuu Zanzibar Haji Omar Haji, maziko yaliofanyika katika Kijiji cha Shakani Wilaya ya Magharibi ‘B’Unguja leo 12-9-2021.(Picha na Ikulu)

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk. Hussein Ali Mwinyi leo ameongoza mazishi ya Jaji wa Mahkama Kuu Zanzibar, Jaji Haji Omar Haji yaliyofanyika Shakani, Wilaya ya Magharibi ‘B’ Unguja, Mkoa wa Mjini Magharibi.

Viongozi mbali mbali walihudhuria  katika mazishi hayo akiwemo Makamo wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Othman Masoud Othman, Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar Hemed Suleiman Abdullah, Jaji Mkuu wa Zanzibar Omar Othman Makungu pamoja na viongozi wengine wa vyama vya siasa, dini na serikali, wananchi na wanafamilia.

Mapema Alhaj Dk. Mwinyi alijumuika pamoja katika hitma na sala ya kumsalia Marehemu Jaji Haji Omar Haji huko katika Masjid Noor, uliopo Kombeni, Wilaya ya Magharibi ‘B’, Mkoa wa Mjini Magharibi sala ambayo iliyoongozwa na Mufti Mkuu wa Zanzibar Sheikh Saleh Omar Kabih.

Akisoma Wasfu wa Marehemu Jaji Omar Haji, mara baada ya mazishi ya Marehmu, Mrajis wa Mahkama Kuu Zanzibar Mohamed Ali Mohamed alisema kuwa Marehemu amezaliwa Aprili 04, 1967 huko Wilaya ya Mafia katika Mkoa wa Pwani, Tanzania Bara.  

Alisema kuwa Marehemu ameanza Elimu yake ya Msingi kuanzia darasa la Kwanza hadi darasa la Saba mwaka 1978 hadi 1984 huko Mafia na mnamo mwaka 1985 alihamia Zanzibar na kujiunga katika Skuli ya Msingi Kiembesamaki kwa kuendelea na elimu yake hadi mwaka 1987.

Kwa mujibu wa maelezo ya  Mrajis wa Mahkama Kuu  Zanzibar, Mnamo mwaka 1988 hadi 1991 Marehemu alianza Elimu yake ya Sekondari katika Skuli ya Vikokotoni, na kuendelea na masomo yake ya Kidato cha Tano na Sita mnamo mwaka 1993 hadi 1995 katika Skuli ya Sekondari ya Lumumba.

Mwaka 1997 hadi mwaka 1999 Marehmu alijiunga na Chuo cha Mzumbe kwa masomo ya Stashahada ya Sheria  na mwaka  2000 hadi 2004 alijiunga na Chuo Kikuu  cha Zanzibar (ZU) na kuhitimu Shahada ya Kwanza ya Sheria na mnamo mwaka 2008 alisoma Shahada ya Uzamili ya Sheria katika Chuo Kikuu cha Stellenbosch nchini Afrika Kusini.

Akimuelezea  katika nafasi zake za kazi alizopitia Marehemu Haji Omar Haji, Mrajis wa Mahkama Kuu Zanzibar alieleza kwamba Marehemu aliwahi kuwa Mwalimu wa muda katika skuli ya Sekondari ya Haile Sellasie na mnamo Oktoba 1996 aliajiriwa kazi na kuanza akiwa Karani wa Mahkama Kuu Zanzibar.

Marehemu aliwahi kuwa Hakimu wa Mkoa katika Mahkama ya Mkoa Vuga mnamo mwaka 2005 hadi 2008 wakati akiwa Hakimu wa Mkoa alipata nafasi ya kufundisha katika Chuo cha Azania.

Marehemu Haji Omar Haji aliteuliwa kuwa Naibu Mrajis Mahkama Kuu Pemba mnamo mwaka 2009-2011 na mnamo Julai 04,2018 hadi Februari 01,2021 alifanya kazi katika Mahkama ya Afrika Mashariki akiwa ni Mtendaji Mkuu wa Mhkama hiyo.

Aidha, mmano Februari 01, 2021 Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk. Hussein Ali Mwinyi alimteua kuwa Jaji wa Mahkama Kuu Zanzibar na kuapishwa Februari 2021 na mnamo Agosti 16,2021 Jaji Mkuu wa Zanzibar Omar Othman Makungu alimteua kuwa Jaji Mkaazi Pemba.

Marehemu Haji Omar Haji, hadi umauti unamfika alikuwa ni jaji wa Mahkama Kuu Zanzibar na Jaji Mkaazi Pemba.

Marehemu Jaji Haji Omar Haji amefariki jana Septemba 11,2021 katika Hospitali ya Rufaa Manzi Mmoja baada ya kuugua kwa muda mfupi, marehemu ameacha Kizuka Mmmoja na watoto 4, Mwenyezi Mungu ailaze roho ya Marehemu mahala pema peponi, Amin.

Kitengo cha Habari

Ikulu Zanzibar.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.