Habari za Punde

Serikali ya Ujerumani Yaahidi Kuendelea Kushirikiana na Tanzania katika Uhifadhi.

 
Naibu Katibu Mkuu wa Maliasili na Utalii, Juma Selemani Mkomi akizungumza na Mkuu wa Ushirikiano wa Maendeleo kutoka Ubalozi wa Ujerumani hapa nchini DktKatrin Bornemann wakati alipokutana leo Jijini Dodoma kwa ajili ya mazungumzo ya kuimarisha ushirikiano katika shughuli za Uhifadhini nchini

Serikali ya Ujerumani imeahidi kuendelea kushirikiana na Tanzania katika hatua zake za kukuza  na kuendeleza shughuli za Uhifadhi kupitia miradi mbalimbali ambayo nchi hiyo inafadhili katika sekta ya wanyamapori

Hayo yamebainishwa leo Jijini Dodoma  na Naibu Katibu Mkuu wa Maliasili na Utalii, Juma Selemani Mkomi, alipokutana na kufanya mazungumzo na Mkuu wa Ushirikiano wa Maendeleo kutoka Ubalozi wa Ujerumani hapa nchini DktKatrin Bornemann.

Amesema Serikali ya Ujerumani ni miongoni mwa wadau wakubwa wa shuguli za Uhifadhi hapa nchini na wamekuwa wakifadhili miradi mbalimbali ya Uhifadhi inayosaidia  kuleta ustawi wa wanyamapori.

“Serikali ya Ujerumani imeahidi kwamba itaendelea kushirikiana na Tanzania kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo katika sekta ya wanyamapori hususan ujangili na mabadiliko ya tabia nchi ” amesema Naibu Katibu Mkuu Mkomi.

Amesema licha ya  Serikali ya Ujerumani katika kipindi cha miaka mitano iliyopita kuweza  kufadhili miradi mbalimbali  ya uhifadhi kwa kutoa kiasi cha jumla ya shilingi milioni 350 imesema itashirikiana zaidi na Tanzania katika kuhakikisha maisha ya wananchi wanaoishi karibu na maeneo ya Hifadhi  yanaendelea kuboreka 

Kwa upande wake Mkuu wa Ushirikiano wa Maendeleo kutoka Ubalozi wa Ujerumani hapa nchini DktKatrin Bornemann amesema kuwa  nchi yake imeridhishwa na utekelezaji wa miradi inayofadhiliwa na nchi yake ikiwemo vita dhidi ya ujangili 

Kufuatia hali hiyo Dkt.Katrin amesema  kuwa nchi yake itaendelea kusaidia shughuli za uhifadhi ikiwemo Mpango wa Usimamizi wa migogoro kati ya Binadamu na Wanyamapori  ili kuzipunguzia umasikini Jamii za Watanzania wanaoishi karibu na maeneo ya Hifadhi 
 
" Moja ya shabaha yetu kama nchi wahisani ni kuhakikisha kuwa wananchi wanaoishi karibu na maeneo ya Hifadhi  hawaathiriwi na  wanyamapori wakali na waharibifu" amesisitiza Dkt.Katrin

Kwa sasa miradi inayoendelea iliyofadhiliwa na  Serikali ya Ujerumani katika sekta ya Uhifadhi ni mfumo wa Ikolojia wa Serengeti, Selous na Mfumo wa Ikolojia wa Katavi-Mahale.
Mkuu wa Ushirikiano wa Maendeleo kutoka Ubalozi wa Ujerumani hapa nchini DktKatrin Bornemann akizungumza na Katibu Mkuu wa Maliasili na Utalii, Juma Selemani Mkomi ambapo amesema nchi yake itaendelea kufadhili miradi mbalimbali ya shughuli za Uhifadhi hapa nchini.
Naibu Katibu Mkuu wa Maliasili na Utalii, Juma Selemani Mkoni akizungumza na  Mkuu wa Ushirikiano wa Maendeleo kutoka Ubalozi wa Ujerumani hapa nchini DktKatrin Bornemann mara baada ya kikao ambapo Serikali ya Ujeruman yaahidi kuendelea kushirikiana na Tanzania katika shughuli za Uhifadhi
Naibu Katibu Mkuu wa Maliasili na Utalii, Juma Selemani (katikati)  Mkoni akizungumza na  Mkuu wa Ushirikiano wa Maendeleo kutoka Ubalozi wa Ujerumani hapa nchini DktKatrin Bornemann akiwa na Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu, Prisca Lwangili mara baada ya kikao ambapo Serikali ya Ujerumani yaahidi kuendelea kushirikiana na Tanzania katika shughuli za Uhifadhi
Naibu Katibu Mkuu wa Maliasili na Utalii,Juma Selemani Mkoni akiwa kwenye picha ya pamoja naMkuu wa Ushirikiano wa Maendeleo kutoka Ubalozi wa Ujerumani hapa nchini DktKatrin Bornemann, Wengine ni Watumishi kutoka Idara za Wizara ya Maliasili na Utalii.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.