Habari za Punde

One Stop Centre kuanzishwa kila Wilaya

Na Kassim Abdi 

 Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi kupitia Wakala wa Miundombinu ya TEHAMA inakusudia kuanzisha vituo vya kutolea huduma za pamoja (ONE STOP CENTRE) kwa Kila Wilaya ili kuwarahisishia huduma mbali mbali wananchi wa Zanzibar.

Mkurugenzi Mtendaji wa Wakala wa Miundombinu ya TEHAMA Zanzibar Mhandisi Shukuru Awadh Suleiman ameleza hayo Ofisini kwake Mazizini Jijini Zanzibar wakati akifanya mahojiano na waandishi wa habari.

Amesema Serikali inakusudia kufikisha huduma kwa wananchi wake hasa wa vijini kwa kuwaondoshea usumbufu wa kufuata huduma mjini ikiwemo huduma za vyeti vya kuzaliwa pamoja na stakabadhi nyengine muhimu.

Aidha, ameleeza kuwa Wizara tayari imetiliana saini na kampuni ya simu za Mikononi Zantel kwa ajii ya ujenzi wa minara katika maeneo tofauti ya Zanzibar kwa ajili ya kuongeza nguvu za upatikanaji wa mawasiliano.

Akizungumzia suala la ukuwaji wa uwekezaji Mhandisi Shkuru amesema Wizara kupitia Wakala wa Miundombinu ya TEHAMA inakusudia kuimarisha miundombinu yake ili kuwavutia wawekezaji zaidi kwenda sambamba na azma ya Serikali ya awamu ya nane inayoongozwa na Rais Dk. Hussein Mwinyi.

Mhandisi Shkuru amesema, Wakala wa Miundombinu wa TEHAMA imefanikiwa kulaza miundombinu yake katika Wilaya zote Kumi na moja Unguja na Pemba na wanahudumia zaidi ya taasisi Mia Mbili (200) ambapo katika bajeti ijayo 2022/2023 inakusudia kwenda kuziunganisha taasisi zote za Serikali na Mkongo wa taifa ambazo bado hazijaunganishwa.

Pia, ameeleza kwamba, Zanzibar ina mpango wa kuanzisha Mji wa TEHAMA (Cyber City) utakaojumuisha kuanzishwa kwa kampuni mbali mbali kutoka ndani na nje Nchi (Technology Park) zitakazosaidia kushajihisha ukuaji wa maendeleo na kutoa huduma kwa urahisi.

Akizungumzia Sera ya uchmi wa Buluu Mhandisi Shkuru amesema Mfumo wa TEHAMA una mchango mkubwa katika ukuaji wa Uchumi wa Buluu ambapo kwa kutumia mfumo huo kutawezesha kutangaza shughuli za uvuvi pamoja na masuala ya gesi na mafuta.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.