Habari za Punde

Waziri Mkuu Mhe Kassim Majaliwa Amefungua Mkutano wa Kazi Kati ya TAMISEMI, TARURA na Wakandarasi.

Baadhi ya washiriki wa Mkutano wa Kazi kati ya Ofisi ya Rais TAMISEMI, TARURA na Wakandarasi, wakimsikiliza Waziri Mkuu Kassim Majaliwa wakati  alipofungua mkutano huo, uliofanyika katika ukumbi wa St. Gasper Jijini Dodoma. 
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza wakati alipofungua Mkutano wa Kazi kati ya Ofisi ya Rais TAMISEMI, TARURA na Wakandarasi, uliofanyika katika ukimbi wa St. Gasper  Jijini Dodoma, Februari 12, 2022.
 (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)


WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewaagiza wahandisi wa TARURA wasimamie miradi kwa weledi, uadilifu na uaminifu huku wakizingatia mikataba husika na pia wawe wabunifu kutumia teknolojia mpya, sahihi na rafiki kulingana na upatikanaji wa malighafi za ujenzi.

 

“Pia ninaisisitiza TARURA kufanyia kazi haraka, maelekezo ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kuhusu kujifunza teknolojia inayotumiwa kutengeneza barabara za Zanzibar ambayo imeonesha kuwa nafuu na ya viwango vya juu.”  

 

Ameyasema hayo leo (Jumamosi, Februari 12, 2022) alipofungua Mkutano wa Kazi kati ya Ofisi ya Rais - TAMISEMI, TARURA, Wakandarasi, Bodi ya Usajili wa Wakandarasi, Mfuko wa Barabara na Mamlaka ya Ununuzi wa Umma katika Ukumbi wa Mtakatifu Gasper, Dodoma.

 

Amesema Serikali imefanya jitihada mbalimbali katika kuijengea uwezo TARURA ili iweze kutekeleza makujumu yake ikiwa ni pamoja kuiongezea fedha kutoka sh. bilioni 247.5 ilipoanzishwa mwaka 2017 hadi kufikia Sh. bilioni 752.61 sawa na ongezeko la asilimia 204.3.

 

“Fedha hizo zinajumuisha sh. bilioni 127.50 kutoka Serikali Kuu, sh. bilioni 272.50 kutoka Mfuko wa Barabara, sh. bilioni 322.15 kutoka katika tozo ya sh. 100 kwa lita ya mafuta ya petroli na dizeli na sh. bilioni 30.44 kutoka kwenye ushuru wa maegesho wa magari.”

 

Amesema mwaka 2017, TARURA ilikuwa inasimamia mtandao wa barabara wenye urefu wa kilomita 108,946.19 na sasa mtandao huo umeongezeka na kufikia kilomita 144,429.77 ambazo zimetangazwa rasmi kwenye Gazeti la Serikali Na. 463 la tarehe 25 Juni 2021.

 

Mheshimiwa Majaliwa ameongeza kuwa wakati TARURA inaanzishwa mwaka 2017, barabara za lami zilikuwa kilomita 1,449.55 sawa na asilimia 1.30 na sasa ni kilomita 2,473.55 sawa na ongezeko la kilomita 1,024 sawa na asilimia 70.6.

 

Waziri Mkuu ameiagiza Ofisi ya Rais-TAMISEMI ifuatilie na kuchukua hatua stahiki kwa Halmashauri zote zitakazoshindwa kutekeleza kazi za matengenezo ya barabara kulingana na mkataba wa makubaliano (Annual Performance Agreement).

 

Mheshimiwa Majaliwa ameagiza usanifu wa miradi yote ya vipaumbele ufanyike mapema badala ya kusubiri mpaka fedha zipatikane na hatua za kinidhamu zichukuliwe kwa watendaji wote wanaothibitika kusababisha kazi mbovu na upotevu wa fedha za TARURA.

“Usimamizi wa taratibu za utoaji wa zabuni ufanyike kwa umakini na kwa kuzingatia sheria. Mikataba ya kazi isainiwe kwa wakati, pia tathmini za zabuni zizingatie Sheria ya Ununuzi wa Umma na zihusishe upekuzi ili kupata makandarasi wenye uwezo na kukidhi vigezo stahiki".

Pia, Waziri Mkuu amesema TARURA ianze kutekeleza mpango wa uwekaji taa za barabarani wakati wa ujenzi wa barabara. “Hakikisheni hii inakuwa sehemu ya mkataba wa ujenzi wa barabara zote zinazojengwa, jifunzeni utaratibu huu kutoka TANROADS ambao tayari wanautekeleza”.

Waziri Mkuu amewataka wakandarasi wazawa wajiimarishe katika kazi zao za ujenzi wa barabara ili waweze kufanya kazi yenye ubora, kwa wakati na viwango. “Wakandarasi mnaoomba kazi ni vyema mkajiridhisha na aina, ukubwa, mazingira ya eneo la kazi na kazi mnazoomba ili muweze kujaza gharama za mradi kulingana na uhalisia.”

Amewaagiza watumishi wa TARURA wasijiingize kwenye kazi zenye mgongano wa maslahi. “Waswahili husema mshika mawili moja humponyoka. Kwa mantiki hiyo, ikiwa unataka kufanya biashara na Serikali wakati wewe ni mtumishi ni vyema ukaacha kazi ili ufanye biashara yako kwa ufanisi”.

 

Amewaagiza viongozi wa TARURA wahakikishe wanapoandaa taarifa za miradi wawashirikishe watendaji wa Halmashauri, Wilaya na Mikoa na pia taarifa za utekelezaji zitolewe katika kwa Baraza la Madiwani, Kamati ya Ushauri ya Wilaya (DCC)  na Kamati ya Ushauri ya Mkoa RCC);

Pia, Waziri Mkuu amemuagiza Mtendaji Mkuu wa TARURA, Mhandisi Victor Seff awasilishe kwa Bodi ya Usajili wa Wakandarasi orodha ya wakandarasi wababaishaji na awasilishe nakala kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais –TAMISEMI ili iwasilishwe kwa Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi kwa hatua zaidi za kinidhamu.

Naye, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Innocent Bashungwa amesema Serikali ina matumaini makubwa kupitia watendaji hao na kwamba changamoto zote zinazowakabili hazina budi kufanyiwa kazi kwa wakati ili waweze kutoa huduma bora kwa Watanzania.

Amesema wahakikishe kila mmoja anatekeleza majukumu yake ipasavyo ikiwa ni pamoja na kufanya kazi kwa weledi na kwa viwango vinavyotakiwa ili barabara wazazosimamia zinapitika kwa wakati wote. “Hayo ndio maono ya Mheshimiwa Rais Samia.”

Waziri Bashungwa ameagiza asilimia 60 ya kazi za TARURA zitangazwe mapema, bila kusubiri mpaka mwaka wa fedha uanze ili pale mwaka wa fedha unapoanza iwe ni wakandarasi kuanza kazi.

Awali, Mtendaji Mkuu wa TARURA, Mhandisi Seff alisema miongoni mwa changamoto zinazowakabili ni pamoja na baadhi ya makandarasi kuomba kazi nyingi na wakati mwingine kupata kazi nyingi kuliko uwezo wao, hivyo hulazimika kusubiri hadi kazi iishe eneo fulani ndipo wapeleke vifaa na kuanza kazi eneo jingine.

IMETOLEWA NA:

OFISI YA WAZIRI MKUU,

JUMAMOSI, FEBRUARI 12, 2022.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.