Habari za Punde

Alhaj Dk.Hussein Ameipongeza Jumuiya ya Kuhufadhi Quran Tanzania.

 
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk. Hussein Ali Mwinyi ameipongeza Jumuiya ya Kuhifadhi Qurani Tanzania chini ya Mwenyekiti wake Sheikh Othman Aki Kaporo kwa kuweza kudumisha mashidnano hayo kwa kipindi cha miaka 30 sasa.

Rais Dk. Mwinyi alitoa pongezi hizo leo  katika hafla ya  Fainali ya Mashindano  ya Tuzo za Kimataifa za Mashindano ya Qurani yaliyofanyika katika ukumbi wa Diamond Jubilee, Dar es Salaam ambayo yaliwashirikisha washiriki 13 kutoka nchi za Burundi, Malaysia, Uturuki, Marekani, Urusi, Uganda, Kenya, Yemen, Pakistan, Morocco na wenyeji Tanzania.

Katika hotuba yake Alhaj Dk. Mwinyi alisema kuwa mashindano hayo yalianza kama mashindano madogo yakiwa na muonekano wa kikanda na Kitaifa lakini kutokana na nia thabiti za uongozi wa Jumuiya hiyo umeyaendeleza hadi yakapata umaarufu ambapo hivi sasa yanahusisha ngazi ya Kimataifa.

Alisema kuwa katika kipindi cha miaka 30 Jumuiya hiyo imekumbana na changamoto nyingi lakini kutokana na imani zao pamoja na subira wameweza kuzishinda. “Namuomba Mwenyezi Mungu awazidishie baraka kwa haya mambo mema mnayoyafanya”, alisema Dk. Mwinyi.

Aidha, alisema kuwa mashindano ya Qurani yamekuwa na mchango mkubwa katika kuwatayarisha Maulamaa na Maimamu wazuri wenye ufasaha wa kusoma na uwezo mkubwa wa kuhubiri mbele ya hadhara mbali mbali.

Aliongeza kuwa mashindano ya Qurani ya Kimataifa yamekuwa na mchango mkubwa katika kuitangaza Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kuipongeza Jumuiya hiyo kwa kuyasimamia na kuyaongoza mashindano hayo hasa ikizingatiwa kwamba yanawashirikisha washiriki kutoka mataifa mbali mbali duniani.

Alieleza jinsi alivyovutiwa na mipango na mikakati inayoendelezwa na Jumuiya hiyo katika kuimarisha elimu, malezi na ustawi wa watoto na jamii kwa jumla hatua ambayo imewezesha kuanzisha shule na kutoa huduma nyengine za jamii na kuzinasihi Jumuiya nyengine za kidini  kuiga mfano huo.

Alhaj Dk. Mwinyi alitumia fursa hiyo kuwapongeza kwa dhati washiriki wote kwa kuwa ameshuhudia kwamba wote wamefanya vizuri na kwa wale ambao hawakubahatika kupata zawadi aliwahimiza waondoke wakiwa na ari ya kutafuta ushindi katika mashindano yajayo.

Sambamba na hayo, Alhaj Dk. Mwinyi aliipongeza Jumuiya hiyo ya Kuhifadhi Qurani kwa kutimiza miaka 30 pamoja na mafanikio makubwa yaliyopatikana katika kipindi hicho huku akitumia fursa hiyo kuwashukuru wadhamini wa hafla hiyo iliyofana.

Pongezi maalum alizitoa kwa Jumuiya hiyo kwa juhudi zao za utunzaji mazingira ambapo imeonesha jinsi ilivyopokea vyema maagizo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan katika umuhimu wa utunzaji mazingira nchini.

Katika mashindano hayo mshindi wa kwanza katika Hifdhi Qurani kati ya washiriki 10 walioshindana mshindi wa mwanzo alikuwa Abdulhakim Naji Mohammed Ali kutoka Yemen aliyejikusanyia zawadi ya Dola za Kimarekani 5,000 ambapo washindi wa pili walikuwa wawili Ahmed Bashir Aden kutoka Marekani na Aiemiddin Farkhudinov kutoka Urusi  na mshindi wa tatu ni Abdulmalik Ramadhan Selemani kutoka Tanzania.

Katika mashindano ya Tajwid ambapo washiriki walikuwa watatu, mshindi wa kwanza alikuwa ni Ahmad Salumu Mkwewa kutoka Tanzania.

Nae Mufti Mkuu wa Tanzania Sheikh Abubakar Zubeir Bin Ally akitoa salamu zake aliipongeza Jumuiya hiyo pamoja na viongozi wake kwa kuendeleza mashindano hayo huku akisisitiza haja ya kuwajali na kuwasaidia walimu wa Qurani kwa kuwapa nguvu ili waongeze juhudi za kuwahifadhisha vijana Qurani.

Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo Othamn Ali Kaporo alitoa historia ya Jumuiya hiyo na kueleza jinsi hatua mbali mbali ilizopita hadi kufikia ilipo hivi sasa ambapo waumini mbali mbali wa dini ya Kiislamu wameshiriki katika kuiunga mkono wakiwemo viongozi mbali mbali wa Serikali.

Sheikh Salaah Akrabi akitoa maelezo mafupi ya miaka 30 ya Jumuiya hiyo iliyoanzishwa mwaka 1992, alisema kuwa mashirikiano ya pamoja ndio yaliyoifikisha Jumuiya hiyo hapo iliopo licha ya changamoto kadhaa ilizopitia.

Katika hafla hiyo, Tuzo mbali mbali zilitolewa kwa viongozi waliotoa michango yao katika kuiendeleza na kuiimarisha Jumuiya hiyo pamoja na wafadhili ambao wanaiunga mkono Jumuiya hiyo akiwemo Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk. Hussein Ali Mwinyi, Mzee Ali Hassan Mwinyi, Dk. Mohammed Kharib Bilal, Mufti Mkuu wa Tanzania Sheikh Sheikh Abubakar Zubeir, Mufti Mkuu wa Zanzibar Sheikh Saleh Omar Kabih, Sheikh Khalid Mfaume pamoja na viongozi wa Jumuiya hiyo na wengineo. Pia, tuzo zilitolewa kwa wadau wengine mbali mbali wakiwemo wanataaluma.

Imetayarishwa na Kitengo cha Habari,

Ikulu Zanzibar.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.