Habari za Punde

Serikali Kuendelea Kufungua Fursa kwa Wanawake – Naibu Waziri Katambi.

Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Kazi, Vijana na Ajira Mhe. Patrobas Katambi akihutubia wakati wa hafla ya uzinduzi wa mradi wa WAENDELEZE iliyofanyika nyumbani kwa balozi wa Uholanzi nchini Tanzania
Balozi wa Uholanzi nchini Tanzania Mhe. Wiebe de Boer akieleza jambo wakati wa hafla hiyo iliyofanyika Jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Lindam Bi. Zuhura Muro akifafanua kuhusu mradi wa WAENDELEZE wakati wa hafla ya uzinduzi wa mradi huo iliyofanyika nyumbani kwa balozi wa Uholanzi nchini Tanzania Jijini Dar es Salaam.
Sehemu ya washiriki na wanufaika wa mradi wa WAENDELEZE wakifuatilia hotuba ya Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Kazi, Vijana na Ajira Mhe. Patrobas Katambi (hayupo pichani) wakati wa hafla hiyo.
Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Kazi, Vijana na Ajira Mhe. Patrobas Katambi (kushoto) akizungumza na Balozi wa Uholanzi nchini Tanzania Mhe. Wiebe de Boer alipokabidhiwa zawadi ya begi lenye nembo ya mradi wa WAENDELEZE ikiashiria mchango wake katika kufanikisha mradi huo. Katikati ni Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Lindam Bi. Zuhura Muro.

Na: Mwandishi Wetu – DAR ES SALAAM

SERIKALI imeazimia kuendelea kufungua fursa zaidi kwa wanawake nchini katika kufanya biashara, kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji ikiwa ni pamoja na kuwapatia mafunzo ya kukuza biashara na mitaji, kufungua masoko na kuwatambua vitendea kazi muhumu kwa ajili ya kufanyia biashara zao.

Hayo yameelezwa na Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Kazi, Vijana na Ajira Mhe. Patrobas Katambi wakati akizindua mradi wa WAENDELEZE unaoratibiwa na Serikali kwa kushirikiana na Ubalozi wa Uholanzi nchini Tanzania.

Alisema kuwa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan imeendelea kutoa fursa kwa wanawake kujiendeleza kibiashara ili kuinua uwezo wao na kuwawezesha katika kuchangia maendeleo ya Taifa.

“Mradi huu wa Waendeleze ni moja ya jitihada za Serikali inayoongozwa na Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa ushirikiano mzuri na wadau wa maendeleo ambao unalenga kumuinua mwanamke anayefanya biashara aweze kufikia hatua za juu zaidi,” alisema Naibu Waziri Katambi

Aliongeza kuwa katika kufanikisha mradi huo wa WAENDELEZE, Ubalozi wa Uholanzi nchini umewezesha mafunzo kwa wafanyabiashara wanawake kwa kushirikiana na Taasisi ya Uongozi ambapo wanawake kutoka kanda ya ziwa, kanda ya nyanda za juu kusini, kanda ya kati, kanda ya magharibi na kanda ya mashariki wamenufaika.

“Tumeshuhudia hapa wafanyabiashara wanawake wanaojishughulisha na shughuli mbalimbali za uzalishaji mali ikiwemo kilimo, ufugaji, usindikaji na kadhalika namna mafunzo hayo yalivyowasaidia kufungua fursa nyingi ikiwa ni pamoja na kukuza mtandao wa biashara zao na masoko,” alisema

Aidha, Naibu Waziri Katambi aliwasihi wanawake walionufaika na mafunzo hayo kutoa elimu na kuwa mfano wa kuigwa katika maeneo wanayofanya biashara ili kuwapa hamasa wengine.

Sambamba na hayo alitumia fursa hiyo kuwahimiza Wanawake, Vijana na Watu wenye Ulemavu kuchangamikia fursa ya mikopo ya asilimia 10 (4% Vijana, 4% Wanawake na 2% Wenye Ulemavu) kupitia mapato ya ndani ya Halmashauri ili kuanzisha na kuendeleza shughuli au miradi itakayowaingizia kipato na kutimiza ndoto zao.

Kwa upande wake, Balozi wa Uholanzi nchini Tanzania Mhe. Wiebe de Boer alisema kuwa serikali ya ufalme wa Uholanzi itaendelea kushirikina na Serikali katika kuboresha na kuendeleza wafanyabiasha wanawake nchini kupitia mradi huo wa WAENDELEZE.

Naye, Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Lindam Bi. Zuhura Muro, alisema kuwa mradi huo umewawezesha wafanyabiashara wanawake kupata hamasa ya kuchangia pato la Taifa na pia kupitia shughuli zao za kiuchumi wameweza kutoa fursa za ajira kwa wengine.

Pamoja hayo, Mkuu wa Kitengo cha Kilimo Biashara kutoka Benki ya NMB, Bw. Issack Masusu alieleza kuwa benki hiyo ya NMB imepunguza riba katika eneo la sekta ya kilimo na kilimo biashara ambapo riba hiyo imeshuka kutoka asilimia 18 hadi 10.

“Benki ya NMB imetenga kiasi cha Tsh. Bilioni 100 kwa ajili ya kuwezesha mikopo kwa wafanyabiashara ambapo kiasi cha laki 2 hadi bilioni 10 zimekuwa zikitolewa kwa mkopaji mmoja, hivyo ni vyema wanufaika wa mradi huu wakakimbilia fursa hiyo ambayo itakuwa chachu katika ukuaji wa biashara zao,” alisema Masusu

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.