Na Immaculate Makilika – MAELEZO, Zanzibar
Bodi ya Utalii
Tanzania Bara (TTB) na Kamisheni ya Utalii Zanzibar (ZCT) zimeendelea
kufanyakazi kwa pamoja katika eneo la
Utangazaji wa utalii nchini.
Ambapo imeelezwa kuwa,
utalii una mchango mkubwa katika uchumi wetu. Takwimu zinaonyesha kuwa kwa
mwaka 2019/2020 utalii ulichangia asilimia 17.2 katika pato la Taifa la
Tanzania Bara na asilimia 27 upande wa Zanzibar.
Akizungumza leo akiwa Visiwani Zanzibar, Msemaji Mkuu wa Serikali na Mkurugenzi wa
Idara ya Habari – MAELEZO, Gerson Msigwa wakati akitoa taarifa ya wiki kuhusu
utekelezaji wa miradi ya Serikali katika maeneo mbalimbali nchini, alisema kuwa sekta hii
imekumbwa na changamoto kubwa ya Janga la Uviko-19 lakini juhudi za kukabiliana
na changamoto hizo zimeendelea kuzaa matunda ambapo mwaka 2020 watalii walikuwa
620,867 na sasa wameongezeka hadi kufikia watalii 922,692 Bara na Visiwani.
“Tumepata changamoto
ya janga la ugonjwa wa Korona (Uviko-19) ambapo sekta hii imeathirika na
kusababisha idadi ya Watalii kushuka kutoka 1,527,230 waliotembelea Tanzania
mwaka 2019 hadi 620,867 mwaka 2020. Hata hivyo juhudi tulizozifanya za kuchukua
tahadhari dhidi ya ugonjwa huo na kuwavutia zaidi watalii tumefanikiwa kuanza
kuongeza idadi ya watalii ambapo katika mwaka 2021 idadi imeongezeka hadi
kufikia 922,692,” alisisitiza Msigwa.
Aidha
amesema kuwa, TTB
na ZCT zimeendelea kufanya jitihada mbalimbali katika kuratibu na kushiriki
kuandaa maonesho ya Kimataifa ya Utalii, mfano ni Onesho la Utalii la Jumuiya
ya Afrika Mashariki (EAC Tourism Expo) lililofanyika Arusha kwa mafanikio
makubwa na Dubai Expo 2020 ambayo inaendelea huko Dubai.
Vilevile, kumekuwepo
na ushirikiano wa Sekta Binafsi, Wafanyabiashara wa Sekta ya Utalii wa Bara na
Zanzibar (Tour Operators) ambao wanafanya kazi pamoja hasa katika kupokea
wageni na kuuza safari kwa wageni wanaokuja kutembelea
vivutio vya utalii
nchini.
No comments:
Post a Comment