Habari za Punde

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Akagua Miradi ya Maendeleo Kisiwani Pemba.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe., Hemed Suleiman Abdulla akizungumza na Wakandarasi wakati wa ziara yake kukagua Miradi ya Maendeleo katika Mkoa wa Kusini Pemba, inayojengwa kupitia Fedha za Mkopo wa IMF. (Picha na OMPR)

Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeamua kuwapa Wakandarasi wazawa kujenga  majengo ya miradi ya Serikali ili kuunga mkono juhudi  zinazochukuliwa na Serikali ya Awamu ya Nane inayoongozwa na Rais Dr. Hussein Ali MWINYI.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla alitoa kauli hiyo wakati wa muendelezo wa ziara ya kukagua miradi ya maendeleo Mkoa wa Kusini Pemba inayojengwa kwa fedha za mkopo wa IMF.

Alisema ni Imani ya Serikali kuwa Wakandarasi hao watasimamia ujenzi wa miradi waliyopewa kwa ufanisi wa hali ya juu ili kuweza kukamilisha miradi hiyo kwa kiwango na kwa wakati uliopangwa.

Mhe. Hemed alieleza kuwa Serikali imeelekeza fedha hizo katika ujenzi wa Skuli na Hospitali maeneo ambayo yanawagusa moja kwa moja wananchi wa Zanzibar ili kumaliza tatizo la huduma hizo ambalo lilikuwa likiwakabili wananchi wa Zanzibar kwa muda mrefu.

Kwa upande wao wananchi wa maeneo yalionufaika na Miradi hiyo waliishukuru Serikali ya Awamu ya Nane inayoongozwa na Rais Dr Hussein Ali Mwinyi kwa kuwasogezea huduma hizo muhimu karibu na maeneo yao ya makaazi ambapo ilikuwa ndio kilio chao kikubwa. 
 
Katika ziara hiyo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alipata fursa ya kutembelea nakukagua Bohari Kuu ya Dawa Pemba ambapo hakuridhishwa na mwenendo wa Bohari hiyo na kumuagiza Mkurugenzi Mkuu Wizara ya Afya Zanzibar kuhakikisha Dawa zinakuwepo za kutosha kisiwani Pemba ili kuondosha changamoto ya Dawa kisiwani humo na kuongeza kuwa Serikali itasimamia upatikanaji wa kutosha wa huduma hizo kwa wananchi wake.

Mapema asubuhi Mhe. Hemed alitembelea Hospitali ya Abdallah Mzee Mkoani Pemba kujionea huduma  ya CT Scan iliyofungwa Hospitali hapo wiki mbili zilizopita  iliyogharimu Zaidi ya Dola Laki saba za Kimarekani.

Katika ziara hiyo Mhe. Hemed alimuagiza Mkurugenzi Mkuu Wizara ya Afya kuhakikisha wanamuhamisha Mtaalamu  Mmoja wa Mionzi kutoka Hospitali ya Rufaa Mnazi mmoja na kupangiwa kazi katika Hospitali ya Abdallah Mzee Pemba ili kukabiliana na uhaba wa wataalamu hao.

Imetolewa na Kitengo cha Habari (OMPR)
12 Februari 2022
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe.Hemed Suleiman Abdulla akitembelea Hospitali ya Abdallah Mzee Mkoani Pemba kujionea huduma  ya CT Scan iliyofungwa Hospitali hapo wiki mbili zilizopita  iliyogharimu zaidi ya Dola laki saba za Kimarekani. ili kutowa huduma hiyo kwa Wananchi wa Pemba.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.