Habari za Punde

MAJALIWA ATAJA MAFANIKIO LUKUKI YA SERIKALI YA AWAMU YA SITA •Awasilisha mapitio na mwelekeo wa kazi za Serikali na makadirio ya mapato na matumizi ya fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na Bunge.

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ametaja mfanikio ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo pamoja na utoaji wa huduma za kijamii, huku akibainisha mafanikio makubwa yaliyopatikana katika Sekta mbalimbali.

Amesema Serikali inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan, imeshuhudia mafanikio makubwa katika kuimarisha miundombinu hususan barabara, reli, viwanja vya ndege, bandari, huduma za kiuchumi na kijamii, ujenzi wa madarasa, hospitali, zahanati na vituo vya afya, huduma za maji, utawala bora, mapambano dhidi ya rushwa na ufisadi, pamoja na kuhamasisha uwekezaji na utalii.

“Serikali itahakikisha sera za mapato na matumizi katika muda wa kati zinajikita katika kutekeleza vipaumbele vilivyoainishwa. Msukumo mkubwa utakuwa kuhakikisha usimamizi madhubuti wa fedha za umma na kuzielekeza kwenye maeneo yatakayoongeza tija, ajira na kuinua uchumi wa mwananchi mmoja mmoja. Aidha, Serikali itahakikisha miradi ya kipaumbele na kimkakati inayoendelea kutekelezwa inakamilika kwa wakati ikiwa ni pamoja na utekelezaji wa miradi mipya.”

Ameyasema hayo leo, (Jumtano Aprili 6 2022) Wakati akiwasilisha mapitio na mwelekeo wa kazi za Serikali na makadirio ya mapato na matumizi ya fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na Ofisi ya Bunge kwa Mwaka 2022/2023, Bungeni Jijini Dodoma.

Amesema Serikali ya Awamu ya sita itahakikisha miradi ya kipaumbele na kimkakati inayoendelea kutekelezwa inakamilika kwa wakati ikiwa ni pamoja na utekelezaji wa miradi mipya.

Waziri Mkuu ametaja miradi ya kimkakati inayotekelezwa na Serikali katika sekta ya miundombinu kuwa ni pamoja na Ujenzi wa Reli ya Kisasa kwa Kiwango cha Kimataifa (Standard Gauge Railway- SGR) ambapo ujenzi wa kipande cha Dar es Salaam - Morogoro (Km 300) umefikia asilimia 95.3,  kipande cha Morogoro - Makutupora (Km 422) asilimia 81.1; na Mwanza - Isaka (Km 341) umefikia asilimia 3.9.

Miradi mingine ni pamoja na  Utekelezaji wa Mradi wa Kufua Umeme wa Maji wa Julius Nyerere (Megawati 2,115) ambao umefikia asilimia 56.79, Kukamilika kwa ulipaji wa fidia katika maeneo ya kipaumbele ya Mradi wa Ujenzi wa Bomba la Mafuta Ghafi kutoka Hoima (Uganda) hadi Chongoleani - Tanga (Tanzania) pamoja na kusaini Mkataba kati ya Nchi Hodhi na Wawekezaji (Host Government Agreement - HGA) na Mkataba wa Ubia (Shareholding Agreement - SHA).

Waziri Mkuu alitanabaisha miradi mingine ambayo ni Ujenzi wa Barabara na Madaraja Makubwa ambapo ujenzi wa barabara ya mzunguko katika Jiji la Dodoma yenye urefu wa kilomita 112.3, Kuboresha Usafiri wa Abiria na Mizigo katika Maziwa Makuu, ujenzi wa viwanja vya ndege pamoja na uendelezaji wa ujenzi wa mji wa Serikali.

Amesema katika Sekta ya Elimu Serikali imeendelea kujenga miundombinu ya elimu kwa lengo la kuhakikisha watoto wanapata elimu katika mazingira bora na yenye staha.

“Kupitia utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano Dhidi ya UVIKO-19, tumefanikiwa kupunguza msongamano wa wanafunzi kwa kuongeza madarasa 12,000 katika shule za sekondari, madarasa 3,000 katika vituo shikizi na mabweni 50 kwa wanafunzi wenye ulemavu. Ujenzi huo wa vyumba vya madarasa umewezesha wanafunzi wote waliochaguliwa katika mwaka 2022 kujiunga na kidato cha kwanza kwa mkupuo mmoja. Kitendo hiki ni utekelezaji wa Ilani ya CCM ya Mwaka 2020 inayotaka upatikanaji wa elimu hapa nchini uimarishwe kwa kujenga miundombinu ya kutosha na usawa katika utoaji wa elimu.”

