
Na Mbaraka Kambona, Liwale
Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega amesema katika bajeti ya mwaka 2021/2022 Serikali itajenga bwawa la kunyweshea Mifugo lenye thamani ya Shilingi Milioni 480 katika Kijiji cha Kimambi, Wilayani Liwale, Mkoani Lindi.
Ulega aliyasema hayo Septemba 20, 2021 alipofanya ziara katika Wilaya ya Liwale, Mkoani Lindi kwa lengo la kusikiliza kero za Wafugaji na Wakulima ili kuzitatua.
Alisema ujenzi wa bwawa hilo utasaidia kutatua changamoto ya maji ambayo inawakabili wafugaji wa maeneo hayo na utasaidia pia kutatua migogoro baina yao na wakulima Wilayani humo.
"Rais Samia Suluhu Hassan anakwenda kuwajengea bwawa lenye thamani ya Shilingi Milioni 480 hapa Kimambi, ujenzi wa bwawa hilo utasaidia kuwaondosha katika migogoro," alisema Ulega
Naibu Waziri Ulega alisisitiza kuwa pesa hizo zipelekwe kufanya kazi iliyopangiwa ya ujenzi wa bwawa la kunyweshea mifugo huku akiwataka viongozi wa Wilaya hiyo kuhakikisha pesa hizo zinatumika vizuri.
Aidha, alisema kuwa Rais Samia Suluhu Hassan amewapa pia Majosho mawili katika Kijiji cha Kimambi na Kijiji cha Luwele.
"Sasa kwa sababu huku mifugo imekuwa mingi sana, Mimi nakuongezeeni Josho lingine hapa ili mifugo mingi iweze kuogeshwa ," aliongeza Ulega
Naye, Mbunge wa Liwale, Zuberi Kuchauka alitumia nafasi hiyo
kumshukuru Rais wa Awamu ya Sita, Mama Samia Suluhu Hassan kwa kuwapelekea pesa
hizo huku akisema kuwa bwawa hilo likikamilika hawatarajii tena kuona migogoro
katika Vijiji vilivyotengwa kwa ajili ya Wafugaji Wilayani humo.
- Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega akiongea na
Wafugaji na Wakulima wa Kijiji cha Kimambi, Wilayani Liwale, Mkoani Lindi
(hawapo pichani) alipofanya ziara katika Wilaya hiyo Septemba 20, 2021 kwa
lengo la kutatua kero zao. Katika ziara hiyo Ulega alisema Serikali
itajenga bwawa la kunyweshea Mifugo Kijijini hapo lenye thamani ya
Shilingi Milioni 480. Kushoto ni
Mkuu wa Wilaya ya Liwale, Judith Nguli.
- Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega (katikati) akitoa
maelekezo kwa Mkuu wa Wilaya ya Liwale, Judith Nguli (kulia) alipotembelea
kukagua eneo lililotengwa kwa ajili ya kujengwa bwawa la kunyweshea Mifugo
katika Kijiji cha Kimambi, Wilayani Liwale, Mkoani Lindi Septemba 20,
2021.
No comments:
Post a Comment