Habari za Punde

Wizara Afya na Ustawi wa Jamii Wazee Jinsia na Watoto Mhe Nassor Ahmed Mazrui Azungumza na Waandishi wa Habari Mikakati ya Kuboresha Huduma za Afya kwa Wananchi Wake.

 

Waziri wa Afya , Ustawi wa Jamii, Wazee, Jinsia na Watoto Nassor Ahmed Mazrui . Akizungumza na Waandishi wa habari juu ya Ufafanuzi wa Miradi ya Maendeleo inayotekelezwa katika Wizara yake, kwa Fedha za Mkopo kutoka Shirika la Fedha Duniani (IMF) Hafla iliyofanyika Ukumbi wa Hoteli ya Verde Mjini Zanzibar.
Baadhi ya Waandishi wa Habari na Wafanyakazi wa Wizara ya Afya , Ustawi wa Jamii, Wazee, Jinsia na Watoto. Wakimsikiliza Waziri wa Afya , Ustawi wa Jamii, Wazee, Jinsia na Watoto Nassor Ahmed Mazrui . akitoa Ufafanuzi wa Miradi ya Maendeleo inayotekelezwa katika Wizara yake, kwa Fedha za Mkopo kutoka Shirika la Fedha Duniani (IMF) Hafla iliyofanyika Ukumbi wa Hoteli ya Verde Mjini Zanzibar.
Baadhi ya Waandishi wa Habari na Wafanyakazi wa Wizara ya Afya , Ustawi wa Jamii, Wazee, Jinsia na Watoto. Wakimsikiliza Waziri wa Afya , Ustawi wa Jamii, Wazee, Jinsia na Watoto Nassor Ahmed Mazrui . akitoa Ufafanuzi wa Miradi ya Maendeleo inayotekelezwa katika Wizara yake, kwa Fedha za Mkopo kutoka Shirika la Fedha Duniani (IMF) Hafla iliyofanyika Ukumbi wa Hoteli ya Verde Mjini Zanzibar.
Waziri wa Afya , Ustawi wa Jamii, Wazee, Jinsia na Watoto Nassor Ahmed Mazrui . Akizungumza na Waandishi wa habari juu ya Ufafanuzi wa Miradi ya Maendeleo inayotekelezwa katika Wizara yake, kwa Fedha za Mkopo kutoka Shirika la Fedha Duniani (IMF) Hafla iliyofanyika Ukumbi wa Hoteli ya Verde Mjini Zanzibar.

Hotuba ya Mhe. Waziri wa Afya Ustawi wa Jamii Wazee Jinsia na Watoto Zanzibar Mhe.Nassor Ahmed Mazrui, wakati akizungumzia Miradi ya Maendeleo kwa Fedha za IFM.Katika ukumbi wa Hoteli ya Verde Mtoni Zanzibar.12.Novemba,202. 

Ndugu Waandishi wa Habari.

Assalaamu alaykum. 

Nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu, aliyetupa uhai na nguvu ya kutuwezesha kukutana hapa leo, katika shughuli hii adhimu tukiwa katika hali ya afya njema.

Leo hii tumepata fursa tena ya kuzungumza na Wananchi kupitia waandishi wa Habari.

Ndugu Waandishi wa Habari, Wizara hii ina majukumu ya msingi yafuatayo: -

Kuhakikisha kwamba wananchi wote wa Zanzibar bila ya ubaguzi wa aina yoyote wanakuwa na afya njema pamoja kuwapatia huduma bora za kinga na tiba;

Kuratibu na kusimamia upatikanaji wa haki kwa makundi yenye mazingira magumu kwa kuimarisha mifumo ya hifadhi ya jamii na huduma kwa Wazee, Watoto na wanaoishi katika mazingira magumu zaidi; na

Kuratibu na kusimamia utekelezaji wa haki za wanawake na watoto katika kukabiliana na vitendo vyote vya udhalilishaji ikiwa ni pamoja na kusimamia utekelezaji wa sera, sheria zinazohusu maendeleo ya wanawake na watoto pamoja na kuwaendeleza wanawake kwa kuzingatia mipango ya Kitaifa, Mikataba ya Kimataifa na Kikanda. 

Ndugu Waandishi wa Habari, Itakumbukwa kwamba, hivi karibuni Serikali ya awamu ya nane (8) inayoongozwa na Mhe Rais Mwinyi imeadhimisha mwaka mmoja tokea kuingia madarakani.  Katika maadhimishisho hayo ambayo yaliadhimishwa kwa shughuli mbali mbali, kilele chake kilifanyika tarehe 6 November, 2021 katika hoteli ya Golden Tulip, Kisauni mjini Unguja ambapo Mheshimiwa Rais alihutubia Taifa. 

