Habari za Punde

Anzeni Kutoa Huduma za Kisaikolojia Kwa Njia ya Mtandao.Dkt.Jingu.

Katibu Mkuu, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto, Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii, Dkt. John Jingu akizindua Kituo cha Elimu, ushauri na Msaada wa Kisaikolojia kilicho chini ya Taasisi ya Ustawi wa Jamii leo mkoani Dar Es Salaam.

Katibu Mkuu, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto, Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii, Dkt. John Jingu akizungumza katika uzinduzi wa Kituo cha Elimu, ushauri na Msaada wa Kisaikolojia kilicho chini ya Taasisi ya Ustawi wa Jamii leo mkoani Dar Es Salaam.

                             Picha zote na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini WAMJW

Na Mwandishi Wetu

Katibu Mkuu, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto, Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii, Dkt. John Jingu ameitaka Taasisi ya Ustawi wa Jamii kuanza kutoa huduma za Ushauri na Msaada wa Kisaikojia kwa njia ya mtandao ili kuweza kuwafikia watu wengi.

 

Dkt. Jingu ametoa agizo hilo leo Novemba 15, 2021 mkoani Dar Es Salaam wakati akizindua  Kituo cha Elimu, ushauri na Msaada wa Kisaikolojia kilicho chini ya Taasisi ya Ustawi wa Jamii.

 

Dkt. Jingu amesema kuwa kuanza kutoa huduma hizo katika Kituo cha Elimu, Ushauri na Msaada wa Kisaikolojia kutaongeza ufanisi na kupunguza msongamano pindi wateja wakatapo kuwa wengi Kituoni hapo.

 

 “Anzisheni huduma kwa kutumia mtandao wa kijamii, sisi wizarani tumekwisha anza kutoa huduma kwa njia ya mtandao ili kurahisisha huduma” alisema Dkt. Jingu

 

Aidha Dkt. Jingu amesisitiza kuwa kituo hicho kina uhitaji mkubwa katika jamii kwani kuna matatizo mengi katika jamii ikiwemo mafarakano ya ndoa, kifamilia, misongo ya mawazo kutokana na ukosefu wa vipato toshelezi na ajira, kukata tamaa kutokana magonjwa sugu na ya kudumu  kama kansa na mengine yasiyoambukiza  hivyo kitasaidia kutoa huduma kwa wananchi ambao wamepatwa na matatizo ya Kisaikojia.

 

Ameyataja matatizo mengine yatajayosaidiwa katika Kituo hicho kuwa ni changamoto ya watoto wa wanaoishi na kufanya kazi mitaani, waraibu wa dawa za kulevya, masuala ya VVU na Ukimwi na matatizo mengi ambayo yanaikumba jamii yetu. 

 

Pia Dkt. Jingu ameipongeza Taasisi ya Ustawi wa Jamii kwa kuwa mstari wa mbele kushirikiana na wadau kutoa huduma za ushauri na msaada wa kisaikolojia pindi majanga yanapojitokeza hasa majanga ya moto, mafuriko na majanga mengine akitolea mfano maafa ya moto mjini Morogoro ambapo Taasisi ilikwenda kutoa msaada kwa wahanga. 

 

Dkt. Jingu ameuasa uongozi wa Taasisi ya Ustawi wa Jamii kukitunza na kukiendeleza kituo cha hicho cha elimu, Ushauri na Msaada wa kisaikolojia ili kiendelee kuwa msaada kwa Jamii kwani kitawasaidia watu wengi wenye hitaji la Huduma hizo. 

 

Akitoa ufafanuzi kuhusu kituo hizo Mkuu wa Taasisi ya Ustawi wa Jamii, Dkt. Joyce Nyoni amesema kuwa ukarabati wa kituo hicho umegharimu kiasi cha Shillingi 34,570,445 kutoka ufadhili Shirika la Koica.

 

Dkt. Joyce amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan kwa jinsi ambavyo amekuwa mstari wa mbele katika kusimamia ustawi wa Jamii hasa suala la malezi na makuzi ya watoto. 

 

Ameongeza kuwa katika kuhakikisha utaalam huo unaendelea Taasisi hiyo inatoa kozi mbalimbali kulingana na mahitaji katika jamii kwa ngazi ya cheti hadi ngazi ya uzamili na kukamilika kwa kazi ya kukarabati kituo hicho kutaboresha mazingira ya utoaji huduma na kitarahisisha upatikanaji wa huduma. 

 

“Kulikuwa hakuna faragha katika utoaji huduma kabla ya Kituo hiki kukarabatiwa kwani huduma zilitolewa maofisini kwa wahadhiri lakini sasa vyumba vya kutolea huduma vina mazingira mazuri ya huduma kutolewa kwa faragha’’ alisema Dkt. Joyce. 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.