Habari za Punde

Miradi mikubwa ya uwekezaji, Serikali kuzingatia maslahi mapana ya wananchi - Dk Mwinyi


 

                               STATE HOUSE ZANZIBAR

                       OFFICE OF THE PRESS SECRETARY

                                          PRESS RELEASE

 

Zanzibar                                                                        January 20, 2022

 

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi  Dk. Hussein Ali Mwinyi  amesema Serikali itazingatia maslahi mapana ya wananchi katika utekelezaji wa mradi mkubwa  wa Uwekezaji uliopangwa kufanyika  katika eneo la Kizingo, Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja.

Dk. Mwinyi amesema hayo wakati alipofanya mkutano na waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali hapa nchini, mara baada ya kuwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume kufuatia kukamilika kwa ziara yake ya siku tatu ya Kiserikali  aliyofanya katika nchi za Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE).

Alisema Serikali inatambua na kuthamini shughuli mbali mbali zinazofanywa na wananchi, ikiwemo Wavuvi katika eneo hilo la Kizingo, hivyo itahakikisha inazingatia namna bora ya kuliendeleza eneo hilo na kuwapatia wazawa maeneo ya michezo, ajira na mafunzo kutokana na mradi utakaowekezwa, sambamba na maeneo mengine ya visiwa ambako miradi mingine ya aina hiyo itafanyika.

Alisema kupitia ziara hiyo kuna Kampuni kubwa zilizoonyesha nia ya kuwekeza hapa nchini na kubainisha sekta tano zitakazofanyiwa kazi, ikiwemo ya ujenzi wa Bandari ya Mangapwani ambayo inahusisha bandari tofauti, ikiwemo ya Mafuta na Gesi.

Kuhusiana na sekta ya Uvuvi, Dk.Mwinyi alisema kuna Wawekezaji watakaoanzisha Viwanda vya kuchakata samaki, hatua itakayokwenda sambamba na harakati zinazofanywa na wananchi katika ufugaji wa samaki.

Alisema katika kuimarisha sekta ya Utalii, kuna Wawekezaji watakaokuja kwa ajili  kuanzisha ujenzi wa Kumbi za Mikutano, hatua itakayochochea ujio wa watalii na wageni mbali mbali hapa nchini.

Aidha, Dk. Mwinyi alieleza kuwa Muwekezaji anaewekeza katika mradi mkubwa Hoteli  eneo la Kizingo, atakuwa na mradi mwengine wa ujenzi wa Hoteli kubwa ya Kitalii ya Nyota sita (six stars)  katika eneo la Matemwe, Mkoa Kaskazini Unguja, huku akibainisha utayari muwekezaji  kuwekeza katika moja ya Visiwa vidogo viliopo hapa nchini.

Katika hatua nyengine, Dk. Mwinyi alitumia fursa ya ziara hiyo kukumbushia  ahadi zilizotolewa na Serikali ya Abu Dhabi kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar  (awamu iliyopita), kuhusiana na ujenzi wa Hospitali ya Wete Pemba, ujenzi wa Barabara ya Fumba – Kisauni pamoja na Fedha za Uwezeshaji wa Vijana Dola Milioni 10, na  Serikali hiyo kuhakikisha fedha hizo zitapatikana hivi karibuni.

Vile vile, alisema Serikali hiyo imekubali kurejesha safari za Ndege zilizokuwa zikifanywa na Shirika la  Ndege la Fly Dubai hadi Zanzibar, pamoja na safari za Ndege za Shirika la Emirates zilizokuwa zikifanyika hadi Dar es Salaam na kubainisha kuwa safari za Shirika hilo  hivi sasa zitafika hadi  Zanzibar.

Alisema hatua hiyo imekuja baada ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuahidi  kutumia njia bora na sahihi katika upimaji wa Ugonjwa wa UVIKO-19.

Rais Dk. Mwinyi aligusia juu ya uendelezaji wa mji mpya katika eneo la Hoteli ya Bwawani, ambapo eneo la Hekta 260 litatumika, na kueleza kuwa kuna Wawekezaji walionyesha nia ya kuja kuendeleza mazungumzo kati yao na Serikali kupitia mradi huo unaotarajiwa kuzalisha ajira kwa kiwango kikubwa.  

Alisema ana matumaini makubwa kuwa ziara hiyo itafungua milango ya Uwekezaji hapa  Zanzibar na kusema tayari Serikali imetoa kiwanja kwa ajili ya ujenzi wa Ofisi za Ubalozi mdogo wa UAE hapa Zanzibar ili kurahisisha shughuli za uwekezaji wa miradi mbali mbali na shughuli za kidiplomasia.

Alisema Serikali itaendelea kuwajengea maaizngira  bora Wawekezaji, kwa kuhakikisha hawapati usumbufu au urasimu katika shughuli wanazofanya, sambamba na miradi inayoanzishwa  kuhakikisha inazinufaisha  pande  zote mbili.

Katika ziara hiyo, ambapo Rais Dk. Mwinyi aliondoka nchini Januari 16, 2022, pamoja na mambo mengine alishuhudia utiaji wa saini wa miradi mikubwa ya Uwekezaji kati ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Kampuni ya ‘Eagle Hills Regional  Properties’ ya UAE.

Imetayarishwa na Kitengo cha Habari,

Ikulu Zanzibar

 

 

 

 

 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.