Katika hotuba yake alieleza kwa kina Mpango wa Utekelezaji wa Serikali katika kipindi cha mwaka mmoja ujao na kuelekea miaka minne iliyo kwenye awamu hii. Maadhimisho hayo yalihudhuriwa na Viongozi mbali mbali wa chama na serikali. Aidha katika hotuba yake aliahidi Serikali yake imepanga kutumia fedha katika kuimarisha miradi iliyopo na kuanzisha miradi kadhaa ya maendeleo. Serikali ya Awamu ya 8 katika kutekeleza hilo imetenga kiasi kikubwa cha fedha ambazo zitatumika kupitia sekta mbali mbali. Hii ni Pamoja na sekta ya inayojumuisha maendeleo na ustawi wa Jamii wa Wazee, Jinsia na Watoto.

Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuufufua Uchumi kutokana na janga la UVIKO-19 imechukua mkopo wa fedha kutoka Shirika la Fedha Duniani (IMF) jumla ya shilingi Billion 230 utakaoharakisha maendeleo hayo. Kutoka na Umuhimu wa Sekta ya Afya katika utoaji uduma kwa Jamii Wizara yangu imepatiwa kiasi  cha shilingi bilioni 69.

Ndugu Waandishi wa Habari.

Hili la matumizi ya Mkopo wa IMF ndio leo ambalo nataka kulifanyia ufafanuzi ili muweze kujua zitatumika vipi na kwa maeneo yepi, kwenye Sekta ya Afya.

Ndugu Waandishi wa Habari, Sekta yangu imepanga kutekeleza Miradi mbali mbali ya kuimarisha miundombinu ya afya na upatikanaji wa vifaa tiba 

Kwanza, nianze na miradi ya kuimarisha miundombinu ya Afya ikiwemo ujenzi wa hospitali mpya ngazi ya Mkoa wa Mjini Magharibi, eneo la Lumumba itakayokuwa na uwezo wa kulaza wagonjwa 200 kwa wakati mmoja. Hospitali ya Mkoa itakuwa na ghorofa tano, itakuwa na huduma za wagonjwa kwa nje (OPD) na waliolazwa (IPD). Hospitali itakua na huduma za kisasa za MRI, CT scan na kutoa huduma zote za kitaalamu zikiwemo huduma za Sikio, Pua na Koo (ENT), Aidha kutakua na huduma za macho, meno, kliniki na wodi za kulaza wagonjwa mbali mbali. Ujenzi huu una nia ya kuongeza wigo wa huduma na kupunguza idadi ya watu wanaokwenda hospitali ya Mnazi Mmoja ambayo itaendelea uboreshwa ili ikidhi hadhi yake yakuwa hospitali ya rufaa. 

Kuhusu miundombinu ya Hospital ya Mkoa ya Abdalla Mzee tutajenga chumba cha Wagonjwa mahututi ICU, Chumba cha Kuhifadhia maiti na kuweka vifaa vya kisasa vya uchunguzi kama “Digital X ray”, huduma za figo “Dialysis”, vifaa vya chumba cha upasuaji na kuweka mtambo wa gesi tiba “Oxygen Plant” ambao utasambaza moja kwa moja kwenye kitanda cha mgonjwa.

Sambamba na ujenzi huo, Serikali itajenga hospitali 10 katika ngazi ya Wilaya zinazotegemewa kwa kila moja kulaza wagonjwa 100 kwa wakati Mmoja, pamoja na nyumba za wafanyakazi kwa baadhi ya hospitali zitakazotosha familia 16.  Hospitali hizo zitajengwa katika maeneo ya Unguja na Pemba

Kwa Unguja ujenzi huo utakua kwenye maeneo yafuatayo:

Chumbuni, Magogoni,Kivunge,Pangatupu,Dunga,Makunduchi, 

Kwa upande wa Pemba ni: 

Micheweni, Vitongoji Chakechake na Kinyasini Wete Pemba.

Ndugu Waandishi wa Habari.

Michoro ya Hospitali zote hizi imekamilika na taratibu za manunuzi ili kuwapata wakandarasi wa ujenzi zitatangazwa rasmi kwa kutumia njia ya haraka ili kazi iliyokusudiwa ifanyike kwa muda uliopangwa. Kazi za ujenzi zinaanza mwezi wa Disemba, 2021 na kukamilika Juni, 2022.

Hospitali hizi zitatoa huduma za wagojwa wa nje (OPD) na waliolazwa, uchunguzi kwa kutumia vifaa vya kisasa (X-ray ya kijiditali, Ultrasound, upimaji wa damu kujuwa kiwango cha damu, uwepo wa magojwa ya sukari, mafuta kwenye damu, mabadiliko ya damu yanayohusiana na figo na kadhalika). Huduma nyengine ni Pamoja na huduma za ICU, magojwa ya wanawake, Kliniki za waja wazito, huduma za uzazi wa kawaida na wa operesheni, upasuaji mdogo (wanaume na wanawake), huduma za watoto ikiwemo sehemu ya kuwaweka “watoto njiti”. Hospitali zote zitakuwa na sehemu ya kutoa huduma kamilifu kwa wahanga wa Unyanyasaji wa Kijinsia (One stop centres).