Aliongeza kuwa Serikali imeendelea kuimarisha upatikanaji wa elimu ya juu kwa kuongeza fedha za mikopo kwa ajili ya wanafunzi ambapo katika mwaka 2021/2022, jumla ya shilingi bilioni 570 zimetumika ikilinganishwa na shilingi bilioni 464 zilizotumika mwaka 2020/2021. Vilevile, idadi ya wanufaika imeongezeka kutoka 149,398 mwaka 2020/2021 hadi wanafunzi 177,605 mwaka 2021/2022.

Amesema katika sekta ya Afya serikali imeendelea na ukarabati wa miundombinu ya kutolea huduma za afya nchini, Miundombinu hiyo, inahusisha hospitali za rufaa za kanda, hospitali za rufaa za mikoa, hospitali za halmashauri, vituo vya afya na zahanati.

Kuhusu ukuaji wa uchumi katika kipindi cha Januari hadi Septemba, 2021, amesema uchumi wa Taifa ulikua kwa asilimia 4.9 ikilinganishwa na ukuaji wa asilimia 4.8 katika kipindi kama hicho mwaka 2020.

“Kuongezeka kwa kasi ya ukuaji kumetokana na jitihada mbalimbali zinazoendelea kuchukuliwa na Serikali ikiwemo utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano Dhidi ya UVIKO - 19 na miradi mbalimbali ya maendeleo.”

Majaliwa amesema Serikali ya Awamu ya Sita imeendelea kufanya maboresho makubwa katika Sekta ya Kilimo ambapo mwezi Desemba 2021, Serikali ya Awamu ya Sita iliipatia Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania mtaji wa shilingi bilioni 208 ikiwa ni nyongeza kwenye mtaji wa awali wa shilingi bilioni 60 uliowekwa na Serikali wakati wa uanzishwaji wa benki mwaka 2012.

Waziri Mkuu amesema Serikali imeendelea kusimamia kikamilifu sekta ya madini na kuhakikisha inakuwa na mchango mkubwa kwenye Pato la Taifa ambapo Mchango wa sekta ya madini katika kipindi cha Januari hadi Septemba umeongezeka kutoka asilimia 6.5 mwaka 2020 hadi kufikia asilimia 7.3 mwaka 2021. Na kuiwezesha Serikali kukusanya kiasi cha shilingi bilioni 406.6 za maduhuli sawa na asilimia 62.6 ya lengo la kukusanya shilingi bilioni 650 kwa mwaka.

“Mafanikio hayo ni kielelezo tosha cha kuendelea kuimarika kwa sekta hii kufuatia usimamizi thabiti unaowekwa na Serikali.”

Kuhusu utekelezaji wa miradi ya maji amesema Serikali ina dhamira ya dhati kuhakikisha upatikanaji wa huduma ya maji mijini na vijijini unafika zaidi ya wastani wa asilimia 95 na 85 mtawalia ifikapo mwaka 2025.

“Hadi Februari, 2022, hali ya upatikanaji wa maji safi maeneo ya mijini imefikia asilimia 86. Aidha, kati ya miradi 114 inayotekelezwa katika maeneo mbalimbali, miradi 40 imekamilika na kuanza kutoa huduma kwa wananchi wapatao 1,978,730 na miradi 74 ipo katika hatua mbalimbali za utekelezaji.”

Waziri Mkuu pia amewashukuru washirika wa maendeleo zikiwemo nchi rafiki, taasisi na mashirika ya kimataifa, madhehebu ya dini na mashirika yasiyo ya kiserikali kwa kuendelea kuunga mkono juhudi za Serikali kujenga uchumi shindani na viwanda na kuiletea nchi maendeleo.

“Mchango wao umekuwa muhimu katika kuiwezesha nchi yetu kupiga hatua kubwa kimaendeleo kulingana na mipango tuliyojiwekea.”

(Mwisho)

IMETOLEWA NA:

OFISI YA WAZIRI MKUU,

S. L. P. 980,

41193 – DODOMA,

JUMATANO, APRIL 6, 2022.


No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.