Habari za Punde

Sheria ya kuanzishwa kwa Mamlaka ya kudhibiti na kupambana na dawa za kulevya imeanza kutumika rasmi MKUTANO NA WAANDISHI WA HABARI KUHUSU SHERIA YA KUANZISHWA  KWA MAMLAKA YA UDHIBITI NA KUPAMBANA NA DAWA ZA KULEVYA  ZANZIBAR 

Ndugu Katibu Mkuu OMKR, 

Watendaji wa OMKR, 

Watendaji wa Mamlaka ya Udhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya, Ndugu waandishi wa Habari, 

Assalam aleikum. 

Awali ya yote napenda kumshukuru Mwenye Enzi Mungu Mwingi wa Rehma kwa kutukutanisha  hapa leo hii, tukiwa wazima wa afya na tukitimiza majukumu ya kulipeleka mbele Taifa letu. 

Ndugu waandishi wa Habari, lengo kuu la kuwaita hapa ni kuutarifu umma kupitia kwenu kuwa  SHERIA YA KUANZISHWA KWA MAMLAKA YA KUDHIBITI NA KUPAMBANA NA  DAWA ZA KULEVYA ZANZIBAR imeshatiwa Saini na Mheshimiwa Rais wa Zanzibar na  Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, na imeanza kutumika rasmi baada ya kutiwa Saini. 

Sheria hii inajulikana kama Sheria ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Zanzibar,  Namba 8 ya mwaka 2021. 

Mantiki na Madhumuni ya sheria hii; 

Madhumuni ya sheria Namba 8 ya 2021 ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya  Zanzibar ni kuanzisha Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya yenye na uwezo kamili wa kupeleleza, kukamata, kuchunguza na hatimae kupeleka Mahkamani mashauri  yanayohusiana na dawa za kulevya Pamoja na makosa mengine yanayofanana nayo. Aidha sheria  hii imefuta taasisi iliokuwa ikisimamia Uratibu wa masuala ya dawa za kulevya nchini ambayo ni  Tume ya Kitaifa ya Kuratibu na Udhibiti wa Dawa za Kulevya na kuanzisha taasisi inayojulikana  kama Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Zanzibar, itakayoongozwa na  Kamishna Mkuu na itakuwa chini ya Baraza la Taifa la Kudhibiti na Kupambana na Dawa za  Kulevya, ambalo linaongozwa na Mwenyekiti wake Mheshimiwa Rais wa Zanzibar na  Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi. 

Tofauti ya Sheria hii na ya zamani; 

Kwa ujumla Sheria hii mpya kwanza, imeanzisha Mamlaka yenye nguvu ya kisheria na thabiti ya kusimamia udhibiti wa dawa za kulevya nchini ambapo, Taasisi hii mpya ina uwezo wa  kuchunguza, kukamata, kupeleleza na kufungua mashtaka mahakamani; 

Kamishna Mkuu au ofisa aliyeidhinishwa anaweza kuhoji, kupeleleza au kufanya ukaguzi kwa  mtu yeyote au kikundi chochote cha watu kadri atakavyoona inafaa;

Kamishna Mkuu au ofisa aliyeidhinishwa, atakuwa na uwezo wa kukagua, kupekuwa, kuzuia,  kukamata, kuweka kizuizini na kufanya uchunguzi kuhusiana na makosa yaliyo chini ya Sheria  hii; 

Kamishna Mkuu au ofisa aliyeidhinishwa ambaye ana sababu za msingi za kuamini kwamba gari,  ndege, meli, chombo cha kubebea mizigo au chombo chengine chochote cha usafiri kimetumika  au kinatumika katika kutenda kosa chini ya Sheria hii, anaweza kukisimamisha, kuingia na  kuifanyia upekuzi gari, ndege, meli, chombo cha kubebea mizigo au chombo chengine cha usafiri  na anaweza kwa madhumuni hayo kuvunja au kufungua mlango na kuondoa kizuizi cha kuingia  ndani ya chombo; 

