Habari za Punde

Utiaji wa Saini Ukarabati wa Skuli ya Sekondari Mtule Kusini Unguja.

Na Maulid Yussuf  -WEMA.

Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar imetiliana saini makabidhiano ya ukarabati wa Skuli ya Sekondari Mtule ilioko Paje Mkoa wa kusini Unguja.

Utiaji wa saini huo umefanyika katika maeneo ya viwanja vya Skuli hiyo, ambapo Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Bw.Ali Khamis Juma amesaini hati hizo na Mkurugenzi wa Ufundi wa kampuni ya RANS bwana Yunus Ali Gare amesaini kwa upande wa wakandarasi wa ukarabati wa majengo hayo.

Akizungumza baada ya utiaji wa saini, Katibu Mkuu bwana Ali amesema makabidhiani hayo ya matengenezo ya Skuli hiyo yanaenda sambamba na matengenezo ya Chwaka Tumbe, ambao matatizo yake yanalingana.

Amesema Serikali imefanya juhudi za makusudi kuona Skulj ambazo zinavuja kuhakikisha zinafanyiwa matengenezo makubwa ili ziweze kutumika kwa muda mrefu.

Amesema mategemeo ya Serikali baada ya kumalizika matengenezo hayo, Skuli hiyo itakuwa na mazingira mazuri na kuwa suala la kuvuja litakuwa halipo tena.

Aidha amewataka Wakandarasi wa Skuli hiyo kuhakikisha wanazingatia muda kwa mujibu waliokusudiwa ili wanafunzi waweze kuingia kwa wakati na kusoma bila ya usumbufu wa aina yeyote.

Amewahakikishia kuwa Wizara itaendelea kuwa kafibu nao ili kuhakikisha panapotokea changamoto iweze kutatuliwa kwa wakati na kuhakikisha malengo yaliyopangwa yanatimia.

Nae Mkurugenzi Mipango Sera na Utafiti Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali bwana Khalid Msoud Waziri amesema matengenezo hayo ni mpango maalum wa utekelezaji wa ilani ya CCM na ahadi za mhe Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi katika kuhakikisha anaweka mazingira mazuri katika sekta ya Elimu nchini.

Hata hivyo, Afisa Elimu Wilaya ya Kusini Unguja, mwalimu Mussa Nahoda Makame ametoa pongezi kwa Rais Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi baada ya kutembelea Skuli hiyo kwa kuona tatizo la ubovu na kuamua kutoa agizo juu ya kufanyiwa matengenezo Skuli hiyo.


Mwalimu Mkuu wa Skuli ya Sekondari Mtule mwalimu Is.haka Hamad Khatib, amesema Skuli hiyo ilikuwa katika hali mbaya kutokana na  mapaa kuvuja, hivyo amesema imani yao baada ya matengenezo hayo Skuli yao  itakuwa katika hali nzuri.


Kwa upande wake Mkurugenzi wa Ufundi wa Kampuni ha RANS bwana Yunus Ali Gare ameishukuru Wizara ya Elimu kwa kuendelea kuwaamini kwa kuwakabidhi kazi hiyo ya matengenezo ya jengo la Skuli hiyo ambapo ameahidi kumalizika kwa wakati waliokubaliana.

Amesema wamekuwa wazoefu wakubwa na Wizara kwa ujenzi wa majengo ya Skuli ambapo matarajio yao kufanya matengenezo yenye viwango yatakayodumu kwa muda mrefu, ukizingatia suala hilo ni la jamii ikiwa wao pia linawahusu.

Aidha amesema ukarabati huo utafanyika kwa kipindi cha miezi sita mpaka kumalizika kwake, huku akiahidi kutoa ushirikiano katika masuala yote yatakayojitokeza katika ukarabati huo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.