Habari za Punde

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi Amekutana na Kuzungumza na Uongozi wa AFREXIM BANK Ikulu leo Zanzibar.16-2-2022.

 

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akizungumza na Ujumbe wa Afrexim Bank kutoka Nchini Egypt ukiongozwa na Makamu wa Rais Mtendaji  Bw,Amr Kamel (kulia kwa Rais) walipofika Ikulu Jijini Zanzibar kwa mazungumzo yaliofanyika katika ukumbi wa Ikulu leo 16-2-2022.na (kushoto kwa Rais) Waziri wa Biashara na Maendeleo ya Viwanja Zanzibar Mhe. Omar Said Shaban na Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi Mhandisi Zena Ahmed Said.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk. Hussein Ali Mwinyi ameiomba Benki ya ‘AFREXIM Bank’ kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kupata mchanganuo wa masoko wa zao la Mwani, ili wakulima wa zao hilo hapa nchini waweze kunufaika kikamilifu.

Dk. Mwinyi ametoa ombi hilo wakati alipokutana na Uongozi wa AFREXIM Bank kutoka nchini Misri, uliofika Ikulu Jijini Zanzibar ikiwa ni muendelezo wa mazungumzo  yake na Serikali kwa lengo kubaini maeneo mbali mbali yenye fursa ya Uwekezaji hapa nchini.

Amesema kupitia Sekta ya Kilimo, Zanzibar inategemea  mazao makuu mawili ya Biashara, ikiwemo zao la Mwani ambapo wakulima wa zao hilo wanakabiliwa na changamoto kubwa ya kuuza mwani  kwa  bei ya kiwango cha chini katika masoko.

“Soko la zao la Karafuu liko vizuri, tatizo kubwa liko kwenye soko la zao la mwani, ni eneo ambalo tunahitaji kupata ushirikiano ili kuongeza kuliongezea thamani zao hilo pamoja na kuinua kiwango cha bei ili wakulima wetu waweze kunufaika”, alisema.

Dk. Mwinyi alisema Zanzibar ina maeneo mengi ya uwekezaji kupitia sekta ya Uchumi wa Buluu, ikihusisha sekta ya utalii, mafuta na gesi,uvuvi na kadhalika, hivyo akabainisha umuhimu wa Benki hiyo katika kushirikiana na Serikali kuendeleza sekta hizo.

Alisema Zanzibar inakabiliwa na changamoto ya kuwa na miundo mbinu chakavu isiyokidhi mahitaji ya uhifadhi wa mafuta.  

Rais Dk. Mwinyi alipongeza utayari wa Benki hiyo katika kuendeleza mazungumzo  yatakayofanikisha  kuanzishwa kwa ujenzi wa miundo mbinu ya Kituo cha mikutano ya Kimataifa pamoja na maeneo ya Viwanda.

Aliipongeza Benki ya AFREXIM ina uwezo mkubwa na imekuwa ikishirikiana na Serikali mbali mbali Barani Afrika katika uwekezaji wa miradi mkubwa ya maendeleo.

Aidha, alipongeza juhudi za uongozi wa Benki hiyo wa kukutana na  na Uongozi wa Wizara ya Biashara na Maendeleo ya Viwanda kwa lengo la  kujadili fursa mbali mbali ziliopo nchini, ambapo AFRIMEX Bank inaweza kusaidia katika nyanja mbali mbali ikiwemo utoaji wa mikopo kwa Makampuni mbali mbali.

Nae, Makamo wa Rais Mtendaji, Maendeleo ya Biashara na Benki ya Ushirika ya AFREXIM Bank Amri Kamel alimpongeza mapokezi makubwa waliyopata, sambamba na kupata fursa ya kuona maeneo  mbali mbali  ya Uwekezaji.

Aidha, alisema Uongozi huo utaendelea kuzungumza na taasisi mbali mbali zinazohusika na sekta za uwekezaji pamoja na kufanyia kazi ushauri uliotolewa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi, ili kufanikisha malengo yaliokusudiwa.

Ujio wa Uongozi wa AFREXIM Bank hapa nchini unafuatia ziara iliofanywa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi , mapema mwaka huu nchini Afrika Kusini na kukutana kwa mazungumzo na Uongozi wa Benki hiyo.                                       

Imetayarishwa na Kitengo cha Habari,

Ikulu Zanzibar.

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akizungumza na Ujumbe wa Afrexim Bank kutoka Nchini Egypt ukiongozwa na Makamu wa Rais Mtendaji  Bw,Amr Kamel (kulia kwa Rais) walipofika Ikulu Jijini Zanzibar kwa mazungumzo yaliofanyika katika ukumbi wa Ikulu leo 16-2-2022.na (kushoto kwa Rais) Waziri wa Biashara na Maendeleo ya Viwanja Zanzibar Mhe. Omar Said Shaban na Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi Mhandisi Zena Ahmed Said.

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akimkabidha zawadi maalum ya Mlango wa Zanzibar (Zanzibar Door) Makamu wa Rais Mtendaji wa Afrexim Bank Bw. Amr Kamel, baada ya kumalizika kwa mazungumzo yao yaliofanyika katika ukumbi wa Ikulu Jijini Zanzibar.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.