Habari za Punde

Zawadi ya Miwani ya Mpingo.

 


Na.Adeladius Makwega  Mbagala.

Siku moja nilipokuwa natoka nyumbani kwangu huko kwa akina yakhe nilipata usafiri wa haraka wa kwenda kwa akina pangu pakavu tia mchuzi, nilipoingia katika daladala nilikaa jirani na mama mmoja ambaye alikuwa na wajihi unaofanana sana na Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Bi Samia Suluhu Hassan. Ama kweli duniani wawili wawili.

Nilimpenda sana mama huyu namna alivyokuwa akizungumza, kwani nadhani alikuwa akitokea Zanzibar. Nilivutiwa sana na mama huyu kwani alikuwa amependeza sana na miwani yake ilikuwa na rangi nyeusi.

Miwani ile ilifanya aonekane amependeza mno, nikasema kwa hakika na mimi nitaweka oda na mimi nitengenezewe miwani kama hiyo.

Nikiwa nimeketi katika kiti cha mbele cha dereva na mama huyu akiwa kiti cha dirishani nilimwambia umependeza sana alicheka tu na mwisho alisema asante. Akaniuliza kitu gani kilichokuvutia mno, nikamjibu kuwa haswa hiyo miwani. Alitabasamu huku safari yetu ikiendelea.

Nilimuuliza hiyo ni miwani ya macho au ya urembo? Alinijibu kuwa yeye anavaa miwani ya aina mbili nayo ni ya urembo na pia anayo ya kuona mbali. Nilimuuliza kumbe hivyo ndiyo ilivyo kwa wote wanaovaa miwani? Alinijibu kuwa ni kweli. Nikamuuliza kumbe hata waheshimiwa wengi wanavaa miwani kumbe mingine ya urembo na mingine ya macho? alinijibu kuwa ni kweli kabisa.

Kumbuka tupo katika daladala na hayo mazungumzo yanapamba moto huku dereva akitusikiliza kwa makini akidhani kuwa mie na huyu mama tunafahamiana kumbe wala, ilinijia picha ya uvaaji wa miwani ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu, Marehemu Magufuli alikuwa akivaa miwani, na hata Mheshimiwa Rais Jakaya Kikwete, Marehemu Rais Benjamin Mkapa, Mheshimiwa Rais Ali Hassani Mwinyi na Marehemu Rais Julius Nyerere.(haya niliyafikiri kwa sekunde kadhaa) Alafu nikamwambia huyu mama kumbe mnaovaa miwani mnaona karibu na mbali vizuri sana.

Akasema ehh! tunaona karibu na mbali vizuri sana, wewe uoni Mheshimiwa Samia anavaa miwani anaona kote vizuri sana. Alipoyasema haya kama aliingia katika akili yangu kile nilichokuwa nakifikiria.

Nikamwambia kumbe, ngoja nimnunulie zawadi ya miwani Mheshimwa Rais Samia Suluhu miwani mizuri sana, miwani imara, miwani ya kudumu. Mama huyu alicheka sana, akasema wewe unataka kumchokoa pweza. Nikamjibu hapana nampa kama zawadi Mheshimiwa wetu. Nikamwambia miwani hii itakuwa na mishikio iliyotengenezwa kwa mti wa mpingo. Mti huu wa mpingo utakuwa umeshikilia miwani yote tangu flemu zake hadi mishikio, sifa yake kubwa hata ikiangushwa haitoweza kuvunjika.

Mama huyu alicheka akasema kuwa haiwezi kumuumiza Mheshimiwa? Nilijibu kuwa itatengenezwa vizuri sana na haiwezi kumletea madhara Mheshimiwa.

Miwani yangu hii itakuwa na lenzi mbili yaani lenzi mbonyeo ya kuona mbali na ile lenzi mbinuko ya kuona karibu. Pale atakapotaka kuona karibu ataweza kuiona karibu kwa haraka na hata akitaka kuona mbali ataweza kufanya hivyo kwa haraka kwa kutumia kipachiko chake maalumu kuruhusu hali anayotaka kwa wakati husika.

Mama huyu aliniambia kweli hiyo miwani yako itakuwa hatari, nikasema itakuwa maalumu kwa ajili ya Mheshimiwa Rais tu. Miwani yangu hii itafungwa na kamba maalumu ya iliyotengenezwa kwa ngozi laini lakini imara ya twiga ili Mheshimiwa akiining’iniza haitoweza kuanguka. Mama huyu alicheka na kasema kwanini usitengeneze kwa ngozi ya mnyama mwingine nilimjibu kuwa nampenda sana twiga huwa hana papara na miwani hiyo itamuwezesha Mheshimiwa kuona bila papara. Nilimwambia mama huyu kuwa nitamtengenezea pia mkebe mzuri uliotengenezwa kwa mpingo ambapo utatumika kuhifadhi miwani hiyo.

Nikaulizwa ehh, hiyo miwani itamfikiaje Mheshimiwa? Ah dereva wa daladala aliingilia kati akasema kaka hiyo miwani yako itakuwa tabu mno kumfikia mheshimiwa. Mama huyu akasema nitakupa namba yangu ukishatengeneza nitampatia. Mama huyu ambaye alikuwa abiria mwezangu akasema kuwa mie nitamsubiria Mheshimiwa akienda kwetu Zanzibar akiwa anatoka msikitini nitamsalimia nitamkabidhi zawadi hiyo ya miwani.

Miwani yangu hii itakuwa na sharti moja tu hakuna atakayeruhusiwa kuijaribu isipokuwa yeye mwenyewe tu. Nilimuuliza mama huyu je miwani yangu itafika salama kwa Mheshimiwa na kuelezwa masharti ya miwani hii? Dereva wa daladala hii alisema kuwa kama mama huyu namna alivyo nina hakika kuwa akikabidhiwa miwani hiyo itamfikia Mheshimiwa salama salimini.

Mara daladala yetu ilizimika gafla dereva akasema kuwa gari imeishiwa mafuta kwa hiyo konda alishuka na kidumu cha lita tano ili akachuke mafuta na mie nilichukua namba ya simu ya  mama huyu na kuondoka zangu kwenda huko madongo poromoka na kuwaacha abiria wengine, yule mama na dereva wakimgonja konda arudi na mafuta ili waendelee na safari.

Kwa hiyo kwa sasa nipo katika kazi yangu ya kuitengeneza miwani hiyo itakapokamilika nitawasiliana na mama huyu ambaye alikuwa abiria mwenzangu niliyekutana naye katika daladala hiyo ili nikamilishe zoezi langu.

makwadeladius@gmail.com

0717649257

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.