Habari za Punde

Kuwepo Kwa Wataalamu wa Sheria Wenye Ujuzi ni Mageuzi ya Kiuchumi na Kijamii Nchini.

 

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akihutubia katika hafla ya ufunguzi wa jengo jipya la Mahkama Kuu Zanzibar Tunguu Wilaya ya Kati Unguja, ikiwa ni shamrashamra za kusherehekea maadhimisho ya Miaka 58 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar.(Picha na Ikulu) 

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi  Dk. Hussein Ali Mwinyi amesema kuwepo kwa wataalamu wa sheria wenye ujuzi ni muhimu katika kuleta mageuzi ya kiuchumi na kijamii nchini.

Dk. mmwinyi amesema hayo katika hafla ya Ufunguzi wa jengo la Mahakama Kuu, liliopo Tunguu Mkoa wa Kusini Unguja.

Alisema juhudi za Serikali za kuimarisha majengo na upatikanaji  wa vifaa, hazina budi kuambatana na utoaji wa mafunzo, ambapo wafanyakazi wa kada ya sheria watapata fursa ya kushiriki; ndani na nje ya nchi na hivyi kufanikisha dhamira ya kukuza uchumi.

Alisema Wataalamu wa sheria wanapaswa kuishauri Serikali katika masuala muhimu mbali mbali muhimu ya maendeleo, ikiwemo uandaaji wa mikataba mbali mbali na Taasisi za Kimataifa.

Alieleza kuwa kukamilika kwa ujenzi wa jengo hilo ni hatua muhimu katika kutekeleza azma ya Serikali ya kuweka mazingira bora ya kufanyia kazi katika Utumishi wa Umma, kama ilivyobainisha katika mkakati wa mabadiliko katika Utumishi wa Umma wa 2010.

Dk. Mwinyi alisema kwa miaka mingi Mhimili wa Mahakama ulikuwa ukikabiliwa na changamoto  ya ufinyu wa nafasi na uchakavu wa majengo, mengi yake yakiwa yamerithiwa kutoka kwa Wakoloni, ikiwemo Jengo la Mahakam Kuu liopo Vuga, Jijini Zanzibar.

Alieleza kuwa uchakavu wa jengo hilo umesababisha kuwepo kwa changamoto nyingi za kiutendaji.

Alisema Serikali itaendelea na dhamira yake ya kujenga majengo ya kisasa na kuweka  vifaa vya kufanyia kazi vinavyoendana na mabadiliko na mahitaji ya wakati uliopo.

Alitoa wito kwa watumishi wa Umma kutunza vifaa na mejengo yaliiopo katika maeneo yote ya kazi kwa kutambua kuwa ni mali ya wananchi.

Rais Dk. Mwinyi aliuagiza Uongozi wa Mahakama kuendelea kulitunza jengo la Mahakama liliopo Vuga, huku akisisitiza azma ya Serikali ya kulifanya eneo la Mji Mkongwe kutumika kwa shughuli za utalii, sambamba na kubainisha azma ya Serikali ya  kuhamisha ofisi zote za serikali  ziliomo katika eneo hilo ili kulifanya eneo hilo kuwa maalum kwa shughuli za Utalii.

Alimshukuru Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Awamu ya saba Dk. Ali Mohamed Shein kwa maono na kuja na wazo la ujenzi wa jengo jipya la Mahakama, na kusema uamuzi wake ulikuwa ni wa kimaendeleo.

Akigusia changamoto zinazoihusu Mahakama, aliagiza Uongozi wa Mahakama  kuendeleea kuzitafutia ufumbuzi changamoto mbali mbali zinazoikabili mhimili huo.

Alisema Ujenzi wa Jengo hilo ni mikakati ya serikali katika kuimarisha utoaji wa huduma kwa wananchi, na kubainisha uwezo wa serikali wa kupanga na kutekeleza miradi ya maendeleo kwa kutumia rasilimali zake wenyewe.

“Ujenzi wake umezingatia mahitaji ya wananchi kwa namna tofauti, ikiwemo upatikanaji wa huduma za Benki na watu wenye mahitaji maalum…..ni imani yangu kuwa watendaji watakaofanyakazi katika jengo hili watafanya kazi kwa kuzingatia uwabikaji na uadilifu”, alisema.

Alisema vifaa na mifumo iliomo katika jengo hilo itawawezesha watendaji kufanyakazi kwa weledi na umakini mkubwa.