Ndugu Waandishi wa Habari, 

Serikali itanunua magari 12 ya kubebea wagonjwa (ambulances). Gari hizo zitakuwa za aina ya Toyota Land cruiser zitakazonunuliwa moja kwa moja kutoka kiwandani zitasambazwa katika hospitali zote za Wilaya na mbili katika hospitali za Mikoa; vile vile, Serikali itanunua magari matano (5) ya kusambazia dawa katika hospitali na vituo vya afya Unguja na Pemba. Huduma hii itaondosha gharama zinazotumika hivi sasa za kukodi gari za kampuni binafsi kwa kufanya kazi hiyo na pia kuhakikisha usalama wa dawa na vifaa tiba vinavyosafirishwa

Ndugu Waandishi wa Habari, 

Kila hospitali ya wilaya itakuwa na Mtambo wa kuchomea taka hatarishi kwa lengo la kudhibiti mazingira. Aidha kati ya mitambo hiyo, miwili itakuwa ni yenye uwezo mkubwa wa kuchoma taka hatarishi nyingi kwa wakati mmoja na itafungwa katika hospitali ya Mkoa ili iweze kutoa huduma kwa hospitali za karibu za Serikali na pia Sekta binafsi  

Ndugu Waandishi wa Habari, Huduma za Damu Salama zitaimarishwa kwa kupatiwa vitendea kazi muhimu vinavyoendana na mahitaji husika ili kuweza kutoa huduma muda wote, hali ambayo kwa sasa kitengo hakina vifaa hivyo. Uwepo wa vifaa hivyo kutaongeza damu iliyopimwa na kuwa tayari kupewa mgonjwa anaehitaji

Ndugu Waandishi wa Habari, 

Serikali itaweka mitambo 2- katika Hopsitali za Pangatupu na Abdalla Mzee ya kuzalisha gesi tiba (oxygen) kila mmoja ikiwa na uwezo wa kuzalisha mitungi 400 kwa siku, itakayotumika kwenye hospitali nyengine Pemba na Unguja zitakazohitaji huduma hii. 

Ndugu Waandishi wa Habari, 

Serikali inahakikisha kwamba Hospitali zote tunazozijenga zitakuwa na vifaa tiba vya kisasa katika utoaji wa huduma za uchunguzi za mionzi (X ray, CT-scan na Ultrasound) na za maabara ili kutambua maradhi mbali mbali ikiwemo figo, saratani nakadhalika, 

Ndugu Waandishi wa Habari, 

Matarajio/faida zitakazopatikana baada ya kukamilika mradi ni kupeleka huduma za Afya zilizo bora karibu na wananchi, pia itapunguza idadi ya wagonjwa wanaosafirishwa nje ya Zanzibar. 

 Ndugu waandishi wa Habari, 

Hizi huduma za afya ambazo Serikali yetu inaziimarisha hazitokuwa na maana kama hatutozitumia, naomba niwaambie wananchi wote, kike kwa kiume kuanza kuhudhuria kliniki mapema, hii ni Pamoja na wajawazito kujifungulia Hospitali. Aidha tujitahidi kupeleka watoto wote kupimwa ili kujua maendeleo yao ya afya na ukuaji wao, hii ni pamoja na kupata chanjo zote stahiki ili kuwakinga na maradhi. 

Ndugu waandishi wa Habari 

Hitimisho

Nachukua fursa hii kuishukuru Serikali ya awamu ya 8 chini ya Uongozi mahiri wa Dr Mwinyi, juhudi za kuwaletea maendeleo wananchi zimeanza kuonekana ikiwa pamoja na uimarishwaji wa Sekta ninayoiongoza. Ambapo zinaimarisha kwa juhudi kubwa ili kuwafikishia wananchi huduma safi kwa wananchi wote wa Zanzibar. Huduma ambazo zinapatikana karibu na ulipo na bila ubaguzi wowote.

Mwisho

Nachukua nafasi hii vile vile kuwakumbusha Wazanzibari wote kupata Chanjo dhidi ya UVIKO 19. Idadi ya waliopata chanjo inaendelea kuongezeka. Napenda mufahamu hadi  tarehe 10 Novemba  2021 jumla ya watu 70,000 tayari wameshapatiwa chanjo hizo hapa Zanzibar. Hivyo nawasihi wananchi wote wenye umri kuazia miaka 18 na kuendelea wajihimu kuchanja. Kwani ukichanja utakua umetengeneza kinga ya kupambana na ugonjwa huu thakili, si hivyo tu bali utakua pia unawakinga wengine na maambukizo. Inatakiwa tufahamu pia kuwa Kinga ni bora kuliko tiba na wageni wote wanakaribishwa Zanzibar ipo Salama

Ndugu waandishi wa habari

 Ahsanteni sana kwa kunisikiliza.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.