Habari za Punde

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe.Hemed Suleiman Abdulla Amefanya Ziara Katika Bandari Kuu ya Malindi Zanzibar.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe.Hemed Suleiman Abdulla akizungumza na Uongozi wa Shirika la Bandari Zanzibar wakati wa ziara yake katika Bandari ya Malindi Zanzibar aliyoifanya leo kuangalia utendaji kazi wa bandari hiyo.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar ameutaka Uongozi wa Shirika la Bandari la Zanzibar kuongeza kasi ya kiutendaji ili kurahisisha Huduma zao kwa  wale wanaowahudumia .

Wito huo umetolewa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla alipofanya ziara ya kukagua eneo  linalotumika kushushia na kupakia Makontena Bandarini Malindi Jijini Zanzibar. 

Amesema Muamko wa Wafanyabiashara kwa  Wenye Meli za Mizigo ni mkubwa ambao umeamsha ari kutokana na Uongozi wa Awamu ya Nane  ili wananchi wapate huduma mbali mbali kwa urahisi. 

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amesema muitiko wa Meli kubwa za Kimataifa kuja kushusha Mizigo Zanzibar ni jitihada za Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt Hussein Ali Mwinyi kuwaomba na kuwashawishi Wafanyabiashara kuweza kuleta mizigo yao Zanzibar kwa kuwepo kwa taratibu nzuri zinazowaongoza katika Shughuli zao.

Pamoja na mambo mengine Mhe. Hemed amekemea tabia ya Wafanyabiashara wanaotoa mizigo wakati wa usiku ambao hufanya hivyo kwa kutaka kufanya  udanganyifu kwa lengo la kuikosesha Serikali mapato, na kueleza kuwa hatua hiyo inapelekea kuwepo kwa mwanya wa vitendo vya rushwa eneo hilo. 

Kwa upande wake Naibu Mkurugenzi wa Shirika la Bandari Zanzibar Ndugu Akif Ali Khamis ameeleza kuwa licha ya udogo wa eneo la kuhifadhia Makontena bado wanaendelea kuzungumza na wafanyabiashara wanaoleta mizigo kutoa mizigo kwa wakati hatua ambayo inatoa nafasi kwa wafanyabiashara wengine kushusha mizigo yao na kutanua uchumi wa Nchi jambo ambalo ndio ndoto ya Serikali ya Awamu ya Nane.

Imetolewa na Kitengo cha Habari (OMPR)
24 Februari 2022.



No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.