Nae, Kaimu Jaji Jaji Mkuu Zanzibar Khamis Ramadhan Abdalla alisema ujenzi wa jengo hilo umekuja kunatokana na jengo la Mahakama Kuu liliopo Vuga kuwa na changamoto nyingi, ikiwemo ya ufinyu wa Ofisi, kutokuwa rafiki kwa jamii ya watu wenye ulemavu pamoja na kutokuwa na mfumo wa Tehama.

Alisema wakati wa kipindi cha vikao vya  Mahakama ya Rufaa, baadhi ya Majaji hulazimika kuchukua likizo ili kupisha Majaji wa Mahakama ya Rufaa kuendelea na majukumu yao.

Alisema changamoto kubwa inayokabili Mahakama katika usikilizaji wa kesi za Udhalilishaji ni kwa mashahidi  kushindwa kufika Mahakama kutoa ushahidi, huku baadhi ya nyakati wahusika wa kesi hizo wakibainika kufunga ndoa.

Kaimu Jaji Ramadhan, alitumia fursa hiyo kuiomba Serikali kufikiria uwezekano wa kujenga jengo jipya la Mahakama Kisiwani Pemba, kufuatilia lile liopo hivi sasa katika eneo la Kichungwani   Chakechake kuwa katika mazingira yasiofikika kirahisi kutokana na changamoto ya ukuaji  wa Mji.

Aidha, Waziri wa Nchi (OR) Katiba, Sheria, Utumishi wa Uma na Utawala Bora Haroun Ali Suleiman alisisitiza  haja ya watendaji wa Mahakama kuwajibika ipasavyo kiutendaji ili kwenda sambamba na mazingira halisi ya jengo hilo.

Katika hatua nyengine, akitoa ‘Salamu za mahakama ya Tanzania’, Jaji Mkuu wa Tanzania Pro. Ibrahim Khamis Juma alisema ujenzi wa jengo hilo ni kielelezo cha dhamira ya Serikali katika kuhakikisha mhimili wa Mahakma unawezeshwa, hivyo akaiomba Serikali kuendelea na uwezeshaji huo hadi ngazi za chini.

Alisema jengo hilo ni zuri na linalotoa matumaini katika utoaji wa haki, hivyo akabainisha mtihani unaowakabili watendaji wa Mhimili huo katika kuhakikisha matumaini ya wananchi yanafikiwa, kuendana na mahitaji ya ujenzi wa Uchumi wa Buluu.

Aliwataka Majaji na Mahakimu kujiwekea taratibu za kuwajibika na kuhakikisha jengo hilo linaendana na kasi ya maendeleo ya Zanzibar, huku kuahidi Mahakama Kuu ya Tanzania kuendelea kushirikiana kikamilifu na Mahakama Kuu ya Zanzibar.

Mapema, Mtendaji Mkuu wa Mahakama Kai Bashiru Mbarouk  alisema Jengo hilo la Mahakama Kuu liliopo Tunguu  limegharimu shilingi Bilioni 16.8, ambapo fedha zote hizo kwa asilimia mia moja  zinatoka katika mfuko wa  serikalini. 

Alisema jengo hilo lililojengwa na Kampuni ya Advent Construction Limited limejengwa katika eneo la Ekari 4.3 likiwa ni la Ghorofa nne ambapo msingi wake ni wa Ghorofa saba, ambapo ujenzi wake umezingatia mambo mbali mbali kuhimu ikiwemo Usalama.

Alieleza baadhi ya wakati ujenzi wa jengo hilo ulilazimika kusimama kutokana kujitokeza kwa changamoto mbali mbali , ikiwemo ukosefu wa mchanga wenye sifa unaohitajika, pamoja na kuibuka kwa janga la Ugonjwa wa Uviko – 19, hali iliyochelewesha uletaji wa vifaa.

Mkuu wa Mkoa Kusini Unguja Hadidi Rashid Hadidi, alisema pamoja na vyombo vya Sheria kufanikiwa katika ushughulikia wa makosa ya Udhalilishaji , bado uendeshaji wa kesi hizo unakabaliwa na tatizo kubw akwa baadhi ya Wazazi kushindwa kushirkiana na vyombo hivyo vya sheria.

Imetayarishwa na kitengo cha Habari,

Ikulu Zanzibar.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.