Endapo mtu anachunguzwa au anashitakiwa kwa kosa chini ya Sheria hii, Kamishna Mkuu  anaweza, pale ambapo anaamini kwamba ushahidi wowote unaohusiana na kosa au mali  unapatikana katika akaunti ya benki, kufanya maombi mahkamani ya amri ya kuzuia akaunti ya  benki; 

Bila ya kujali masharti ya sheria yoyote, Kamishna Mkuu au ofisa aliyeidhinishwa anaweza wakati  wowote kwa madhumuni ya Sheria hii kufanya uvamizi na kuingia katika jengo lolote ambalo  anaamini kwamba kosa limetendeka au litatendeka ndani ya jengo hilo; 

Sheria imeanzisha Baraza la Taifa la Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya, ambalo  linaongozwa na Mwenyekiti wake Mheshimiwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la  Mapinduzi. Baraza litasimamia utekelezaji wa Sera ya Taifa ya Kudhibiti Dawa za Kulevya na  litakuwa ndio chombo kikuu cha maamuzi na lenye usimamizi wa jumla kwa Mamlaka hii jambo  ambalo tunaamini kuwa janga hili la dawa za kulevya litaweza kudhibitiwa kwa haraka na ufanisi  zaidi na pia kutakuwa na usimamizi madhubuti katika kudhibiti na kupambana na dawa za kulevya nchini; 

Kwa sheria hii, Mamlaka inaweza kutoa maelekezo pale itakapohitajika kwa taasisi yoyote ya  Serikali au idara katika kutekeleza masharti ya Sheria hii, na taasisi au idara hiyo itawajibika  kutekeleza maelekezo hayo; 

Sheria hii pia imetoa majukumu ya jumla kwa taasisi za umma katika kuzuia na kupambana na  dawa za kulevya nchini, Baraza litapokea na kuzipitia taarifa za taasisi za umma juu ya majukumu  yao katika kuzuia na kupambana na dawa za kulevya. Taasisi hizo ni: 

(a) Idara ya Usalama wa Taifa Zanzibar; 

(b) Jeshi la Polisi Zanzibar; 

(c) Chuo cha Mafunzo Zanzibar; 

(d) Ofisi ya Uhamiaji Zanzibar; 

(e) Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Zanzibar; 

(f) Shirika la Bandari Zanzibar; 

(g) Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali; 

(h) Mamlaka ya Uvuvi wa Bahari Kuu; na 

(i) Taasisi nyengine yoyote kama Baraza litakavyoona inafaa.

Kwa kuzingatia kwamba kila mmoja anatimiza wajibu wake katika kudhibiti na kupambana na  dawa za kulevya nchini, na kwa kuhakikisha kuwa kwa kiasi kikubwa makosa yanayohusiana na  utumiaji na usafirishaji wa dawa za kulevya yanazibitiwa kwa njia zote, hali itakayopelekea  kupunguza athari zitokanazo na dawa za kulevya nchini, sheria hii imeanzisha Kamati za Kuratibu  Udhibiti wa Dawa za Kulevya katika kila Mkoa ambazo zitaongozwa na Waheshimiwa Wakuu  wa Mikoa husika; 

Lengo la ujumla la sheria Namba 8 ya 2021 ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za  Kulevya Zanzibar; 

Sheria hii imelenga kudhibiti makosa mbali mbali yanayohusu uhalifu wa dawa za kulevya na  makosa yanayo fanana nayo ambapo jumla ya vifugu 26 vimekataza moja kwa moja uhalifu huu  wa dawa za kulevya pamoja na makosa yanayofanana nayo kama: 

Sheria inaharamisha mambo mbalimbali ikiwemo kilimo cha bangi, mirungi, kulima,  kumiliki, kusafirisha, kuuza na kununua mbegu zinazoweza kuzalisha dawa za kulevya  kwa kutoa adhabu ya kifungo cha maisha

Kufadhili biashara ya dawa za kulevya adhabu ya kifungo cha maisha na kutaifisha  mali zote. 

