Habari za Punde

Serikali ya Rais Mhe Samia Suluhu Hassan Kuwainua Kiuchumi Wananchi wa Ruangwa.

 

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega akiongea na Uongozi wa Wilaya ya Ruangwa alipotembelea Ofisi ya Mkuu wa Wilaya hiyo, Hassan Ngoma (wakwanza kushoto) Septemba 22, 2021. Katika kikao hicho kifupi Ulega aliueleza Uongozi huo kuwa Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan imejipanga kuwainua  kiuchumi Wananchi wa Wilaya hiyo kwa kuwapelekea miradi ya ufugaji wa Kuku, Mbuzi na Samaki.
Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega akiongea na Wafugaji na Wakulima wa Kijiji cha Nangurugai Kilichopo Wilayani Ruangwa, Mkoani Lindi Septemba 22, 2021. Lengo la ziara yake hiyo ni kusikiliza kero za Wakulima na Wafugaji na kuzitatua.

Na. Mbaraka Kambona

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega amesema Serikali inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan imejipanga kupeleka miradi ya maendeleo ya  ufugaji Kuku, Mbuzi na  Samaki katika Wilaya ya Ruangwa ili iwasaidie  kuinua Uchumi wao.

Ulega aliyasema hayo  wakati akiongea na Viongozi wa Wilaya ya Ruangwa iliyopo Mkoani Lindi  Septemba 22, 2021.

Alisema kutokana na kasi kubwa ya maendeleo ya Wilaya hiyo inayochochewa na shughuli za uchimbaji madini Serikali imeona ni vyema kupeleka miradi hiyo kwa kina mama na vijana ili kukuza uchumi wao na kukidhi mahitaji ya mazao ya Mifugo katika Wilaya hiyo.

Naibu Waziri Ulega aliitaja miradi hiyo ambayo  itapelekwa katika Wilaya hiyo na kuwasaidia wakina mama na vijana ni pamoja  ufugaji wa kuku na ufugaji wa Samaki na Mradi wa Kopa mbuzi lipa mbuzi.

"Mwezi Oktoba tutaanza na Vikundi kumi, tutaleta Wilayani hapa kuku elfu mbili (2000) ikiambatana na semina ya kuelekeza namna ya kufuga kuku hao kibiashara," alisema Ulega

Aidha, Waziri Ulega alimuagiza Mkuu wa Wilaya ya Ruangwa, Hassan Ngoma kutafuta eneo zuri ambalo watalitumia kuanza kufanya ufugaji wa Samaki.

"Sasa tafuteni eneo na kikundi kimoja kizuri ili tuje kuweka shamba darasa la ufugaji wa samaki, kikundi hicho kitakuwa kinavuna Samaki hao na watawafundisha na wengine kuhusu ufugaji huo wa samaki," aliongeza Ulega

Waziri Ulega alimuahidi Mkuu wa Wilaya hiyo kuwa atapeleka wataalamu wa shughuli ya ufugaji wa Samaki ili kuwasaidia wananchi hao.

Naye, Mkuu wa Wilaya hiyo alisema kuwa kufuatia kuchipuka kwa shughuli za madini Wilayani humo kumepelekea kuongezeka kwa mahitaji mbalimbali muhimu ikiwemo mahitaji ya nyama, mayai, Samaki na maziwa ambayo mengi yamekuwa yakiagizwa katika maeneo mengine ya nchi na hivyo alimuomba Naibu Waziri kuona hizo fursa na kuwawezesha wananchi wa Wilaya hiyo ili waweze kuzitumia.


No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.