Habari za Punde

Mkurugenzi TAMWA-ZNZ asikitishwa na wanaotaka mabadiliko ya sheria kumtia hatiani mtoto wakike anaebakwa

 

Na Muhammed Khamis,TAMWA-ZNZ

Mkurugenzi wa Chama cha Waandishi wa habari wanawake TAMWA-ZNZ Dkt,Mzuri Issa amesema mtazamo wa baadhi ya wanajamii kutaka watoto wakike  wanaobakwa waliofikisha miaka ­(15) wawe sehemu ya kupata adhabu kisheria ikiwemo kufungwa wanapaswa kufikiri upya na kubadili mtazamo huo.


Aliyasema hayo wakati alipokua akizungumza na baadhi ya wanafunzi katika warsha maalumu ilioandaliwa na klabu ya jinsia katika chuo kikuu cha kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere kampasi ya karume Zanzibar.


Alisema katika siku za hivi karibu wamekua wakijitokeza baadhi ya watu kudai mabadiliko ya sheria ya mtoto na kutaka mtoto yoyote wa kike anaefikisha mika 15 na kujihusisha na mapenzi awe sehemu ya adhabu ikiwemo kufungwa gerezani na wasiwe wanaume pekee ndio wanaostahili kupewa adhabu hiyo.

 

Alisema lazima jamii itafakari upya na kufahamu kuwa mara zote mtoto wa kike hushawishiwa na mwanaume na ndipo hujikuta wakifanya vitendo visivyokua visivyopata baraka ya ndoa ukizingatia wengi wa watoto wakike wenye umri huo hua ni umri wa balekh.

 

Alieleza kuwa haiwezekani na haingii akilini kutaka mtoto wakike aadhibiwe ukizingatia baadhi yao wapo wanaolazimishwa na wakati mwengine hata kubakwa.

 

‘‘Haingii kabisa akilini mtoto abakwe kisha kwa sababu tu kafikisha umri wa miaka 15 pia sheria imuadhibu ikiwa ni pamoja na kufungwa gerezani hili hapana na nilazima kila mmoja asimame kulipinga kwa maslahi ya Taifa‘‘alisisitiza Dkt,Mzuri.

 

Akiendelea kufafanua zaidi Mkurugenzi huyo alisema kuna kitu ambacho hwenda wanajamii hawakijui undani wake lakini mara nyingi watoto wenye umri mdogo wanaojihusisha na mapenzi ni wahanga wa vitendo vya ubakwaji tangu wakiwa wadogo na ndio maana mara nyingi watoto wa aina hii huendelea na tabia hiyo kutokana na kuathiriwa kwao kisaikolojia.

 

Kutokana na mazingira ya aina hiyo alishauri kuwe na mbinu zaidi za kuwalinda watoto wakike ikiwemo elimu zaidi kutolewa kwa watoto na wazee wa kiume kuhusu umuhimu wa kulinda heshima ya mtoto wa kike kwenye jamii zao.


Alisema ndani na nje ya Zanzibar ni nadra sana kukuta familia wakiwafahamisha watoto wao wa kiume  kuhusu kuheshimu na kulinda heshima mtoto wakike bali ni watoto wakike pekee ndio hupewa elimu ya kujilinda wenyewe huku wenza wao wakiachiwa bila kupewa elimu, na kusema hwenda ni miongoni mwa sababu zinazopelekea matendo haya kuongezeka.


Kwa upande wake Mkuu wakitengo klabu  ya jinsia chuoni hapo Dkt,Venancy Kalumanga alisema wanamkakati wa kuanzisha klabu za jinsia katika skuli mbali mbali visiwani hapa kwa  lengo kupambana na vita dhidi ya udhalilishaji.

 

Alisema kutokana na kuongezeka kwa wimbi la udhalilishaji ni wazi kuwa mapambano dhidi ya matendo hayo haipaswi kuachiwa Serikali pekee bali kila mmoja anapaswa kuwajibika kwa namna ambayo anadhani itaweza kusaidia kupunguza au ikiwezekana kumaliza kabisa.

 

Akizungumza katika warsha hiyo  Mkuu wa dawati la jinsia Wilaya ya mjini Magharib Unguja ,Mkaguzi wa Polisi Muhammed Mwadini Kificho alisema elimu zaidi inahitajika kwa kuwa hadi leo hii wapo baadhi ya watu hawajayapa uzito matukio ya udhalilishaji.

 

Alitolea mfano kwa mwezi januari pekee mwaka 2021 vitendo vya udhalilishaji 52 viliripotiwa katika dawati hilo ambapo kwa mwezi januari mwaka huu matukio 21 yameripotiwa na mengi katika hayo ni watoto wa kike kuingiliwa kinyume na maumbile.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.