Habari za Punde

Maslahi ya Madaktari Wahudumu na Wafanyakazi wa Kada ya Afya Kuimarishwa Maslahi Yao.

 

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akihutubia na kulifungua  Kongamano la Pili la Madaktari na Wahudumu wa Afya lililofanyika katika ukumbi wa Chuo cha Utalii Maruhubi Unguja Jijini Zanzibar, lililoandaliwa na Taasisi ya Jamiyyatul Akhlaqul Islaamia (JAI) na kuwashirikisha Madaktari.Wauguzi,watoa huduma ya Afya na Masheikh.(Picha na Ikulu)

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk. Hussein Ali Mwinyi amesisitiza kuwa ahadi ya Serikali katika kuimarisha maslahi ya madaktari, wahudumu na wafanyakazi wa kada ya Afya nchini; kuwa ipo pale pale na itatekelezwa mapema iwezekanavyo.

Alhaj Dk. Mwinyi amesema hayo katika ufunguzi wa kongamano la Pili la Madaktari na wahudumu wa Afya, lililofanyika katika ukumbi wa Chuo cha Utalii Maruhubi, Jijini Zanzibar.

Amesema kwa kutambua kazi kubwa inayofanywa na madaktari, wahudumu na wafanyakazi wa Kada ya Afya, Serikali imeweka mazingatio maalum katika kuimarisha stahiki zao, ili kuimarisha utendaji wa kazi.

Alisema  baada ya kupitia upya maslahi ya wafanyakazi wa sekta ya Afya Zanzibar imebainika kuwa hayaendani na ‘scheme of service’ na kubainisha miongoni mwa kasoro iliopo ni ile ya wafanyakazi wa muda mrefu kupata maslahi duni, hivyo akabainisha hatua ya Serikali ya kutoa maslahi maslahi kuambatana na ‘scheme of service’.

Alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeweka kipaumbele katika kuimarisha sekta ya Afya, ikianzia na uimarishaji wa miundombinu kwa kuhakikisha kila Wilaya inakuwa na Hospitali ya kisasa ili kuwaondolea usumbufu wananachi kufuata matibabu nje za Wilaya zao wanazoishi.

Alhaj DFk. Mwinyi alisema Serikali inaendelea na kazi ya kuimarisha mifumo ya utoaji wa huduma pamoja na kugharamia upatikanaji wa Huduma za Afya kupitia mfumo wa Bima ya Afya.

“Dhamira ya Serikali ni kuongeza Bajeti ya Wizara ya Afya kila mwaka ili kuwa  na uwezo wa kununua madawa na vifaa tiba, kusomesha madaktari na wauguzi pamoja na kuongeza idadi ya madaktari Bingwa na wafanyakazi mbali mbali, sambamba kupunguza idadi ya wagonjwa wanaopelekwa  nje ya nchi kwa matibabu”, alisema.

Alisema mipango hiyo inafanikishwa kutokana na kuvutia wawekezaji pamoja na kujenga mashirikiano kati yake  na Sekta binafsi.

Rais Alhaj Dk. Mwinyi alisema ushirikiano unaoendelea kati ya Taasisi ya Jamiiyatul Akhalaqul Islamia (JAI) na Serikali zote mbili, unakwenda sambamba na malengo ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuimarisha sekta ya Afya nchini.

Alisema amevutiwa sana na kaulimbiu ya Kongamano hilo isemayo ‘malipo ya wema ni wema’ na kubainisha mafundisho na mazingatio makubwa yaliomo ndani yake  kwa madaktari na wauguzi;  kuwa wana dhima ya kutoa huduma muhimu za afya katika mazingira mbali mbali .

Alisema kauli mbiu hiyo inaakisi pamoja na watendaji hao kutegemea malipo kutoka kwa waajiri wao kutokana na huduma wanazotoa, lakini pia wanapaswa kuwa na nia njema ya kujitolea huku wakitegemea malipo bora zaidi kutoka kwa Mweneyzi Mungu.

Rais Dk. Mwinyi aliihakikishia JAI kuwa Serikali itaendelea kuiunga mkono ili iweze kutekeleza malengo yake ipasavyo na kubainisha kutiwa moyo na mafanikio  yaliokwisha kupatikana tangu kuanzishwa kwa taasisi hiyo .

Aidha, aliipongeza Taasisi hiyo kwa hatua ayke ya kushirikiana na Wizara Afya na Utibabu kuandaa kongamano hilo na kusema Serikali inathamini juhudi za taasisi  katika shughuli mbali mbali zinazolenga  kuimarisha sekta ya Afya nchini.

Nae, Waziri wa Afya na Utibabu Ahmeid Nassor Mazrui alisema   Wizara ya Afya na Utibabu imekuwa ikitupiwa lawama nyingi dhidi ya Wauguzi wake kutokana na dosari mbali mbali wanazozionyesha katika utendaji wao, ikiwemo utoaji wa kauli mbaya kwa wagonjwa, hivyo akabainisha haja ya kuwapa mawaidha watendaji hao ili kufanya kazi zao kwa weledi na uadilifu.

Alieleza kuwa ipo haja ya kupandishwa daraja utoaji wa huduma kwa wagonjwa ili kuwajenga imani.

Alisema wakati Serikali ikijiandaa kuingia katika mpango wa utoaji wa a Huduma ya Bima ya Afya, kuna umuhimu kwa watendaji wa Wizara hiyo, ikiwemo Madaktari na Wauguzi kutoa huduma bora, huku akibainisha kuwepo watendaji wanaowajibika na kundi la wasiowajibika, hivyo akasisitiza umuhimu wa kubadili tabia.

Alisema Kongamno hilo litasaidia sana kuwapa imani wananchi, huku akiwataka wauguzi kujitathmin ili kuweza kutoa kutoa huduma bora kwa jamii.

Aidha, akiwasilisha Risala ya Taasisi ya Jamiiyatul AkhlaqulIslamia (JAI), Naibu Katibu Mkuu JAI Sheikh Khalid Rajab alisema lengo la Kongamano hilo ni kuwaita Madaktari na Wauguzi pamoja na wafanyakazi wa Kada ya Afya, kuangalia namna bora ya kufanyakazi zao kwa misingi ya Dini ya Kiislamu.

Katika hatua nyengine, akizungumza katika Kongamano hilo Prof. Assad Mussa Assad  aliwataka watendaji wa Kada ya Afya (professionals) kuisoma  Dini yao ili kuipa thamani yake huku akiwataka  wale waliokwisha kuelimika kuwafunza wengine pamoja na kuifanyia kazi dini hiyo.

Alitumia fursa hiyo kusisitiza umuhimu wa watendaji hao kuwahimiza vijana kushiriki katika shughuli hizo.

Kongamano la Pili la Madaktari na wahudumu wa Afya, limeandaliwa kwa ushirikiano kati ya JAI na Wizara ya Afya na Utibabu na kuwashirikisha  Madakrati, wauguzi, wafanyakazi wa Hospitali za Serikali , binafsi pamoja na Vikosi vya SMZ  , Wakuu w aMabaraza ya Madaktari, Wanafunzi kutoka Vyuo Vikuu vinavyotoa elimu ya Huduma  ya Afya pamoja Wawakilishi w ataasisi mbali mbali.

Abdi Shamna, Ikulu Zanzibar

Postal Address: 2422 Tel.:0777476982. Fax: 024 2231822 

 E-mail: abdya062@gmail.com

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.