Habari za Punde

Dkt. Stergomena Lawrence Tax amefanya ziara Zanzibar kutatua mgogoro wa ardhi

Waziri wa Ulinzi na Jeshi la kujenga  Taifa  Dkt.Stergomena Lawrence Tax akizungumza na wananchi wa kisakasaka kuhusu utatuzi wa mgogoro wa ardhi uliopo baina yao na Jeshi huko kisakasaka wilaya ya Magharibi “B” Mkoa wa Mjini Magharibi.
Mkuu wa Wilaya ya Maghribi "B"Hamida Mussa Khamis akizungumza machache na kumkaribisha Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) Dkt.Stergomena Lawrence Tax kuzungumza na wananchi kuhusu mgogoro wa Ardhi uliopo Kisakasaka baina ya wananchi na Jeshi la wananchi.
Waziri wa Ulinzi na Jeshi la kujenga  Taifa (JKT) Dkt.Stergomena Lawrence Tax akisikiliza maoni ya  Mwananchi kutoka Shehia ya Maungani Khatib Omar Khatib kuhusu mgogoro wa ardhi uliopo katika Shehia ya kisakasaka baina ya wananchi na Jeshi huko kisasaka katika kikao maalum cha kujadili mgogro huo.
Kamishna Msaidizi wa Milki Wizara ya Ulinzi na Jeshi la kujenga Taifa (JKT) Luteni Kanali  Yenu Mgugule akizungumza katika kikao maalum cha kujadili mgogoro wa Ardhi baina ya Jeshi na Wananchi huko Kisakasaka Wilaya ya Maghribi "B" Mkoa wa Mjini  magharibi .
Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya makaazi Joseph Kilangi akitolea ufafanuzi mgogoro wa ardhi baina ya wananchi na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) katika kikao maalum cha kujadili mgogoro huo,huko  kisakasaka Wilaya ya Magharibi “B” Mkoa wa Mjini Magharibi.

Na Faki Mjaka-Maelezo Zanzibar  10.03.2022

WAZIRI wa Ulinzi na Jeshi la kujenga Taifa, Dkt. Stergomena Lawrence Tax amefanya ziara Zanzibar kwa lengo la kumaliza mgogoro wa ardhi baina ya Jeshi la wananchi JWTZ na wananchi wanaopakana na eneo la Kambi ya Jeshi ya Kisakasaka Wilaya ya Magharib B Unguja.

 

Katika ziara hiyo Waziri Taxi alifanya mkutano wa hadhara uliowashirikisha viongozi mbalimbali wa serikali na wananchi wa shehia tatu za Kisakasaka, Maungani na Fuoni ili kumaliza mgogoro uliodumu kwa muda mrefu.

 

Waziri Tax alisema mkutano huo ni mwendelezo wa mipango ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar katika kuhakikisha wanamaliza migogoro ya ardhi nchini. 

 

“Serikali zetu zote mbili chini ya Mama Samia na Dkt. Mwinyi zimedhamiria kuyatatua matatizo ya ardhi nchini na ndio maana nimekuja hapa kushuhudia suluhu inavyoenda ya tatizo lililodumu kwa muda mrefu hapa Kisakasaka” alisema Waziri Tax.

 

Alieleza kuwa ili jeshi liweze kufanya kazi kwa ufanisi, linahitaji ardhi ya kutosha katika harakati zake ikiwemo eneo kubwa la mazoezi na uhifadhi wa Vifaa vya kijeshi hivyo wananchi wa maeneo yanayopakana na Kambi wanapaswa kutoa ushirikiano unaohitajika.

 

Waziri Tax alifafanua kuwa, katika hatua za kumaliza mgogoro huo wizara yake kwa kushirikiana na Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makaazi Zanzibar imefanikiwa kufanya zoezi la upimaji na kufanya tathmini ya maeneo 83 ya ardhi ambayo yanaendelea kufanyiwa kazi ili kukamilika kwa wakati. 

 

"Tayari utaratibu umekamilika, watendaji wapo katika hatua za mwisho kuandaa kitabu cha tathmini ili kila Mtu apate haki yake" alisema Waziri Tax.

 

Alibainisha kuwa Serikali kupitia Bunge la Jamuhuri ya Muungano limefanikiwa kutenga fedha kwenye Bajeti ya mwaka jana kwa ajili ya kukamilisha malipo ya wananchi walioathiriwa na mgogoro huo. 

 

Mkuu wa wilaya ya Magharib B, Hamida Mussa Khamisi aliwataka Wananchi hao kuiamini Serikali yao kuwa itaendelea kuwalipa fidia kama ilivyoahidi. 

 

Alisema tayari Serikali ya Jamhuri ya Muungano imeshatenga fedha katika Hazina yake kwa ajili ya kuwalipa fidia waathiriwa wa mgogoro huo.

 

“Zamani tulikuwa tunajiuliza nani atawajibika kutafuta Pesa kwa ajili ya fidia za wananchi hawa, bahati nzuri Serikali ya Jamhuri imeliona hilo na imetuhakikishia wananchi watapatiwa stahiki zao kwa wakati” alisema Bi Hamida.

 

Alisema pongezi za dhati zinapaswa kwenda kwa Rais Samia na Rais Mwinyi kwa kuonesha kwa vitendo juhudi zao za kutatua changamoto zinazowakabili wananchi hasa migogoro ya ardhi.

 

Nae Kamishna Msaidizi wa Miliki Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Luteni Kanali Yenu Mgugule alisema kuchukuliwa kwa baadhi ya maeneo yaliyopakana na Kambi za Jeshi kunatokana na kuengezeka kwa mahitaji ya kijeshi hasa katika zama za sayansi na teknolojia.

 

Alisema katika zoezi la upimaji na tathmini walizingatia zaidi haki za binadamu jambo ambalo litawafanya wananchi wengi wa eneo hilo kushukuru kwa haki zao.

 

Mapema katibu Mkuu wizara ya Ardhi na Makazi Zanzibar Joseph Kilangi, aliwaomba wananchi hao kutoa ushirikiano wa kutosha kwa viongozi katika kutatuwa migogoro hiyo.

 

Aidha aliwaomba wananchi hao kutojaribu kujiingiza tena katika maeneo yaliyopatiwa suluhu ili kuepuka matatizo yanayoweza kujitokeza.

 

Kwa upande wake Mwenyekiti wa kamati ya wananchi Khamisi vuai Makame aliwashukuru viongozi kwa kazi nzuri waliyoifanya na kuwaomba viongozi watekeleze yale waliyoahidi.

 

Ikumbukwe kuwa mgogoro kati ya Jeshi la Wanchi JWTZ na wanchi wa maeneo ya kisakasaka ulianza toka mwaka 1986 bila kupatiwa ufumbuzi. Kupitia utawala wa Rais Samia na Dkt. Mwinyi mgogoro huo umeshughulikiwa kikamilifu na upo katika hatua za mwisho ili kupatiwa suluhu ya kudumu.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.