RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk.Hussein Ali Mwinyi akiitikia dua ikisomwa na Mufti Mkuu wa Zanzibar Sheikh.Saleh Omar Kabi (kulia kwa Rais) baada ya kumalizika kwa Sala ya Ijumaa iliyofanyika katika Masjid Barwan Mlandege Unguja Jijini Zanzibar leo 20-5-2022.(Picha na Ikulu)
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk.Husssein Ali Mwinyi akiwa katika viwanja vya Masjid Barwan Mlandege Unguja Jijini Zanzibar akiondoka baada ya kumalizika kwa Sala ya Ijumaa iliyofanyika katika msikiti huo leo 20-5-2022 na (kushoto kwa Rais) Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja Mhe.Idrisa Mustafa Kitwana.(Picha na Ikulu)
STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar 20.05.2022
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj
Dk. Hussein Ali Mwinyi amesema kuna
umuhimu wa kuliombea dua Taifa, wakati huu Dunia ikikabiliwa na msukosuko wa
kiuchumi unaotokana na vita vinavyoendelea kati ya Russia na Ukrane.
Dk. Mwinyi amesema hayo katika salamu alizotoa kwa waumini waliohudhuria Ibada ya Sala ya Ijumaa iliofanyika Masjid Barwani Mlandege, Jijini Zanzibar.
Alisema wakati huu Dunia ikipita katika msukosuko wa kiuchumi unaotokana na vita vinavyoendelea kati ya Russia na Ukrane na kusababisha baadhi ya bidhaa muhimu kuadimika sambamba na kuongezeka bei, kuna umuhimu wa jamii kuiombea dua nchi pamoja na Viongozi wake ili kuvuka salama katika hali hiyo.
Alisema baadhi ya nchi za Ulaya, Bara Hindi na Mashariki ya mbali zimefunga usafirishaji wa bidhaa inazozalisha, kama vile unga wa ngano, mafuta ya kupikia pamoja Petroli na badala yake kutumia wenyewe na hivyo kusababisha upungufu wa bidhaa hizo duniani.
Alieleza hatua hiyo imesabahisha mfumko wa bei na kuongeza ugumu wa maisha katika jamii.
Alhaj Dk. Mwinyi alisema Serikali inafanya kila juhudi na kuchukua hatua mbali mbali ili kupunguza athari zitokanazo na tatizo hilo.
Aidha, Alhaj Mwinyi aligusia matatizo yaliomo katika jamii yanayosababishwa na baadhi ya wananchi kujihusisha na vitendo viovu, ikiwemo udhalilishaji wa kijinsia, uingizaji;uuzaji na matumizi ya dawa za kulevya pamoja na wizi na kusema juhudi za pamoja zinahitajika kati ya Jamii na Serikali ili kukabiliana na vitendo hivyo.
Nae, Katibu Mtendaji Ofisi ya Mufti wa Zanzibar, Sheikh Khalid Ali Mfaume alisisisitiza umuhimu wa waislamu kukamilisha ibada ya funga ya sita katika mwezi huu wa Shawwal, baada ya kuhitimisha ibada ya funga ya Ramadhani.
Mapema, Khatibu katika sala hiyo ya Ijumaa Sheikh Ali Suleiman aliwakumbusha waislamu umuhimu wa kumpwekesha Mwenyezi Mungu kwa kuondokana na vitendo vya shirki.
Alitumia fursa hiyo kuelezea hadithi ya Mtume Muhammad (SAW) akibainisha madhambi makubwa ya kumshirikisha Mungu, sambamba na kusema Quraan imeeleza kuwa jambo hilo ni sababu ya kuporomoka kwa amali zote za mja.
Alisema njia pekee ya mja kupata mafanikio mema Duniani na akhera ni kuacha kumshirikisha Mwenyezi Mungu.
Wakati huo huo, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk. Mwinyi alipata fursa ya kuwatembelea wagonjwa Bi Hasina Bint Gharib na Bwana Omar Haji Omar waliolazwa kutokana na magonjwa tofauti katika Hospitali ya Rufaa Mnazi mmoja, jijini hapa.
Imetayarishwa na Idara ya Mawasiliano
Ikulu Zanzibar.
No comments:
Post a Comment