Habari za Punde

Umuhimu wa Kutafakari Mafanikio na Changamoto Zilizojitokeza Katika Kipindi cha Miaka 29 Katika Demokrasia ya Vyama Vingi vya Siasa.

 

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe,Dk.Hussein Ali Mwinyi akihutubia katika hafla ya ufunguji wa Mkutano wa Wadau wa Kujadili hali ya Demokrasia ya Vyama Vingi vya Siasa Nchini Tanzania, uliowashirikisha Viongozi wa mbalimbali wa Vyama vya Siasa Tanzania uliofanyika katika ukumbi wa Hazina Jijini Dodoma

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi  Dk. Hussein Ali Mwinyi amesema kuna  umuhimu wa kutafakari mafanikio na changamoto zilizojitokeza katika kipindi cha miaka 29 tangu  mfumo wa  Demokrasia ya vyama vingi vya siasa kuanzishwa hapa nchini.

Dk Mwinyi amesema hayo wakati akifunga mkutano maalum uliojadili hali ya mfumo wa Demokrasia ya  vyama vingi vya siasa  nchini , uliofanyika katika Ukumbi wa  Jengo la Hazina Mjini Dodoma.

Alisema historia inaonyesha kuwa mkutano huo ni muhimu kwa vile katika kipindi hicho cha miaka 29 kuna mambo mengi ya mafanikio yaliopatikana pamoja na changamoto mbali mbali zilizojitokeza, ambazo zimetolewa  mapendekezo kwa lengo la kuzitafutia ufumbuzi.

Alisema amefurahishwa na mapendekeezo ya maazimio yaliofikiwa katika mkutano huo, ikiwemo suala la umuhimu wa kuheshimu sheria na kudumisha amani na utulivu, umoja wa kisiasa pamoja na kuendeleza uchumi katika mfumo wa Demokrasia ya siasa ya Vyama vingi na kusema jambo hilo ni muhimu kwa vile maendeleeo ya nchi yanategemea sana uwepo wa amani na utulivu.

Alieleza kuwa mfumo wa vyama vingi umepanua wigo wa majukwaa ya kidemokrasia, uhuru wa kutoa maoni na kuchagua pamoja na kutoa fursa ya kuishauri na kuikosoa Serikali, hivyo akatowa wito kwa Watanzania kuhakikisha wanaendeleza siasa zenye malengo ya kulinda na kuendeleza maslahi ya Taifa.

“Ni vyema tujiepushe na siasa za chuki zenye lengo la kutugawa”, alisema.

Aidha, alisema kwa kawaida utulivu wa kisiasa hutokana na mikutano ya aina hiyo ambapo watu hukaa na kujadiliana pamoja na kubadilishana mawazo huku wakiweka mbele maslahi ya taifa, hivyo akawataka Watanzania kuendeleza utamaduni wa kuzungumza na kuheshimu sheria.

Rais Dk. Mwinyi akazipongeza Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa pamoja na   Baraza la Vyama vya Siasa kwa kuandaa mkutano huo muhimu na kumualika katika ufungaji wake.

Nae, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu,  Sera, Bunge, Uratibu, Kazi, Ajira, Vijana, wenye Ulemavu Jenista Mhagama alisema kazi inayoendelea kufanyika hapa nchini ni muhimu katika kuimarisha misingi ya Demokrasia na usimamizi thabiti wa Demokrasia na kubainisha suala la ulinzi wa Demokrasia kuwa ni la watu wote.

Alitumia fursa hiyo kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mama Samia Suluhu Hassan pamoja na Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Dk. Hussein Ali Mwinyi kwa ushirikishwaji wa viongozi wa vyama vya upinzani  serikalini, ikiwa ni hatua ya kujenga ustawi wa Taifa na kudumisha Demokrasia ya vyama vingi hapa nchini.

Mapema, Mwenyekiti wa Mkutano huo Pro. Rwekiza Mkandala alisema  katika mkutano huo mambo kadhaa yamefikiwa, ikiwemo hoja ya mkutano wa aina hiyo kufanyika mara kwa mara pamoja na vyombo  vyenye maamuzi kuzingatia wajibu wa kutenda haki.

Aidha, alisema mkutano umeazimia  hoja ya Demokrasia kutegemea mazingira ya nchi husika na Watanzania kuondokana na utamaduni wa kuiga.

Vile vile mkutano umefikia azimio la kuitaka Serikali na Vyombo  vya Dola kuhakikisha vinaepuka upendeleo pale vinaposhughulikia masuala ya kisiasa pamoja na kuzingatia umuhimu wa sheria ya Jeshi Polisi kufanyiwa mapitio ili kuondokana na vitendo vya uonevu.

Mkutano huo wa siku tatu uliofunguliwa na Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania umeshirikisha makundi yote, ikiwemo watu wenye ulemavu.   

Kitengo cha Habari,

Ikulu Zanzibar

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.