Habari za Punde

Uzinduzi wa Filamu ya Vuta N'KUVUTE Ukumbi wa Ngome Kongwe Forodhani Jijini Zanzibar.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe.Hemed Suleiman Abdulla akikabidhiwa zawadi ya Picha Maalum ya Filamu ya VUTA N'KUVUTE  na Muandaaji wa Filamu  hiyo wakati wa hafla ya uzinduzi wake uliofanyika katika ukumbi wa Ngome Kongwe Forodhani Jijini Zanzibar,akipokea kwa Niaba ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi na (kulia) Waziri wa Habari na Michezo Zanzibar Mhe. Tabia Maulid Mwita.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla akiwa pamoja na viongozi mbali mbali wa serikali na Taasisi ya ZIFF wakati akiwasili katika Ukumbi wa Ngome Kongwe kwajili ya uzinduzi wa Filamu ya VUTA N’KUVUTE.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe.Hemed Suleiman Abdulla akizungumza na viongozi pamoja na waalikwa mbali mbali waliohudhuria katika uzinduzi wa Filamu ya VUTA N’KUVUTE iliofanyika katika Ukumbi wa Ngome Kongwe Forodhani ambapo Mhe. Hemed alimuakisha Rais Dk. Mwinyi katika uzinduzi huo.

Baadhi ya wasanii walioshiriki katika uwigizaji wa Filamu ya VUTA N’KUVUTE wakiwa jukwaani katika hafla ya uzinduzi wa filamu iyo uliofanyika katika Ukumbi wa Ngome Kongwe Forodhani.

Na.Kassim Abdi - OMPR.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi ameupongeza uongozi wa Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo kwa kushirikiana pamoja na wamiliki wa Filamu ya VUTA N’KUVUTE kwa kuipa sifa Zanzibar katika ngazi ya kimataifa kupitia tasnia ya uwigizaji wa filamu.

Rais Dk. Mwinyi alisema hayo kupitia hotuba yake ilisomwa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar katika uzinduzi wa Filamu ya VUTA N’KUVUTE uliofanyika katika Ukumbi wa Ngome Kongwe Jijini Zanzibar.

Alisema uzinduzi wa filamu hiyo ambayo imepata sifa kimataifa ni ithibati ya mafanikio yanayoendelea kupatikana katika tasnia ya filamu hapa Zanzibar na katika Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kwa ujumla.

Rais Dk. Mwinyi alisema ni jambo la fahari kuona uongozi wa Wizara ya habari unatekeleza kwa vitendo ahadi alizozitoa wakati wa uzinduzi wa Baraza la kumi la wawkilishi ambapo aliahidi kushughulikia sanaa, burudani na michezo.

Alisema sekta ya sanaa ina mchango mkubwa ikiwemo kuwaunganisha wazanzibar, kuitangaza Zanzibar kikanda na kimataifa sambamba na kutoa ajira kwa vijana.

Aidha, Rais Dk. Mwinyi aliwahimiza waandaji na waigizaji wa filamu kuhakikisha kwamba, filamu wanazozitengeneza zinaendana na mila, silka na tamaduni za Kitanzania kwani kazi ya sana haiishi katika kutumbuiza bali pia lazima itekeleze jukumu la msingi la kuelimisha jamii na kutangaza tamaduni.

« Hivyo, kwa ufundi kabisa tuhakikishe kwamba, filamu tunazoigiza kwa namna moja fulani zinakuwa na utambulisho wa taifa letu » Alisema Rais Dk. Mwinyi

Alieleza kuwa, kuna haja ya kujivunia kupitia uzinduzi wa Filamu ya VUTA N’KUVUTE kutokana na filamu hiyo kuakisi mandhari ya Zanzibar kutokana na kutaja mitaa, majina ya watu, lafudhi ya lugha ambapo watazamaji watakuwa na kazi ya kuchambua fani na maudhuri yanayopatikana katika filamu hiyo.

Alibainisha kuwa, jitahada za kukuza na kuendeleza sana aya muziki na filamu zina mchango mkubwa katika kuikuza, kuilinda, kuitangaza na kuisambaza lugha ya kiswahili pamoja na utamaduni wake, hivyo amehimiza katika utengenezaji wa filamu hizo kuzingatiwe matumizi mazuri ya lugha ya Kiswahili.

« Nashauri kwamba, kuna haja ya kuandaa wataalamu wa kutosha wenye kufahamu lugha nyengine kubwa zinazozungumzwa duniani kwa ajili ya kuweka tafsiri ya yale yanayozungumzwa ili filamu zetu ziweze kuuzika kirahisi katika soko la kimataifa.

Alileza kuwa, watu wengi hupenda kutoka nchi mbali mbali kuangalia filamu za kigeni zilizotafsiriwa kinachozungumzwa, hatua hiyo itatoa fursa kufundisha watu kiswahili bila wao wenyewe kujua au kutaka.

Rais Dk. Mwinyi amesema filamu ya VUTA N’KUVUTE kupitia kuoneshwa katika matamasha mbali mbali inaweza kuiletea sifa zaidi Zanzibar na Tazania kwa ujumla Duniani kote pamoja na kuipatia nchi tunzo nyingi za kitaifa na kimataifa.

« Naamini mafanikio hayo yatakayopatikana kutokana na filamu hii yatazidi kuhamasisha wasanii wengine wa filamu nchini mwetu » Alieleza DK. Mwinyi

Katika uzinduzi huo, Dk. Mwinyi alitumia fursa hiyo kumpongeza mwandishi mashuhuri Shafi Adam Shafi wa riwaya ya VUTA N’KUVUTE kutokana na umahiri wake na ubunifu wa hali ya juu aliouonesha katika utunzi wa riwaya hiyo iliojaa visa vya mapenzi na mapambano.

Kabla ya kumalizia Hotuba yake, Rais Dk. Mwinyi aliwahimiza na kuwashawishi wasanii chipukizi kuendelea kujituma kwani safari ya mafanikio inahitaji ujasiri,uvumilivu na mipango imara na kueleza kuwa wapo wasanii wanaoharibu maendeleo yao kwa kutaka mambo mengi makubwa katika hatua za awali, jambo ambalo linawafanya baadhi ya wasanii kupoteza mweleko mapema na kushindwa njiani.

Kabla ya kumkaribisha mgeni rasmi Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Mhe. Tabia Maulid Mwita amesema wizara anayoisimamia itaendeleza jitihada za kuinua Sanaa ikiwemo filamu kwa kutafuta wafadhili wa kusaidia tasnia hiyo kama ilivyofanyika kwa upande wa mpira wa miguu na mbio za riadhaa.

Alisema, Uwigizaji wa Filamu kwa namna moja au nyengine unasaidia kuinua uchumi na kipato cha wananchi kutokana na baadhi ya vijana kujiajiri kupitia sekta hiyo, hivyo Wizara ya habari itatoa msukumo wa kipekee ili kutengeza mazingira mazuri kwa wasanii.

Nae, Mwenyekiti wa Tamasha la Filamu la Nchi za Majahazi (ZIFF) Prof. Martin Mhando alimueleza mgeni rami kuwa taasisi yao itaendelea kufanya kazi nzuri kwa ajili kuitangaza Zanzibar kimataifa kupitia tasnia ya Filamu ili kuwafanya wageni wengi kufika na kuitembelea Zanzibar jambo ambalo litasaidia kuinua sekta ya utalii.

Prof. Mhando alitumia fursa hiyo kuiomba serikali kuiunga mkono ZIFF katika kutatua changamoto mbali mbali zinazowakabili kwa ajili ya kuendeleza tasnia ya Filamu Zanzibar.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.