Habari za Punde

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe Hemed Suleiman Amekutana na Kuzungumza na Uongozi wa Chuo Cha Bima na Hifadhi ya Jamii Afrika.

Mwenyekiti Mtendaji wa Chuo cha Bima na Hifadhi ya Jamii Afrika Dk. Baghayo Saqware akimkabidhi Zawadi Maalum Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla wakati alipofika Afisini kwake Vuga kukitambulisha Chuo Chao.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla akizungumza na uongozi wa Chuo cha Bima na Hifadhi ya Jamii Afrika waliofika Afisini kwake Vuga kujitambulisha na kubadilishana nae mawazo.

Na.Kassim Abdi.OMPR.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla ameuhakikishia uongozi wa Chuo cha Bima na Hifadhi ya Jamii Afrika kuwa serikali ya Mapinduzi Zanzibar itaendelea kutoa ushirikiano wake katika kufanikisha azma ya kufungua chuo chao hapa Zanzibar.

Mhe. Hemed alileza hayo wakati akizungumza na viongozi wa chuo hicho waliofika Afisini kwake Vuga kwa ajili ya kujitambulisha na kubadilishana nae mawazo.

Makamu wa Pili wa Rais aliupongeza uongozi wa chuo hicho, kwa kuja na maono ambayo yanadhihirisha uwezo mzuri waliokuwa nao katika kuisaidia jamii ya Watanzania.

Alifafanua kuwa, ujio wa chuo hicho kutasaidia kwa kiasi kikubwa kuitangaza Zanzibar sambamba na kutoa fursa kwa wazanzibar kupata huduma mbali mbali ikiwemo fursa za ajira.

Nae Mwenyekiti Mtendaji wa Chuo cha Bima na Hifadhi ya Jamii Afrika Dk. Baghayo Saqware, alimuleza Makamu wa Pili wa Rais kuwa, uongozi wa chuo hicho unakusudia kuifanya Zanzibar  kuwa kitovu cha huduma za fedha jambo, ambalo litasaidia kuunga mkono ajenda ya uchumi wa Buluu.

Pia alileza kwamba kitendo cha  kuwa kitovu cha huduma za kifedha Zanzibar itafaidika kwa njia nyingi ikiwa ni pamoja na mikataba muhimu ya kimkakati sambamba na taasisi nyengine kifedha kuweka ofisi zao visiwani Zanzibar.

Dk. Saqware  alisema chuo cha Bima na Hifadhi ya Jamii Afrika kina maono yenye mrengo wa kiafrika wa chuo cha kisasa kinachotoa mafunzo ya, utafiti, ushauri na ufumbuzi wa kimkakati katika maeneo ya Bima, Hifadhi ya Jamii, masoko ya mitaji na uongozi katika sekta ya Bima na Fedha.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.