Wajumbe wakiwa katika kikao wakimsikiliza Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Naibu Kamishna wa Uhamiaji, Nasra Mohamed (hayupo pichani) akifungua kikao hicho cha Kamati ya Kitaifa ya kuendeleza michezo Nchini.
Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Naibu Kamishna wa Uhamiaji, Nasra Mohammed akiwa katika picha ya pamoja na Wajumbe wa mkutano wa Baraza la Michezo la Majeshi Tanzania (BAMMATA) na Wajumbe wa Wizara ya Sanaa Utamaduni na Michezo, baada ya kumalizika kwa mkutano wao.
Kamati ya Kitaifa ya kuendeleza
michezo nchini inayojumuisha Wizara ya Sanaa Utamaduni na Michezo, Baraza la
Michezo la Majeshi Tanzania (BAMMATA), Baraza la Michezo la Taifa (BMT) na
Baraza la Taifa la Michezo Zanzibar (BTMZ) leo Oktoba 12, 2021 jijini Dar es
Salaam wamepitisha mpango wa muda mfupi
wa kuandaa Timu za Michezo za Taifa zitakazoshiriki Michezo
ya Jumuiya ya madola nchini Uingereza mapema Julai hadi Agosti 2022.
Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Naibu Kamishna wa Uhamiaji, Nasra Mohamed amesema tayari kamati yake imepitisha mpango huo hatua inayofuata ni kupeleka kwa Wizara yenye Sera na dhamana ya michezo nchini ili utekelezaji wake uanze mara moja kulingana na ratiba.
“Ninafuraha kusema kuwa mpango
huu umeandaliwa vizuri sana na wataalam wa michezo ni matumaini yetu kabla ya
mwezi ujao utakuwa umewasilishwa Wizarani ili tupate baraka na maelekezo
yatakayosaidia utekelezaji wake”. Amefafanua
Afande Mohamed
Aidha amesema Kamati imeteua Kamati ndogo ambayo itafanya kazi ya kuainisha mpango unaonyesha timu zitakazoshiriki, vifaa vya michezo, aina ya michezo itakayochezwa, wachezaji wa kila mchezo na kambi kwa ajili ya michezo hiyo ambapo amesema kambi hizo zitatakiwa kuanza rasmi mapema Januari 2022.
“Tumeitaka kamati ndogo
kufanya kazi usiku na mchana na kukutana na wataalam wa michezo, mashirikisho
na vyama vya michezo kwa kuwa kila mchezo una taratibu zake ”. Amesisitiza
Afande Nasra
Naye, Mwenyekiti Mwenza wa kamati hiyo, Addo Komba ambaye ni Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Maendeleo ya Michezo kutoka Wizara ya Sanaa, Utamaduni na Michezo aliyemwakilisha Mkurugenzi wa Michezo amesema uundwaji wa kamati hiyo ya kitaifa utasaidia kuleta mageuzi makubwa na hatimaye ushindi kwenye mashindano ya kimataifa yatakayoanza mwakani.
“Kipekee namshukuru Mhe. Rais
kwa maelekezo yake ya kutaka Vyombo vya Ulinzi na Usalama kwa kushirikiana
na Wizara tukae na kuaundaa Kamati kwa
ajili ya kuboresha michezo nchini ambapo leo tumeshuhudia
Mpango wa Muda mfupi wa kuandaa Timu za Taifa umekamilika”. Amefafanua Mkurugenzi
Komba
Kaimu Katibu wa BMT Neema
Msitha amepongeza kazi kubwa iliyofanywa
na kamati ndogo na kutaka bajeti na gharama halisi kwa ajili ya mashindano hayo
iandaliwe ambapo amesema ikikamilika italisaidia taifa kupiga hatua kwenye michezo kama
ilivyokuwa kwenye siku za nyuma.
No comments:
Post a Comment