Na. Mwandishi wetu.
Kamishna wa Bodi ya
Mapato Zanzibar (ZRB) Ndg. Yussuph Juma Mwenda amesema kuwa ZRB haitamvumilia
wala kumfumbia macho mlipakodi yeyote ambaye aidha halipi kodi au analipa
viwango vidogo kinyume na uhalisia wa biashara yake inavyofanyika.
Ameyabainisha hayo
wakati alipofanya ziara ya kikazi kukagua Hotel ya The Residence inayomikiwa na
kampuni ya Hotel and Property ambayo ina hadhi ya nyota tano huko Mchangamle
Mkoa wa Kusini Unguja.
Kamishna Mwenda
amesema kuwa, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ina nia njema na Wazanzibari kwa
kuwaalika wawekezaji kuja kuwekeza Zanzibar, hivyo kukamilika na kufanya kazi
kwa miradi hiyo ya uwekezaji kuwe na ufanisi katika ulipaji wa kodi ili
wananchi wapate tija kutokana na uwekezaji huo.
Aidha, Ndugu Mwenda ameueleza
uongozi wa The Residence kuwa viwango vya kodi vinavyowasilisha ZRB na Hoteli
hiyo haviridhishi, hivyo amewataka kuhakikisha kuwa wanaunganisha mifumo yao ya
kibiashara pamoja na mfumo wa ZRB wa kutolea risiti za kielektroniki (VFMS) haraka
iwezekanavyo ili kuondoa mianya ya upotevu wa mapato.
Kwa upande wa
wasimamizi wa Hotel hiyo, wakiwakilishwa na Ndg. Diocles Ishengoma wamesema
kuwa miundombinu ya barabara ambayo watalii wanaitumia kufika katika Hoteli
hiyo sio rafiki jambo linalokwaza katika usafirishaji wa wageni.
Katika ziara hiyo, Kamishna Mwenda pia alitembelea ofisi za ZRB zilizopo Paje, na kuwaahidi watendaji walioko kituoni hapo kuwa uongozi utaiongezea uwezo ofisi hiyo ili iweze kuwahudumia walipakodi wote wa Mkoa wa Kusini Unguja kwa ufanisi.
No comments:
Post a Comment