Habari za Punde

Wanaharakati Z’bar waitaka ofisi ya msajili wa vyama vya siasa kubadili sheria kumuwezesha mwanamke kushika nafasi za uongozi

Katibu mkuu ofisi ya Rais fedha na mipango Dkt,Maliki Juma Akili alipokua akizungumza katika mdahalo huo wa siku moja uliolenga kutazama nafasi ya wanawake katika uongozi na ushiriki wao kwenye masuala ya kidemokrasia Zanzibar.
Mwanachama wa CUF Nadhira Ali Haji akichangia mada katika mdahalo huo na kueleza baadhi ya changamoto ambazo wanawake wanakutana nazo.
Mwakilishi wa ubalozi wa Norway Nchini Tanzania Anette Otilie Pettersen akijadiliana jambo la katibu mkuu ofisi ya Rais fedha na mipango Zanzibar Dkt,Maliki Juma Akili.
Mwakilishi wa ubalozi wa Norway Nchini Tanzania Anette Otilie Pettersen akitoa neno kwa lililonga kuwahamaisha wanawake kuendelea kushiriki katika nafasi za uongozi na umuhimu wao katika masuala ya kidemokrasia.
Mkurugenzi wa TAMWA-ZNZ  Dr Mzuri Issa (katikati) akiongoza baadhi ya viongozi wengine waliohudhuria katika mdahalo huo kuonesha ishara ya kupokea ugeni.
Baadhi ya washiriki wa mdahalo huo wa siku moja wakifuatilia kwa umakini uwasilisilishwaji wa mada katika kongamano hilo.

Muhammed Khamis,TAMWA-ZNZ

 


 

Wanaharakati kutoka Asasi mbali mbali za kiraia na vyama vya siasa visiwani  Zanzibar wamesema wakati umefika kwa ofisi ya Msajili wa vyama vya siasa Nchini  kuweka sheria maalumu ambayo itawalazimisha viongozi wa vyama vya siasa kuzingatia usawa wa kijisia katika za uongozi ndani ya vyama vya siasa na hata za ushiriki katika vyombo vya kutunga maamuzi ikiwemo Bunge na Baraza la wawakilishi.

 

Walisema Zanzibar ya sasa tafauti na hali ilivyokua awali kutokana na jitihada za asasi za kiraia ikiwemo TAMWA-ZNZ  wanawake wengi wamekua na muamko na kujitokeza kugombea nafasi za kisiasa licha ya kuwa bado wengi waoa hawajafikia malengo tofauti na miaka ya nyuma.

 

Walisema iwapo mkakati maalumu wa kisheria utawekwa ikiwemo ofisi ya msajili wa vyama vya siasa kueka  wazi katika sheria ambayo ataainisha idadi ya ushiriki wa wanawake katika nafasi za vyama na nafasi za  kugombea basi ndio sehemu pekee ambayo itaongeza idadi kubwa ya ushiriki wa wanawake katika nafasi za uongozi na demokrasia.

 

Nadhira Ali Haji kutoka chama cha wananchi CUF alisema kwa miaka mingi bado wanawake wameshindwa kutimiza malengo yao huku akitaja baadhi ya sababu kuwa ni pamoja na kukosekana kwa utayari kwa baadhi ya viongozi ambao wanafanya maamuzi kupitia vyama vyao.

Alisema kazi kubwa bado inahitajika kwa wanawake na asasi nyengine zote kila mmoja kuona kuwa nafasi za uongozi hazipaswi kuwa za wanaume pekeao bali hata wanawake wanahitaji nafasi hizo na wanaweza kuzifanyika kazi ipasavyo.

 

Nae mhadhiri kutoka Chuo kikuu cha Taifa Zanzibar (SUZA) Lulua Salim alisema watu wenye mamlaka kupitia vyama vyao wamekua wakiwaona wanawake kama sehemu isiokua na mchango mkubwa kwenye harakati za kisiasa na ndio maana wamekua wakitumiliwa kama sehemu ya kuwapandisha wengine daraja.


Akizungumzia nafasi ya mwananamke katika dini, mwanaharakati wa masuala ya jamii na dini, Ukhti Amina Salum Khalfan, alieleza wanawake na wanaume wana nafasi sawa kwenye dini na kila mmoja ameelezwa na kupandishwa daraja kwa nafasi yake katika ustawi wa jamii zao.

 

Awali akifungua kongamani hilo katibu mkuu ofisi ya Rais fedha na mipango Zanzibar Dkt,Malik Juma Akili amesema jamii inpaswa kufahamu kuwa kuongozwa ama kuwapa wanawake nafasi ya uongozi ni baraka ambayo kila mmoja anapaswa kujivunia.


Alisema tafiti zinaonesha kuwa hali imebadilika sana na wanawake wengi wamekua na muamko wa kushika nafasi za uingozi hivyo inapotokea mtu ama kikundi cha watu kuwanyima fursa wanawake ni sawa na kutowatendea haki.


Alisema mwanamke ni mtu kama walivyo wengine na bila shaka hwenda wanawake wamepewa uwezo  mkubwa zaidi kutokana utulivu wao wanapoongoza na kusisitiza hakuna tena sababu ya kuwanyima wanawake funrsa za uongozi na ushiriki wao katika demokrasia.


Nae Mkurugenzi wa Chama cha Waandishi wa habari wanawake TAMWA-ZNZ Dkt,Mzuri Issa alisema licha ya jitihada mbali mbali zinazoendelea kufanyika lakini bado wanawake wengi wanaedelea kukabiliwa na changamoto katika kutimiza malengo yao.


Akitaja changamoto hizo alisema ni pamoja na ukosefu wa takwimu za uhakika Zanzibar ambazo zingeweza kusaidia mkakati maalumu wa kuwawezesha wanawake kushika nafasi za uongozi.


Kwa upande wake  mwakilishi wa ubalozi wa Norway Nchini Tanzania Anette Otilie Pettersen alisema uwezeshwaji wanawake katika demokrasia Zanzibar ni kigenzo muhimu ambacho kinapaswa kuzingatiwa na wao kama Norway watahakikisha wanaedelea kuunga mkono harakati hizo visiwani hapa kwa lengo la kuhakikisha dhamira hiyo inatimia.

 

Kongamano hilo la siku moja limeandaliwa na TAMWA-ZNZ,PEGAO,ZAFELA kwa kushirikiana na Ubalozi wa Norway Nchini Tanzania huku lengo kuu likiwa ni kutazma nafasi ya ushiriki wa wanawake katika nafasi za uongozi pamoja na demokrasia.

 

 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.