Inaharamisha usafirishaji wa dawa za kulevya, kujihusisha kwa namna yoyote kinyume  cha Sheria na kemikali zinazoweza kuzalisha dawa za kulevya kwa kutoa adhabu ya  kifungo cha maisha

Inaharamisha kumiliki mashine, vifaa na maabara kwa lengo la kutengeneza dawa za  kulevya kwa kutoa adhabu ya kifungo cha maisha na kutaifisha kifaa hicho Pamoja na mali

Mmliki wa jengo kuruhusu jengo litumike kwa uhalifu wa dawa za kulevya, adhabu ni Faini isiyopungua milioni 10 au kifungo kisichopungua miaka 30 au adhabu zote  mbili. 

Sheria imekataza bila ya kuwa na kibali kuingiza, kutoa, kusambaza, kumiliki na kutengeneza kemikali bashirifu, adhabu ni kifungo kisichopungua miaka 30. 

Sheria imetoa adhabu kwa mtu yoyote atakekataa kutoa taarifa ama ushahidi unaohusiana  na uhalifu wa dawa za kulevya au kutoa taarifa za uongo kulipa faini isiyopungua shilingi  milioni 30 na isiyozidi shilingi milioni 50 au kifungo kisichopungua miaka 15 na  kisichozidi miaka 30 au adhabu zote mbili. 

Sheria imekataza kwa namna yoyote ile kusaidia au kusababisha kutendeka au kutenda  uhalifu wa dawa za kulevya na kutoa adhabu sawa sawa na mtenda kosa mwenyewe.

Sheria imekataza kutoa dawa tiba zinazotumika kwa matibabu ambazo zinaweza kutumika  kama dawa za kulevya zinazozibitiwa kisheria kinyume cha utaratibu, inadhibiti matumizi  ya dawa adhabu ni faini isiyopungua Shilingi Milioni Hamsini za Kitanzania au  kifungo kisichopungua miaka thelathini au vyote viwili. 

Sheria imekataza kutumia dawa za kulevya, na akitiwa hatiani, atalipa faini isiyopungua  Shilingi Milioni Tano za Kitanzania au kifungo cha mwaka mmoja au vyote viwili. 

Endapo mtu atajitayarisha au atajaribu kufanya au kutokuzuia kitu kinachosababisha  utendaji wa kosa chini ya Sheria hii, atapewa nusu ya adhabu ambayo angestahiki  kupewa endapo angetenda kosa hilo. 

Mtu atakayekiuka masharti ya kifungu chochote cha Sheria hii, kanuni yoyote au amri  yoyote iliyowekwa chini ya Sheria hii ambapo adhabu yake haikutajwa, ametenda kosa, na  akitiwa hatiani atatumikia kifungo kisichopungua miaka kumi na tano na kisichozidi miaka  thelathini. 

Endapo daktari wa binaadamu, daktari wa meno au daktari wa upasuaji wa wanyama,  ametiwa hatiani chini ya Sheria hii, bila ya kujali masharti ya sheria nyengine yoyote, jina  lake litafutwa katika daftari la usajili na hatofanya kazi ndani ya Zanzibar. 

Endapo kosa limefanywa na kampuni chini ya Sheria hii, mtu ambaye, wakati kosa  linafanyika, alikuwa dhamana na ana jukumu la kusimamia uendeshaji wa shughuli za  kampuni, atachukuliwa kuwa ametenda kosa na, akitiwa hatiani atawajibika. 

Pale ambapo kosa lolote limefanywa na kampuni na imethibitishwa kwamba kosa  limefanywa kwa kuridhiana au kukubaliana au limechangiwa na uzembe wowote kwa  upande wa mkurugenzi, meneja, katibu au ofisa mwengine wa kampuni, mkurugenzi,  meneja, katibu au ofisa mwengine huyo wa kampuni atashtakiwa na kuadhibiwa  ipasavyo na kampuni hiyo itafutiwa usajili au kutaifishwa. 

