Habari za Punde

Umilikishaji wa Ardhi Kuondoa Changamoto kwa Wanawake -- Naibu Waziri Mhe. Ridhiwani.

Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Ridhiwani Kikwete akionesha Hati ya umiliki wa pamoja ya mume na mke ya mkazi wa Mbalizi (kulia) wakati wa zoezi la kutoa hati za ardhi kwa wananchi wa Mbalizi waliokamilisha taratibu za kumilikshwa katika mradi wa Kupanga, Kupima na Kumilikisha Ardhi katika Halmashauri ya Mbeya 

Na Anthony Ishengoma na Munir Shemweta, WANMM MBEYA

Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi  Ridhiwani Kikwete amesema faida kubwa na kipaumbele katika zoezi la Kupanga, Kupima na Kumilikisha ardhi ni kupambana na ukatili dhidi ya wanawake ikiwemo kuondoa changamoto ya akina mama kukosa nguvu ya kumiliki ardhi haki aliyoieleza kuwa itapatikana kwa kutoa hati ya pamoja kati ya mume na mke.  

Naibu Waziri Kikwete amesema hayo Mei 13, 2022 wakati akihutubia wananchi wa Mbalizi Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya wakati wa uzinduzi wa mradi wa Kupanga, Kupima na Kumilikishwa ardhi unaosimamiwa na Chuo cha Ardhi Morogoro (ARIMO) na baadae kushiriki zoezi la ugawaji hati kwa wananchi waliokamilisha taratibu za kumilikishwa ardhi.

Aidha, ameongeza kwa kusema kuwa, Kupima ardhi kutawezesha kutatua migogoro isiyo ya razima kwa kuwa kazi hiyo inahusisha upimaji shirikishi ambao baada ya wataalamu kujiridhisha wakati wa zoezi hilo hati hutolewa bila ya kuwepo migogoro yoyote.

‘’Kumekuwepo na spidi ndogo ya wananchi kwenda kuchukua hati zao lakini niwambie ninyi kuna wakati utafika mutahitaji kulima kadiri ya taratibu za serikali na kuepuka uharibifu wa mazingira kuna wakati itabidi zitumike mbinu za kitaalam ili kuendelea na kilimo.’’Aliongeza  Ridhiwani Kikwete Naibu Waziri Wizara ya Ardhi.

Naibu Waziri Ridhiwani alizitaja faida za kuwa na hati kuwa ni pamoja na kuthaminiwa na kupatiwa uhakika wa kupata huduma za kibenki kwa mmiliki, kuongeza thamani ya ardhi tofauti na ile ardhi isiyopimwa aliyoieleza kuwa haina thamani yoyote hapa nchini.

Kwa upande wake Mkuu wa Chuo Ardhi Morogoro (ARIMO) Bw. Huruma Lugalla amesema chuo chake kilikopeshwa kiasi cha Tsh. Bil 1.2 kwa ajili ya program ya Kupima, Kupanga na Kumilikisha Ardhi kwa wakazi wa Mbalizi mkoani Mbeya ambapo viwanja takribani 35,000 tayari vimepimwa.

Kwa mujibu wa Lugala, kiasi hicho cha fedha walizopatiwa tayari kimewezesha upimaji na utambuzi wa viwanja 31,06 sawa na 89% katika lengo lililokusudiwa.

Aidha Mkuu huyo wa Chuo cha Ardhi Morogoro, aliongeza kuwa upimaji wa viwanja hivyo ulienda sawia na uandaaji wa michoro ya mipango miji na tayari michoro 108 kati ya 120 ambayo ni sawa na asilimia 90% imesanifiwa na kati ya hiyo michoro 80 imewasilishwa ofisi ya Kamishna wa Ardhi wa Mkoa kwa ajili ya idhini. 

Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Ridhiwani Kikwete ambaye amehitimisha ziara yake ya siku mbili mkoani Mbeya alisema zaidi ya Bil. 3 zimefika katika mkoa wa Mbeya kwa lengo la Kupima, Kupanga na Kumilikisha ardhi na kusimamiwa  vizuri na watendaji wa serikali na kukabidhi hati kwa wananchi wa Mbalizi waliokamilisha taratibu za kumilikishwa ardhi.

Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Ridhiwani Kikwete akizungumza wakati wa zoezi la kutoa hati za ardhi kwa wananchi wa Mbalizi waliokamilisha taratibu za kumilikshwa katika mradi wa Kupanga, Kupima na Kumilikisha Ardhi katika Halmashauri ya Mbeya
Sehemu ya wananchi wa Mbalizi katika Halmashauri ya Mbeya waliojitokeza katika zoezi la utoaji hati za ardhi lililofanywa na Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Ridhiwani Kikwete.
Mkuu wa Chuo cha Ardhi Morogoro (ARIMO) Huruma Lugala akizungumza wakati wa zoezi la kutoa hati za ardhi kwa wananchi wa Mbalizi waliokamilisha taratibu za kumilikshwa kwenye Mradi wa Kupanga, Kupima na Kumilikisha Ardhi katika Halmashauri ya Mbeya 
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Ridhiwani Kikwete akimkabidhi Hati ya Ardhi mkazi wa Mbalizi Paulo Mwayinga wakati wa zoezi la kutoa hati za ardhi kwa wananchi wa Mbalizi waliokamilisha taratibu za kumilikshwa kwenye Mradi wa Kupanga, Kupima na Kumilikisha Ardhi katika Halmashauri ya Mbeya.
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Ridhiwani Kikwete akiwa katika picha ya pamoja na wananchi wa Mbalizi mkoani Mbeya baada ya kuwakabidhi hati za ardhi kupitia program ya Kupanga, Kupima na Kumilikisha Ardhi katika Halmashauri ya Mbeya.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.