Habari za Punde

Mabalozi Wanaokwenda Kuiwakilisha Tanzania Nje ya Nchi Kuzitangaza Fursa za Kiuchumi -Dk Mwinyi.

 

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Hussein Ali Mwinyi akizungumza na Mabalozi  waliopishwa hivi karibuni kwenda kuiwakilisha Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Nchi mbali mbali walipofika Ikulu Jijini Zanzibar kwa mazungumzo na kujitambulisha leo.25/10/2021.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Hussein Ali Mwinyi (kulia) akizungumza na Mabalozi  waliopishwa hivi karibuni kwenda kuiwakilisha Jamhuri ya Muungano wa Tannzania katika Nchi mbali mbali walipofika Ikulu Jijini Zanzibar kwa mazungumzo na kujitambulisha leo (pichani wa pili kulia) Mhe.Balozi Anisa Mbega Nchini India (katikati) Mhe.Innocent Shiyo Nchini Ethiopia na (kushoto) Mhe.Togolani Mavura Nchini Korea Kusini.[Picha na Ikulu] 25/10/2021. 

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Hussein Ali Mwinyi amekutana na kufanya mazungumzo na Mabalozi wanaokwenda kuiwakilisha Tanzania nje ya nchi na kusisitiza haja ya kwenda kuzitangaza fusra za kujenga uchumi wa nchi ikiwemo Sera ya Uchumi wa Buluu ambayo ndio Dira ya uchumi wa Zanzibar.

Mabalozi ambao alikutana nao leo Rais Dk. Mwinyi Ikulu Zanzibar na kufanya nao mazungumzo ni Balozi Anisa Mbega anayekwenda kuiwakilisha Tanzania nchini India, Balozi Togolani Edriss Mavura anayekwenda kuiwakilisha Tanzania nchini Korea Kusini. na Balozi  Innocent Shiyo anayekwenda kuiwakilisha Tanzania nchini Ethiopia.

Katika mazungumzo hayo, Rais Dk. Mwinyi aliwaeleza Mabalozi hao kwamba nchi kama Korea Kusini imepiga hatua kwa kiasi kikubwa katika kuitumia bahari kama sehemu moja wapo ya kuimarisha uchumi wake ikiwa ni pamoja na kuwa na viwanda vingi vya uvuvi, bandari na viwanda vya meli hatua ambayo inaweza kusaidia katika kuendeleza Sera ya Uchumi wa Buluu kwa Zanzibar.

Aidha, Rais Dk. Mwinyi alieleza haja kwa Mabalozi hao kwenda kuitangaza Zanzibar kiutalii kutokana na vivutio vyake kadhaa vilivyopo hasa kwa nchi za Korea Kusini na India ambako bado watalii wake wanaokuja kuitembelea Zanzibar hawajawa wengi.

Rais Dk. Mwinyi aliwaeleza Mabalozi hao juhudi zinazoendelea kuchukuliwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar  katika kukuza uchumi wake kupitia ujenzi wa bandari ya kisasa ambayo itajumuisha shughuli mbali mbali ambapo pia, itahitaji wawekezaji.

Alieleza mikakati iliyowekwa katika kuhakikisha inaijengea uwezo Mamlaka ya Kukuza Uwekezaji Zanzibar (ZIPA) iweze kufanya kazi ipasavyo na kuwa kituo maalum kitakachotoa huduma zote za uwekezaji kwa muda mfupi sambamba.

Sambamba na hayo, Rais Dk. Mwinyi alieleza haja kwa Mabalozi hao kusaidia kutafuta soko kwa ajili ya zao la mwani kwa ajili ya kuwasaidia wakulima wa zao hilo sanjari na kutafuta wawekezaji kwa ajili ya kuja kuekeza katika sekta ya viwanda pamoja na gesi asilia hapa Zanzibar.

Nao Mabalozi hao kwa upande wao walimuhakikishia Rais Dk. Mwinyi kuwa juhudi za makusudi watazichukua katika kuhakikisha wanatekeleza vyema majukumu waliyopewa na kutumia fursa hiyo kutoa shukurani zao kwa Rais kutokana na maelekezo aliyowapa.

Kitengo cha Habari

Ikulu Zanzibar.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.