Mmiliki, mkaazi au mtu anayehusika na usimamizi wa eneo atatakiwa kutoa taarifa haraka  iwezekanavyo kwa Kamishna Mkuu au ofisa aliyeidhinishwa juu ya uwepo, ndani ya eneo  lake, wa mimea ya dawa za kulevya, mazao ya dawa za kulevya au dawa za kulevya  ambazo huenda zimelimwa, zimezalishwa au zimetengenezwa isivyohalali.Ikiwa mmiliki,  mkazi, au mtu anayehusika na usimamizi, ameshindwa kutoa taarifa, ametenda kosa, na  akitiwa hatiani, atalipa faini isiyopungua Shilingi Milioni Kumi za Kitanzania na  isiyozidi Shilingi Milioni Hamsini za Kitanzania au kifungo kisichopungua miaka  kumi na tano na kisichozidi miaka thelathini au vyote viwili. 

Mtu ambaye kwa makusudi au kwa nia ovu anatoa taarifa za uongo zinazosababisha  ukamataji au upekuzi chini ya Sheria hii, ametenda kosa, na akitiwa hatiani, atalipa faini  isiyopungua Shilingi Milioni Kumi za Kitanzania au kifungo kisichopungua miaka  miwili au vyote viwili. 

Ufilisi wa Mali; Endapo mtu yoyote ametiwa hatiani kwa kosa chini ya Sheria hii, au  atatiwa hatiani kwa kosa linalofanana nalo, na Mahakama ya jinai nje ya Zanzibar, mali 

anazomiliki yeye mwenyewe au mshirika wake, alizozipata kutokana na dawa za kulevya  katika tarehe ya mashtaka au baada ya tarehe hiyo zitafilisiwa na kuwa mali za Serikali. 

Endapo mtu atatiwa hatiani na Mahakama nje ya Zanzibar kwa mujibu wa sheria yoyote  inayofanana na masharti ya Sheria hii, atashughulikiwa kama vile ametiwa hatiani na  Mahakama yenye uwezo Zanzibar. 

Kitu chochote kilichotumika kwa ajili ya kufichia dawa za kulevya ambazo zinatakiwa  kutaifishwa chini ya Sheria hii, kitu hicho kitataifishwa. 

Endapo mtu ameuza dawa za kulevya ambazo anafahamu au ana sababu ya kuamini  kwamba dawa za kulevya zinatakiwa kutaifishwa chini ya Sheria hii, mapato ya mauzo  yatataifishwa. 

Endapo mtu atamiliki kitu au mali iliyopatikana isivyo halali ikiwa yeye mwenyewe au  mtu mwengine yoyote kwa niaba yake kinyume na sheria hii, kitu au mali hiyo itafilisiwa  na Serikali. 

Kamishna Mkuu au ofisa aliyeidhinishwa anaweza kutoa amri ya kuzuia kitu au mali  wakati wa kufanya uchunguzi, upelelezi au ufuatiliaji chini ya sheria hii, ikiwa anayo  sababu ya kuamini kwamba kitu au mali yoyote kuhusiana na uchunguzi, upelelezi au  ufuatiliaji uliofanyika imepatikana isivyo halali na kitu au mali hiyo kinaweza kufichwa,  kuhaulishwa au kutumiwa kwa namna ambayo inaweza kuharibu utaratibu wa utaifishaji  wa kitu au mali hiyo chini ya Sehemu hii. 

Tiba  

Sheria hii imetupa uwezo wa kuanzisha vituo vya utambuzi, tiba, elimu, uangalizi, urekebishaji wa tabia ili kuweza kuwarudisha kwenye jamii watumiaji wa dawa za kulevya kwa kuzingatia  masharti na kwa namna kama itakayoelekezwa katika kanuni. 

Tayari kituo chetu cha Tiba na Marekebisho ya Tabia kilichopo Kidimni kimeanza rasmi kutoa  huduma hizo, kituo kinatarajiwa kuwa na mafunzo ya ujasiriaamali kwa wale ambao watakuwa  wanapata huduma ndani ya kituo hicho. 

Wito kwa Jamii 

Kutokana na sheria hii kuwa kali sana, nawanasihi wana jamii ya kizanzibari kujiepusha kwa kila  hali na uhalifu huu wa dawa za kulevya kwani madhara yake kiafya na kisheria ni makubwa sana  kwa mtenda kosa Pamoja na jamii yake husika. 

Ahsanteni kwa kunisikiliza. 

Zanzibar bila ya Dawa za Kulevya inawezekana.


No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.